TIZEBA AZUIA HALMASHAURI  KUANZISHA MIRADI MIPYA

0
591

Na PETER FABIAN WAZIRI wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba amepiga marufuku halmashauri  nchini kuanzisha miradi mipya ya sikimu na mabwawa ya umwagiliaji.


Badala yake amezitaka zitenge fedha za kukamilisha miradi ambayo haijakamilika.
Alitoa kauli hiyo alipofungua warsha ya kuwajengea uelewa kuhusu programu ya kuendeleza Sekta ya Kilimo awamu ya pili (ASDP II) kwa halmashauri za mikoa ya Kanda ya Ziwa.


Warsha hiyo  iliwashirikisha mameya, wenyeviti wa halmashauri, wakurugenzi na wataalamu ambao ni wakuu wa idara za kilimo, mifugo na uvuvi.


  Dk. Tizeba aliwaagiza makatibu tawala wa mikoa yote ya Kanda ya Ziwa kusimamia agizo lake hilo hadi  zitakapokuwa zimekamilisha miradi iliyopo kwenye maeneo yao.


Aliwataka wasimamie fedha zinazotolewa kukamilisha miradi hiyo.
Alisema imekuwapo tabia ya baadhi ya wakurugenzi na wakuu wa idara za kilimo, mifugo na uvuvi katika halmashauri kuanzisha miradi mipya na kuacha inayosubiri fedha ili kuikamilisha.


Waziri alisema wakurugenzi hao wamekuwa wakifanya hivyo kutokana na kubanwa na madiwani   kwenye vikao vya baraza.
Alitoa rai kwa maofisa ugani wa kilimo, mifugo na uvuvi kuwatembelea wananchi katika majukumu yao.


“Serikali haitawavumilia wale ambao watashindwa kuwafikia wananchi na kuwapatia utalaamu wa kina ili kutekeleza miradi yao kwa ufanisi.


 “Hili tunataka kulitungia sheria kali   kuhakikisha mkulima, mfugaji na mvuvi atakayekataa kufuata ushauri wa wataalamu wa serikali   achukuliwe hatua za  sheria.


“Hivyo hivyo kwa   wataalamu watakaoshindwa kutoa ushauri mzuri kwao watafutiwa usajili na kufukuzwa kazi, lengo la serikali kuajiri wataalamu hawa ni kuwasaidia wananchi kufikia malengo,” alisisitiza.


Aliwaagiza maofisa mipango na ugani   kuhakikisha wanakuwa na takwimu kwa kuzifuata katika maeneo ya wakulima, wafugaji na wavuvi badala ya kugushi na kutoa takwimu za uongo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here