24.2 C
Dar es Salaam
Monday, September 26, 2022

TCRA ENDELEENI KUTOA ELIMU KWA WASANII

NA CHRISTOPHER MSEKENA


WASANII wamejikuta katika uhitaji mkubwa wa kupata elimu ya mtandao, maudhui na kanuni mpya za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ambazo zimekuwa zikigusa maisha yao ndani na nje ya sanaa.

Itakumbukwa mwaka huu wasanii kama Diamond Platnumz, Nandy, Irene Uwoya na Hamisa Mobetto, ni miongoni mwa nyota waliojikuta mikononi mwa Kamati ya Maudhui ya TCRA baada ya kukiuka kanuni za mtandao kwa kuchapisha picha na video katika kurasa zao za Instagram.

Wasanii hao walilazimika kuomba radhi kwa jamii kupitia mtandao baada ya kukiri makosa yao ambayo waliyafanya kwa bahati mbaya kutokana na kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu matumizi sahihi ya mitandao.

Alhamisi wiki hii Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ilitoa mwaliko kwa wasanii wa Bongo Fleva kuhudhuria semina ili kuwapa elimu ya mtandao, maudhui na kanuni hizo mpya ambazo zimekuwa zikiwatia hatiani mara kwa mara.

Semina hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam kwa mafanikio makubwa, ilihudhuriwa na wasanii wengi nyota na chipukizi na mjadala wa kupeana elimu ya masuala ya mitandao ulipamba moto na kila aliyehudhuria.

Wasanii walipata nafasi ya kuhoji utendaji na uwepo wa TCRA katika kazi zao za muziki hali kadhalika elimu na ushauri ulitolewa kwao kutoka kwa wataalamu na wabobezi wa masuala ya sheria ya mtandao kutoka kamati ya maudhui ya mamlaka hiyo.

Hakika kila msanii aliyefika pale hakutoka kama alivyoingia, alinufaika na semina ile ya kwanza katika sekta ya sanaa nchini. Bila shaka wasanii hao watakuwa watumiaji wazuri wa mitandao.

Imani yangu kwao ni kutokusikia tena msanii wa Bongo Fleva akifikishwa katika kamati ya maudhui TCRA kuhojiwa kuhusu kuchapisha picha za utupu au zinazokiuka kanuni hizo zinazolenga ili kulinda maadili yetu.

Rai yangu kwa mamlaka hiyo ni kuendelea kuyaita makundi mbalimbali ya wasanii na kuwapa elimu kwa sababu naamini msanii ana wafuasi wengi nyuma yake ambao wanaweza kuelimika kupitia elimu aliyopewa msanii mmoja.

Elimu hiyo itolewe kwa makundi ya wasanii wanaofanya sanaa za maigizo, maonyesho na ufundi ili kurahisisha mkakati wa kuwa na jamii safi inayofuata kanuni mpya za mtandao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,051FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles