32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania, Misri kuendeleza ushirikiano sekta ya uchukuzi

Na Esther Mnyika,Mtanzania Digital

Tanzania na Misri zimetangaza kuendeleza ushirikiano wa kibiashara baina ya mataifa hayo katika sekta ya uchukuzi kusaidia kuleta maendeleo na kukuza uchumi wa nchi.

Hayo amezungumzwa na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, Februari 19,2024 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi cha mkakati cha kukuza ushirikiano baina ya Tanzania na Misri.

Amesema ushirikiano wa kidiplomasia baina ya mataifa hayo ni wa muda mrefu, hivyo kikao kilichofanyika ni kikubwa na kina dhamira ya dhati kuendeleza ushirikiano wa kibiashara baina ya mataifa hayo mawili.

“Tunamshukuru sana Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuboresha miundombinu ambayo imeleta mafanikio makubwa hususan katika sekta ya usafirishaji,” amesema

Ameongeza kuwa kazi ya ujenzi bora wa miundombinu unaofanywa na serikali katika sekta ya usafirishaji ni kubwa na inapaswa kuungwa mkono na kila mpenda maendeleo katika taifa.

Kwa mujibu wa Profesa Mbarawa, bila kuwekeza katika miundombinu hakuna maendeleo, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia imewekeza kwa mafanikio sehemu nyingi.

Ameeleza kuwa Bandari ya Dar es Salaam kuna uwekezaji mkubwa umefanyika kupitia mradi wa uboreshwaji wa bandari hiyo kuongeza ufanisi kwa nchi ambazo hazina bandari.

Vile vile wamekutana na Waziri wa Uchukuzi wa Misri aliyeambatana na wawekezaji wakubwa, wataalamu mbalimbali kuwapa uzoefu na kutazama fursa zilizopo hususan katika sekta ya uchukuzi.

“Tanzania kuna fursa tele, tunawakaribisha katika sekta ya bandari hususan ujenzi wa gati 13, 14 na 15 ambapo serikali inawakaribisha kufanya uwekezaji katika eneo hilo na maeneo mengine ikiwemo ya anga,” amesema.

Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi wa Misri, Luteni Jenerali Kamel Alwazeer, amesema wamekuwa na ushirikiano mzuri na Tanzania toka enzi za Rais Gamal Abdel Nasserna na Hayati Mwalimu Julius Nyerere .

Amesema Tanzania ni kitovu cha usafiri na usafirishaji ndani ya Afrika Mashariki kutokana na uwepo wa Bandari ya Dar es Salaam ambayo imekuwa na ufanisi mkubwa kwa nchi.

“Kupitia mkutano huu tutaanza ushirikiano baina ya Bandari ya Dar es Salaam na Bandari ya Savaga iliopo Misri kubadilishana uzoefu na utalamu,”amesema LuteniJenerali Alwazeer.

Pia amesema mkutano huo ni muhimu na una lengo la kuendeleza ushirikiano uliopo kwa mataifa hayo ambayo yamekuwa yakishirikiana kwa muda mrefu.

Katika mkutano huo, taasisi zote zilizoko chini ya Wizara ya Uchukuzi zilitoa taarifa zao za mafanikio na kutangaza fursa zilizopo ikiwemo Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles