22 C
Dar es Salaam
Sunday, June 4, 2023

Contact us: [email protected]

TGC yawatahadharisha wavaa vitu vya madini ya vito bila kupewa elimu

Na Clara Matimo, Mwanza

Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) kinachotoa mafunzo juu ya uongezaji thamani madini ya vito na miamba kimewatahadharisha wananchi wanaopenda kuvaa vitu vya madini ya vito bila kupata elimu ya wataalamu wa jiolojia kwa sababu kila madini yanatabia tofauti kwa maisha na mwili wa binadamu.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella(kushoto) akipewa maelekezo kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na TGC alipotembelea banda hilo kwenye maonesho ya wiki ya madini 2023 iliyofanyika jijini Mwanza kutoka kwa, Esher Njiwa(kulia) ambaye ni Mtaalamu wa Ukataji na Ung’arishaji wa Madini ya Vito na Dhahabu.

Hayo yameelezwa na Mjiolojia kutoka TGC, Esther Njiwa alipozungumza na Mtanzania Digital hivi karibuni jijini Mwanza kuhusu uvaaji wa vitu vya madini ya vito.

“kuna madini yanayosababisha bahati mbaya katika familia na kwa mtumiaji hivyo ni heri kabla ya mtu kuyavaa aonane na mjiolojia ampe elimu ya kutambua jiwe litakalomsababishia yeye na familia yake bahati njema ili kuepuka majanga kwenye familia,”alisema Mjiolojia huyo na kuongeza

“Kila jiwe lina sifa yake kwenye mwili wa binadamu hususani kwenye kuponya magonjwa mbalimbali kama saratani na mafua vilevile yanatengeneza bahati, yanaondoa mapepo wachafu, inaleta nguvu katika mwiliwa binadamu na maisha kwa ujumla, madini
ya ghali kama tanzanite na rubby yanainua uchumi kuna madini ya uponyaji ambayo yanaleta bahati nzuri faida zote hizi mvaaji akionana na mtaalamu wa jiolojia ataelimishwa,”alifafanua Njiwa.

Njiwa ambaye pia ni Mtaalamu wa ukataji na ung’arishaji wa madini ya vito na dhahabu alisema Tanzania ni nchi yenye madini mengi hivyo ni vyema wananchi wakawa wazalendo kwa kuvaa bidhaa za usonara zinazotengenezwa kwa kutumia madini hayo ili wapendeze zaidi pia wachangie kukuza uchumi wa taifa kwani si yote yanayouzwa kwa bei ghari.

“TGC pia tunatoa huduma za uongezaji thamani madini yaani ukataji na ung’arishaji, uchongaji wa vinyago vya miamba, utambuzi wa madini pamoja na kutengeneza bidhaa za usonara kwa kweli tunashukuru Shirikisho la Vyama Vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (Femata), kuratibu wiki ya madini 2023 iliyofanyika kitaifa mkoani Mwanza Mei 3 hadi 9.

“Wiki hiyo imetukutanisha na watu wa rika mbalimbali ambao tulikuwa hatujawafikia na waliamini madini ni dhahabu peke yake kwa hiyo walipoona madini mengine tena vitu vya usonara vilivyotengenezwa kwa madini hayo vinauzwa kwa bei nafuu walibaki wanashangaa,”alisema.

Naye Kaimu Mratibu wa TGC, Daniel Kidesheni aliwaasa vijana nchini kuchangamkia fursa ya elimu wanayoitoa kupitia Wizara ya madini ili waongeze upatikanaji wa ajira katika sekta ya madini kwenye maeneo yao hasa kwa kukata madini, kuyang’arisha na kutengeneza bidhaa za usonara ili kutekeleza adhma ya serikali ya kusafirisha madini nje ya nchi ambayo yameongezwa thamani.

“Tanzania ya sasa hairuhusu kusafirisha madini ghafi nje ya nchi kwa hiyo nawaasa wafanyabiashara ya madini na vijana kote nchini waje TGC wapate elimu ya kukata na kung’arisha madini ili tutengeneze ajira ndani ya nchi na tuongeze kipato kwa taifa,”alisema Kidesheni na kuongeza:

“TGC tunaendelea kutekeleza sera ya madini ya mwaka 2009 kwa kuhamasisha shuguli za uongezaji thamani madini kufanyika nchini na kuunga mkono serikali ya awamu ya sita iliyojikita kutengeneza fursa nyingi za ajira kwa vijana ili kutekeleza ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020/2025,”alieleza Kidesheni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,284FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles