23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

TCRA yazima rasmi simu zisizosajiliwa, Ofisa Nida mbaroni kwa rushwa ya 30,000/-

WAANDISHI WETU-DAR/MIKOANI

LAINI za simu ambazo hazijasajiliwa kwa mfumo wa alama za vidole zimezimwa rasmi na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Hatua hiyo imekuja baada ya siku 20 zilizoongezwa kufikia ukomo baada ya zile za awali zilizomalizika Desemba 31, mwaka jana.

Wakati TCRA ikizima laini hizo, siku ya jana pia ilitawaliwa na matukio mbalimbali, yakiwamo ya mawakala wa kampuni za simu na maofisa wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), kutuhumiwa kuomba na kupokea rushwa kwa wananchi.

Pia watu mbalimbali walitumia mitandao ya kijamii kuagana na ndugu na jamaa zao kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kushindwa kusajili laini kutokana na kutopata namba ama kitambulisho cha taifa kinachotolewa na Nida.

Akizungumza jana, Ofisa Mwandamizi wa TCRA, Semu Mwakyanjala, alisema hakuna uwezekano wa muda huo kuongezwa.

Alisema hadi kufikia Januari 15, jumla ya laini 27,287,091 zilikuwa zimesajiliwa sawa na asilimia 56 ya laini 48,717, 967 zinazotumika.

Mwakyanjala alisema laini 21,430,876 ambazo ni sawa na asilimia 44 zilikuwa hazijasajiliwa kwa alama za vidole.

KIGOGO WA NIDA MBARONI

Mkoani Shinyanga, Jeshi la Polisi liliwakamata watu wawili kwa tuhuma za rushwa wakidaiwa kuwatoza Sh 30,000 wananchi waliojitokeza kujiandikisha na kufuatilia namba zao.

Waliokamatwa kwa tuhuma hizo ni Ofisa Msajili Msaidizi wa Nida mkoani Shinyanga, Haroon Mushi na wakala wa usajili laini za simu za mkononi, Victor Vicent.

Watu hao wanadaiwa kuwatoza fedha wananchi ili wawapatie namba za Nida na kwenda kusajili laini zao za simu kwa alama za vidole.

Tukio hilo lilitokea jana saa saba mchana baada ya Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko kufika ofisi za Nida Shinyanga mjini na kupata taarifa za wananchi kuombwa fedha.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Joseph Paulo, alithibitisha kuwatia mbaroni watu hao na kusema upelelezi bado unaendelea.

Alisema watuhumiwa hao wamekabidhiwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa hatua zaidi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta, alisema akiwa ofisi za Nida kukagua namna utoaji wa namba unavyoendelea, alipata taarifa za wananchi kuombwa fedha kutoka kwa wakala wa usajili laini za simu za mkononi ambaye alikuwa akifanya mawasiliano na ofisa huyo wa Nida.

Alisema mara baada ya kumkamata wakala huyo na kumfikisha polisi kuhojiwa, ndipo aliposema kwamba anashirikiana na mmoja wa maofisa na Nida na kueleza namna wanavyotekeleza jambo lao.

“Tulipopewa taarifa hiyo ikabidi tumkamate na huyu ofisa wa Nida, Haroon Mushi, tumefanya uchunguzi wa simu zao na kubaini kuwapo na mawasiliano ya wananchi kuwaomba fedha na baadhi yao wameshawatumia, bado tunaendelea na uchunguzi zaidi,” alisema Jasinta.

Alitoa wito kwa wananchi wa Shinyanga kuacha tabia ya kutoa fedha ili kupata namba za vitambulisho vya taifa kwa sababu zinatolewa bure, huku akiagiza maofisa wa Nida wafanye kazi usiku kucha na kutofunga ofisi hizo hadi pale watakapowahudumia watu wote.

Naye wakala huyo, Vicent alikiri kufanya kosa hilo na kuomba msamaha wakati Mushi alikanusha tuhuma dhidi yake.

Ofisa huyo wa Nida alisema pia ni kweli amekuwa akipatiwa majina ya watu kwa ujumbe mfupi wa simu (sms) na wakala huyo ili awaangalizie namba zao za Nida.

ACT KWENDA MAHAKAMANI

Chama cha ACT Wazalendo kimesema kitakwenda mahakamani kupinga hatua ya kuzimwa kwa simu zisizosajiliwa kwa alama za vidole iwapo Serikali itaendelea na msimamo wake.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa chama hicho, Ado Shaibu, alisema changamoto waliyonayo wananchi ni kukosa vitambulisho vya taifa kosa ambalo si la kwao.

Alisema wananchi hawapaswi kuadhibiwa kwa kosa la Nida iliyoshindwa kuwapatia vitambulisho hivyo kwa muda mrefu.

“Iwapo Serikali itaendelea na msimamo wake wa kuzima laini zote za simu, zikiwamo za wananchi ambao hawajapata vitambulisho vya uraia, Chama cha ACT Wazalendo kitakwenda mahakamani kupinga hatua hiyo,” alisema Shaibu.

Aliiomba Serikali kusitisha mpango wake huo hadi hapo Nida itakapoweza kuwapatia vitambulisho vya uraia Watanzania wote.

Shaibu alisema mpango huo wa kuzima laini kwa sasa uwahusu wale tu ambao tayari wana vitambulisho vya taifa, lakini hawajasajili laini zao.

Aidha aliitaka Serikali kuiwezesha Nida kuwa na nyenzo na rasilimali watu wa kutosha kuweza kuhimili mahitaji ya vitambulisho kwa Watanzania wengi, ili nayo iwajibike kuvitoa kwa wakati.

“Kwenye baadhi ya maeneo hali ni mbaya zaidi, mathalani Kigoma ambako asilimia 73 ya wananchi bado hawajasajili, sababu kuu ikiwa wengi wakipitia ugumu wa kupata namba au vitambulisho vya taifa,” alisema Shaibu.

Alisema uamuzi wa Serikali kuzima laini hizo utakuwa na athari kubwa kiuchumi na kijamii kwa kuwa miamala mingi ya kifedha inafanyika kwa njia ya simu.

Shaibu alisema kutokana na hali hiyo Serikali itapoteza kodi kubwa inayoipata kupitia miamala hiyo.

KASI NDOGO MITANDAO YA SIMU

Baadhi ya wananchi ambao wamepata namba za Nida katika Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, walisema changamoto kubwa wanayokutana nayo katika usajili wa laini zao ni mtandao wa kampuni za simu kutofanya kazi muda mrefu.

Wananchi hao walisema kuwa licha ya kupata namba za Nida kwa wakati, tatizo kubwa limebaki kwenye mitandao ya simu kuwa na kasi ndogo ya usajili.

Walisema kuwa toka juzi kumekuwapo na tatizo kubwa la mtandao (Network) kushindwa kusajili laini zao na wakati mwingine haupatikani kabisa.

Maduhu Nile, mkazi wa Kidinda mjini Bariadi, alisema awali walikuwa wakisumbuka kupata namba za Nida, lakini kwa sasa wanakutana na tatizo la mtandao kuwa chini na kushindwa kabisa kusajiliwa laini zao.

“Binafsi naweza kusema tatizo si la Nida, ila lipo katika mitandao ya simu, tunashindwa kabisa kusajili laini zetu na hatujui ni kwanini mitandao hiyo inakuwa na kasi ndogo nyakati za asubuhi hadi jioni ila usiku inafanya kazi,” alisema Nile.

Naye Salome Mabula alisema; “Leo ni siku ya tatu nahangaika kupata usajili, mtandao wa TTCL na Airtel umekuwa tatizo kubwa na sijui lini utakaa vizuri. Usiku mimi siwezi maana nina familia na watoto wadogo.”

Meneja wa Kampuni ya TTCL Mkoa wa Simiyu, Bimbona Kyamani, alikiri kuwapo kwa tatizo la mtandao ambalo linakabili mitandao yote kutokana na uwapo wa idadi kubwa ya wananchi wanaohitaji usajili wa laini zao, hasa kipindi hiki cha mwisho.

Alisema ili kukabiliana na tatizo hilo, TTCL wameamua kufanya kazi hadi usiku kuwahudumia wananchi wengi zaidi muda ambao mtandao unafanya kazi kwa kasi na wamefanikiwa kuwasajili wananchi wengi.

“Ni kweli kuna tatizo la mtandao na hilo lipo kwa upande wa Nida, maombi ni mengi kuliko uwezo wa mfumo wa upokeaji taarifa kutoka Nida,” alisema Kyamani.

Ofisa usajili wa Nida Mkoa wa Simiyu, Careen Kuwite, alisema hadi sasa wamefanikisha kutoa namba kwa wananchi kwa asilimia 87 ya waliosajiliwa huku wakiahidi kukamilisha asilimia 23 iliyobaki ndani ya mwezi mmoja.

Alisema kwa sasa wameongeza muda wa kufanya kazi hadi siku za mapumziko kuhakikisha wanatoa huduma kwa wananchi wote.

Hata hivyo, alisema kuna changamoto za wananchi kushindwa kujaza vizuri taarifa zao katika fomu husika.

“Kuna wananchi wengine wanashindwa kabisa kujaza fomu vizuri, hawajui tarehe zao za kuzaliwa wala majina yao sahihi na ndio hao ambao wamekaa muda mrefu bila kupata namba, ila kwa wale wanaojaza vizuri hupata namba ndani ya siku tano,” alisema Kuwite.

DAKIKA ZA LALA SALAMA

Baadhi ya watu walitumia mitandao mbalimbali ya kijamii kutoa ujumbe unaoashiria kuagana na ndugu na jamaa zao kwa kile walichoeleza kuwa hawajajisajili kwa alama za vidole kutokana na kutopata namba ama kitambulisho cha taifa.

Ujumbe huo uliwekwa katika mitandao ya Facebook, makundi mbalimbali ya WhatsApp, Instagram na wengine wakiweka katika akaunti zao za Twitter.

Baadhi ya ujumbe huo ulisomeka; ‘Ifikapo saa 6 usiku TCRA wanabonyeza tu… kwaherini ya kuonana’, ‘Sasa tutarudi kwenye simu za upepo na zile za shule za msingi tulipokuwa tunajibu mitihani’, ‘Naomba tujulishane makazi yenu ya kudumu kabla laini hazijazimwa’.

Habari hii imeandaliwa na Tunu Nassor, Nora Damian, (Dar es Salaam) Damian Masyenene, Sam Bahari (Shinyanga) na Derick Milton (Simiyu)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles