28.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 18, 2024

Contact us: [email protected]

DED Uvinza, Mweka Hazina, Mhandisi watofautiana uwepo wa fedha mbele ya Majaliwa

*Waziri Mkuu aagiza TAKUKURU wachunguze fedha za ujenzi

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Kigoma, Steven Mafiga afanye haraka kuwachunguza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Zainab Mbunda na Mweka Hazina wa Wilaya hiyo, Majjid Mabanga ili kubaini ni kwa nini miradi haiendi wakati fedha zilishatolewa kitambo.

“Kamanda wa TAKUKURU Mkoa kamilisha hiyo kazi kwa haraka sana. Rais wetu analeta fedha nyingi sana lakini kuna watu hawafanyi maamuzi. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri na Mweka Hazina wakae pembeni kupisha uchunguzi, wakati ukiendelea na kazi,” amesema.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo Alhamisi, Septemba 21, 2023 wakati akizungumza na watumishi na wananchi waliohudhuria uwekaji wa jiwe la msingi kwenye jengo la ghorofa moja la Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, lililoko Lugufu, Uvinza, mkoani Kigoma.

Waziri Mkuu amechukua hatua hiyo baada ya kubaini kuwa fedha za miradi ya ujenzi wa hospitali ya wilaya, vituo vya afya vya Rukoma na Sunuka na zahanati za Mgambo na Kajeje zilizotumwa tangu mwaka 2021/2022, zinadaiwa kuwepo kwenye akaunti wakati majengo husika hayajakamilika na taarifa inayotolewa inasema ujenzi uko kwenye hatua ya ukamilishaji.

“Kwa nini lugha ya ukamilishaji hapa Uvinza imeshamiri? Fedha za miradi zikiletwa ziende kwenye kazi iliyokusudiwa. Sasa hapa, Mkurugenzi anasema fedha zipo, Mweka Hazina anasema zimeisha, Mhandisi aliandika dokezo la kuomba vifaa, mtu wa manunuzi anasema hajalipata. Fedha zipo na kazi haziendi. Nimewaweka pembeni kwa sababu nimeona usimamizi ni mbovu,” amesema.

“Leo hii tukitoka Nguruka, Kamanda wa TAKUKURU ingia kazini, angalia hizo fedha ziko kwenye akaunti zipi, angalia kuna shilingi ngapi na zilikuwa zimepangwa kufanya shughuli gani,” amesema.

Kabla ya kuweka jiwe la msingi la jengo la ofisi ya Halmashauri hiyo, Waziri Mkuu alikagua hospitali ya wilaya hiyo na kubaini majengo kadhaa hayajakamilika licha ya kuwa fedha zilitolewa tangu Mei, 2021. Pia alikuta vifaa tiba vingi vikiwa kwenye chumba ambacho hakina milango wala vipoza hewa (Air conditioner) huku vikiwa vimejaa vumbi.

“Ni kwa nini vifaa hivi kwa kielektroniki tena vya gharama kubwa vimeachwa tu hapa, tena vinapigwa na vumbi? Hamuoni huruma kwa fedha za Serikali?” alihoji.

Waziri Mkuu amesema ametembelea mikoa mbalimbali hapa nchini na kuweka mawe ya msingi ama kuzindua majengo ya wagonjwa wa dharura (EMD) lakini haelewi ni kwa nini majengo ya Uvinza hadi leo hayajakamilika. “Kibondo na Kasulu wenzenu wamekamilisha majengo yao, iweje hapa Uvinza bado tu?,” amehoji Waziri Mkuu.

Akitoa taarifa kuhusu ujenzi wa hospitali ya wilaya, Mkuu wa Kituo kwenye hospitali hiyo, Dk. David Patrick alisema mwaka 2019 walipokea sh. bilioni 1.5 za ujenzi wa majengo saba, kisha wakapokea sh. milioni 300 za njia ya watembea kwa miguu.

“Mei, 2021 tulipokea shilingi milioni 500 za wodi tatu, na Machi, 2022 tulipokea shilingi milioni 390 za EMD na nyumba ya watumishi. Pia tulipokea shilingi milioni 523 za vifaa tiba,” alisema.

“Halmashauri ya Wilaya Uvinza ilipokea fedha kiasi cha sh. bilioni moja na milioni mia tano mwaka 2019 kwa ajili ya ujenzi wa majengo saba ya awali ambayo ni jengo la mionzi, wodi ya wazazi, maabara, wagonjwa wa nje, utawala, madawa, jengo la kufulia. Utekelezaji wa mradi wa Hospitali ya Wilaya ulianza tarehe 10 Januari, 2019,” alisema Dk. Patrick.

Mapema, Naibu Waziri wa TAMISEMI (Afya), Dk. Festo Dugange alisema Serikali ilitoa Sh bilioni 1.9, kisha ikatoa sh. milioni 170 na Julai, mwaka huu imetoa milioni 750 kwa ajili ya ujenzi jengo la Halmashauri ambalo hadi sasa lilipaswa kuwa limekamilika.

“Nawapa muda hadi Oktoba 30, 2023 liwe limekamilika na limeanza kutoa huduma,” alisema.

Kuhusu hospitali ya wilaya ya Uvinza, Dk. Dugange alisema fedha zilianza kutumwa mwaka wa fedha 2019/2020 na hadi sasa Sh bilioni 3.4 zimeshapokelewa.

“Julai 2021 tulikuja kukagua na kuelezwa kuwa majengo yangekamilika ifikapo Desemba, 2021. Sh milioni 300 za EMD zilitumwa lakini bado jengo hilo halikamilika,”.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles