Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Mwimbaji wa Injili asili ya Afrika anayeishi Australia Tarisai Vushe, anatarajia kutikisa chati za muziki wa gospo mapema Novemba kupitia wimbo wake mpya Addicted.
Akizungumza na www.mtanzania.co.tz mapema leo Septemba 22, 2023 Tarisai amesema wimbo huo umebeba dhamira ya kweli ya uhusiano wake na Kristo na unakwenda kuhamasisha vijana wengi kumgeukia Mungu na kuacha kuuza nafsi zao kwa shetani.
“Ninamshukuru Mungu kwa kunipa nafasi ya kumtumikia na sasa nipo tayari kuachia wimbo huu Addicted ambao utatoka Novemba, audio na video, huu ndio muda wa vijana kubadilisha maisha yao na kumgeukia Mungu kwa kutengeneza mahusiano naye,” amesema Tarisai.
Aidha, Tarisai amesema wimbo huo umechelewa kutoka kwasababu alikuwa kwenye ziara yake ulimwenguni mwote ambako alipata nafasi ya kufanya huduma na watu mashuhuri kama, William McDowell na Israel Houghton.
Tarisai mwenye asili ya Zimbabwe amesema lengo kubwa la kutangaza muziki wake Afrika ni uzalendo alionao juu ya watu bara hili ndio baada ya kukaa ughaibuni kwa muda mrefu.
“Kwa muda mrefu nimefanya kazi huku magharibu lakini sasa nimeona ni muda wa kuungana na asili yangu, Afrika ni mizizi yangu,” amesema.
Ameongeza kuwa miongoni mwa mastaa anaotamani kufanya nao kazi hapo mbeleni ni Nandy kutokana na upekee wake kwenye muziki.
“Ndiyo ninafikiria kufanya kazi na waimbaji wa Tanzania na miongoni mwao ni Nandy ni msanii mkubwa. Ukuaji wake umekuwa wa kushangaza na anatendea haki kipaji chake,” amesema Tarisai.
Mrembo huyo mbali na kufanya muziki wa gospo ni mwigizaji, mkufunzi wa muziki katika moja ya vyuo vya sanaa nchini Australia na mshinda namba tano wa mashindano ya Australian Idol.