22.5 C
Dar es Salaam
Sunday, May 5, 2024

Contact us: [email protected]

TPDC MHIMILI WA MAPINDUZI YA VIWANDA NCHINI

Sehemu ya viunganishi vya bomba la gesi asilia

Na Mwandishi Wetu

TANZANIA ya leo imebeba kaulimbiu ya “Tanzania ya Viwanda”, hiyo ndiyo dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ambayo ina imani kubwa kuwa ili wananchi wake waweze kupata maendeleo ya kweli, Taifa linahitaji kuwa na viwanda vya kutosha.

Ni ukweli usiopingika kuwa viwanda ni gurudumu la kweli la mageuzi ya kiuchumi ya taifa lolote duniani ndiyo sababu hata kwenye historia ya uchumi wa dunia “mapinduzi ya viwanda” yalitoa maana nyingine kabisa ya maisha ya binadamu kimapato, maendeleo na uchumi.

Sekta ya viwanda Tanzania si ngeni kwa kuwa ilianza toka kipindi cha Serikali ya Awamu ya Kwanza ambapo Mwalimu Nyerere aliamini namna pekee ya kuboresha mazao yetu katika soko la ndani na soko la dunia ni kuyaboresha kupitia viwanda vyetu lakini pia ni viwanda vinachochea sekta nyingine kukua kwa haraka pamoja na kutoa fursa nyingi kwa Watanzania kuajiriwa kwenye viwanda hivyo.

Ujenzi wa viwanda nchini hutegemea vitu vingi ambavyo tunaweza kuviita vivutio vya uwekezaji ambavyo vinaweza kuwa sera rafiki ya Serikali kwa wawekezaji, uwepo wa malighafi, ardhi, soko, usafirishaji, nguvu kazi, utulivu wa nchi pamoja na uwepo wa nishati ya uhakika na gharama rafiki katika uzalishaji.

Tanzania kama nchi tumekuwa na vivutio vyote kasoro uwepo wa nishati ya kutosha, uhakika na kwa bei rafiki katika uwekezaji ili kuweza kuzalisha bidhaa zitakazokuwa na bei ya kiushindani sokoni.

Nishati ilitokea kuwa tatizo hasa baada ya mabadiliko ya tabia nchi ambapo mabwawa ambayo tumekuwa tukiyategemea kuzalishia umeme kuanza kupungua kina kwa kasi hadi kufikia hatua kusitishwa kuzalisha umeme na kupelekea nchi kuanza kuagiza mafuta na kutumia majenereta ya mafuta kuzalishia umeme ili uweze kutumika pia viwandani.

Pia viwanda vikubwa vililazimika kujenga mitambo ya kufua umeme kwa kutumia mafuta mazito ama dizeli.

Kwa kuwa mafuta haya yalikuwa yakiagizwa kutoka nchi zinazozalisha mafuta duniani iliipelekea taifa kutumia gharama kubwa kununua mafuta hayo na hivyo kupelekea gharama ya nishati kuwa ghali nchini na hivyo kuiondolea sifa kubwa ya upatikanaji wa nishati ya kutosha, uhakika na yenye bei rafiki hasa kwa viwanda.

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), wao wanasema ndio mashujaa katika kuijenga Tanzania ya viwanda katika mahojiano ya kuelekea kumbukumbu ya Mw. Julius K. Nyerere, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mhandisi Kapuulya Musomba, analiongelea Shirika analoliongoza kama Msingi wa Uchumi wa Viwanda Tanzania.

“Ni kazi kwa wananchi kuelewa moja kwa moja mchango wa TPDC katika uchumi wa viwanda wa nchi yetu kwa kuwa sisi ni msingi maana tunawezesha mfano Tanesco kuzalisha umeme kwa matumizi ya nchi na hivyo wananchi wataona tu umeme upo wa kutosha lakini jambo tunalojivunia sisi kama TPDC ni kuona tunachangia zaidi ya asilimia 50 ya umeme unaozalishwa kwenye gridi ya Taifa,” alieleza Mhandisi Musomba.

Akijibu swali kuhusu namna ambavyo TPDC inavyomuenzi Baba wa Taifa Injinia Musomba alieleza: “Mwalimu alivutiwa sana na uchumi wa viwanda na hivyo alijitahidi kuona Tanzania inakuwa Taifa huru kiuchumi kwa kuwa na viwanda vya kutosha na sisi kama TPDC tunaona fahari kuwa sehemu kubwa ya utekelezaji wa malengo ya Baba wa Taifa ambayo pia yamerudi upya kupitia Serikali ya Awamu ya Tano ambapo Rais wetu John Magufuli, ameonyesha nia ya dhati ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda kwa kuhakikisha nishati safi ya gesi asilia, ya uhakika na bei ya  kiushindani sokoni.”

Alisema TPDC baada ya kukamilika kwa miundombinu ya Taifa ya uchakataji na usafirishaji wa gesi asilia kutoka Madimba-Mtwara na Songo Songo-Lindi hadi Dar es Salaam, kumechochea kwa kiasi kikubwa uwekezaji wa viwanda katika maeneo ambayo miundombinu hiyo imepita na hii ni kwa sababu bomba la gesi asilia linaruhusu matoleo ya gesi asilia kwa matumizi mbalimbali ya viwanda na mfano mzuri ni kiwanda cha vigae cha Goodwill kilichopo mkoani Pwani wilayani Mkuranga ambacho tayari kinatumia gesi asilia pamoja na kiwanda cha Dangote ambacho shughuli za uunganishaji wa gesi asilia katika kiwanda hicho kutoka kwenye bomba kubwa zinaendelea.

Akielezea matumizi ya gesi asilia viwandani Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mkondo wa Chini TPDC, Emmanuel Gilbert, alisema:

“Ni jambo la kujivunia kwetu kama TPDC kuona tumefanikiwa kuunganisha gesi asilia ndani ya muda na kiwango kwa mujibu wa mkataba kwa kiwanda cha vigae cha Goowill ambacho mahitaji ya gesi kwa kiwanda ni kiasi cha futi za ujazo milioni 7 za gesi kwa siku kwa awamu ya kwanza na baadaye itafikia futi za ujazo milioni 10 kwa siku.”

“Mafanikio ya mradi huu imewezesha Serikali kuongeza pato la Taifa kutokana na kodi zitokanazo na mauzo ya bidhaa hii ya vigae ndani na nje ya nchi, pia kupunguza matumizi ya fedha za kigeni zilizokuwa zikitumika kuagiza bidhaa hizo nje ya nchi bila kusahau kuongeza nguvu katika harakati za kutengeneza Tanzania ya viwanda pamoja na kutoa ajira kwa Watanzania,” alifafanua  Kaimu Mkurugenzi huyo.

Katika juhudi za kujenga uchumi wa viwanda nchini, Emmanuel, ameeleza kuwa TPDC imefikia makubaliano ya kuingia mkataba wa mauziano ya gesi na kiwanda cha kuzalisha saruji cha Dangote kilichopo katika Mkoa wa Mtwara.  Mradi wa kuweka miundombinu ya kupeleka gesi kiwandani umegawanyika katika sehemu kuu mbili ambapo sehemu ya kwanza inahusisha kufikisha gesi asilia katika mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura na mahitaji yatakuwa futi za ujazo milioni 8 kwa siku. Katika hatua hii ujenzi wa bomba la kepeleka gesi lenye urefu wa mita 100 kutoka katika maungio ya bomba kuu la kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam (Blocj Valve Station – BVS 1) mpaka sehemu ya kuzalishia umeme kwa ajili ya kiwanda umekwishakamilika.

“Katika hatua ya pili ya mradi huu, itahusisha ujenzi wa bomba lenye urefu wa kilomita 2.7 kutoka BVS 1 mpaka kiwandani kwa ajili ya matumizi ya kuzalisha umeme wa muda mrefu (permanent power solution) na pia kutumika kama nishati ya kuzalishia saruji. Hatua hii ya pili mahitaji ya gesi yataongezeka na kufikia futi za ujazo milioni 19-33 kwa siku. Hadi sasa mkandarasi wa kuweka miundombinu hii ya kupelekea gesi hadi kiwandani ameshapatikana na yupo katika majadilino ya kusaini mkataba na Dangote kabla ya kuanza kasi rasmi,” aliongezea Mkurugenzi huyo.

Ndugu Gilbert aliongezea kuwa, TPDC imekamilisha taratibu za manunuzi kwa ajili ya kumpata Mkandarasi (EPC Contractor) uunganishwaji wa bomba la kupeleka gesi asilia kwenye kiwanda cha Lodhia Steel kilichopo Mkuranga, Pwani ambapo bomba hili likikamilika Machi 2018, litawezesha viwanda vingine takribani 12 vilivyopo jirani na Lodhia kuunganishwa na kupata nishati ya gesi asilia kwa ajili ya uendeshaji wa viwanda husika. Kiwanda hiki kitakua na uwezo wa kuchukua gesi asilia kiasi cha futi za ujazo milioni 0.2118 kwa siku.

“Kwa kushirikiana na mbia, Pan African Energy Tanzania Limited – PAET, Shirika limeendelea kusambaza gesi asilia kwa wateja wa viwandani wanaofikia 37 katika Jiji la Dar es Salaam ambao wamekuwa wakihudumiwa na bomba la gesi asilia lililokamilika mwaka 2004 kutoka Songosongo.”

Kwa upande mwingine, Gilbert amefafanua namna TPDC inavyochangia kiasi kikubwa cha uzalishaji wa umeme nchini.

“TPDC imeendelea kuuza gesi asilia kiasi cha futi za ujazo milioni 50-60 kwa siku, kuzalisha umeme ambacho kinatumika kuzalisha umeme katika mitambo inayomilikiwa na Tanesco kwa asilimia mia moja ambayo ni Kinyerezi I, Ubungo II, Somanga Fungu na Mtwara Power Plant. Vile vile Shirika limeendelea kupeleka gesi asilia katika mitambo ya Songas inayozalisha umeme na kumuuzia Tanesco na hivyo kwa ujumla, uzalishaji wa umeme nchini kutokana na nishati ya gesi asilia umefikia zaidi ya asilia hamsini (50%) ya umeme wote unaozalishwa na kuingizwa katika gridi ya Taifa kwa siku.”

“Haya ni mafanikio makubwa kwani kwa kiasi kikubwa tatizo la umeme limepungua kwa sababu ya uhakika wa upatikanaji wa gesi kuzalisha umeme huo na kwa sasa TPDC inajiandaa kupeleka gesi asilia katika mitambo mipya ya Kinyerezi I extension (MW 185) pamoja na Kinyerezi II (MW 240) ili kuendeleza upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini katika kuelekea Tanzania ya viwanda,” aliongeza Emmanuel.

Kwa ujumla, TPDC kupitia idara yake ya Mkondo wa Chini, inaleta faraja hasa pale inapoendelea kufanya mazungumzo na viwanda mbalimbali hasa vile ambavyo viko karibu na miundombinu ya gesi asilia kuweza kuunganisha viwanda hivyo ili viweze kutumia gesi asilia ambayo ni nafuu kwa wastani wa asilimia 30 ikilinganishwa na mafuta na hivyo kushusha gharama za uzalishaji kwa kiasi kikubwa na kuwezesha bidhaa zitakazozalishwa kuwa na bei ya kiushindani kwenye soko la ndani na nje ya nchi.

Miundombinu ya gesi asilia ikiwa ina miaka miwili toka kukamilika kwake tayari tumeanza kuona matunda yake makubwa ni matumaini ya Taifa kuwa miundombinu hii italeta mapinduzi makubwa ya viwanda nchini katika miaka ya hapo mbeleni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles