29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

JESHI LA POLISI LIJIFUNZE KUTENDA HAKI


TUMEPATA kuandika huko nyuma, tukaandika na leo tunarudia kuandika juu ya umuhimu wa kila mtu katika eneo lake kuhakikisha anatenda haki.

Umuhimu wa kutenda haki umefafanuliwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wajibu wa haki umefafanuliwa katika eneo la usawa mbele ya sheria na usawa wa binadamu, haki ya kuishi, uhuru wa mtu binafsi, kufanya kazi, kumiliki mali, uhuru wa mawazo nk.

Tumekuwa tukisisitiza juu ya kutenda haki si tu kwa sababu tunatimiza wajibu wetu kikatiba, bali kwasababu pale haki inapodhulumiwa matokeo yake huwa si mazuri, kwa mfano tutajikuta tumezalisha chuki, mifarakano, visasi n.k.

Tuliwahi kuandika huko nyuma na kusisitiza kwamba kila mtu na hasa vyombo vilivyopewa nguvu kimamlaka vinapaswa kutambua kuwa wajibu huo wa kikatiba una maana moja tu kubwa, kutatua matatizo na si kuyaongeza.

Tumelazimika kukumbusha wajibu huo baada ya kauli iliyotolewa jana na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Siro, kuhusiana na tukio la  Polisi kumshambulia mwandishi wa habari, Silas Mbise.

IGP Sirro, ambaye alikuwa akielezea ulipofikia uchunguzi juu ya suala hilo, alisema Mwandishi huyo alishambuliwa kwa sababu alikataa kutii agizo la askari aliyemkataza kuingia katika sehemu waliyozuiliwa.

Wakati Sirro akitoa kauli hiyo, waandishi wa habari wakongwe wameshangaa na hata kuhoji kipigo alichopewa Mbise ambaye alikuwa hana silaha.

Wamemtaka Sirro asimamie sheria na weledi wa Jeshi la Polisi katika kutekeleza majukumu yao ya kulinda raia na mali zao.

Waandishi hao pia wamehoji sehemu ambayo waandishi hawaruhusiwi kuingia katika Uwanja wa Taifa na kusema kuwa IGP Sirro anajaribu kufukia maovu ya jeshi hilo badala ya kukemea.

Wakati waandishi hao wakongwe wakimpa ushauri huo IGP Sirro, waandishi walioshuhudia tukio hilo wamesema Mbise hakumkunja wala kujaribu kupigana na askari yeyote.

Kwa sababu hiyo basi, IGP Sirro na Jeshi lake wanapaswa kuchunguza jambo hilo kwa misingi ambayo itazingatia haki ya pande zote mbili.

Huko nyuma tulipata kuandika kuwa zipo ripoti ambazo zinaonyesha kuwa barani Afrika kwa muda mrefu sana watu wameumizwa na vitendo vya kudhulumiwa haki zao za msingi.

Kwa mujibu wa ripoti hizo, hata kutopea katika umaskini wa kimawazo, na hivyo wengi kuhadaika na kauli za wanasiasa, viongozi na watu wenye nafasi katika jamii, msingi wake ni dhuluma ya haki zao za msingi.

Kwa misingi kama hiyo, sisi kama chombo cha habari  tunao wajibu wa kukumbusha kwamba vyombo, likiwamo Jeshi la Polisi, kila inachofanya kabla ya kutoa kauli au uamuzi wowote basi vitambue vinao wajibu wa kuchunguza, kusikiliza, kubadilisha na kuboresha.

Jeshi la Polisi linapaswa kutambua kwamba chochote kitakachofanyika bila kufuata misingi ya kutenda haki kitakwenda kuathiri mustakabali mwema wa Taifa letu.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles