27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 16, 2024

Contact us: [email protected]

TATIZO YANGA AU WAAMUZI?

NA ZAINAB IDDY


HIVI karibuni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilimemwondoa mwamuzi, Hussein Athuman, kwenye orodha ya waamuzi wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), baada ya kupata alama za chini ambazo hazimwezeshi kuendelea tena kuchezesha ligi hiyo.

Mwamuzi huyo amekutwa na rungu hilo mara baada ya kuchezesha mchezo namba 150, uliozikutanisha timu za Yanga na Majimaji katika dimba la Majimaji mkoani Ruvuma, Januari 17 mwaka huu huku Wanajangwani wakitoka kifua mbele kwa ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Deus Kaseke.

Ni jambo zuri lililofanywa na TFF kupitia kamati yake ya waamuzi iliyopo chini ya mwenyekiti wake, Salum Chama, kwani ni wazi msimu huu shirikisho hilo limepanga kuhakikisha ligi inachezeshwa na waamuzi bora.

Lakini kutimuliwa kwa mwamuzi huyo, kumezua swali iwapo kama tatizo lipo kwa waamuzi wa ligi au klabu ya Yanga.

Swali hilo linakuja kutokana na hivi karibuni waamuzi wengi wanaokutwa na rungu hilo, lazima wanakuwa wamechezesha mechi inayowahusu mabingwa hao watetezi, Yanga.

Inakumbukwa Aprili 29, mwaka jana katika mchezo wa FA wa kombe linaloandaliwa na TFF, mwamuzi Abdallah Kambuzi, alifungiwa mwaka mmoja wakati msaidizi namba mbili, Charles Simon, akiondolewa kwenye orodha ya waamuzi, huku Yanga wakitinga hatua ya fainali.

Ukimtoa mwamuzi huyo yupo pia aliyechezesha mechi namba 49 kati ya Yanga na Simba, Martin Saanya na msaidizi wake, Samweli Mpenzu, walioondolewa kwenye orodha ya waamuzi wa Ligi Kuu.

Maamuzi hayo yamefanywa na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji ya Bodi ya ligi, iliyobaini mapungufu mengi ya kiutendaji yaliyofanywa, ikiwemo kutoa kadi nyekundu kwa nahodha wa Simba na kukifanya kikosi cha Wanamsimbazi kucheza pungufu mechi iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1 ya Oktoba mosi mwaka jana.

Katika rungu hilo limemkuta pia aliyechezesha mechi ya Mbeya City  na Yanga, iliyochezwa katika Uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya,  pale mwamuzi Rajabu Mrope, aliyechezesha mchezo namba 108  akiondolewa katika orodha za waamuzi wa Ligi Kuu, msimu wa mwaka 2016/2017 na kurudishwa kwenye Kamati ya Waamuzi ili waweze kumpangia daraja lingine la uamuzi.

Mrope alitiwa hatiani kwa kosa la kutojiamini mchezoni kiasi cha kushindwa kutoa maamuzi sahihi pale alipokubali bao la Mbeya City, kisha kukataa na mwisho kukubali tena mechi iliyomalizika kwa Yanga kufungwa 2-1.

Hayo ni machache kati ya mengi yaliyosababisha kufungiwa kwa waamuzi wanaochezesha Ligi Kuu katika michezo, inayoihusisha Yanga na timu nyingine.

Hapo ndipo swali la je, tatizo ni mwamuzi au Yanga, kwanini katika ligi na kombe la FA, lakini ni nadra kuona waamuzi wakifungiwa iwapo mchezo haujaihusisha Yanga.

Jambo hili linasababisha kuzua maswali, kwanini kila anayechezesha mechi ya Yanga afungiwe, je, hii ni kuwatisha waweze kutafsiri vizuri sheria 17 za soka au kuwatisha waweze kuibeba Yanga?

Ni wakati wa TFF kufanya mambo yasiyoweza kuzua maswali, katika hili ni vizuri kuangalia mechi zote na pale panapoonekana kuna tatizo haki itendeke pasipo kuangalia timu gani imefanya kosa na ina watu gani ndani ya shirikisho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles