23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania miongoni mwa nchi 22 duniani zinazoongoza kwa ukoma

VERONICA ROMWALD  – DAR ES SALAAM

Tanzania ni miongoni mwa nchi 22 ambazo bado zina idadi kubwa ya wagonjwa wa ukoma duniani.

Hiyo ni kulingana na tafsiri mpya ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ambalo linaeleza nchi zote zinazopata wagonjwa zaidi ya 1,000 kwa mwaka bado zina hatari ya kurejea kuwa na wagonjwa wengi.

Hayo yalielezwa hivi karibuni na Daktari Mkuu Mwandamizi wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma, Deus Kamara alipozungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu.

Mahojiano hayo yalijikita kuangazia hali ya ugonjwa huo nchini, kuelekea maadhimisho ya Siku ya Ukoma Duniani ambayo hufanyika Jumapili ya mwisho wa Januari kila mwaka. 

“Juhudi kubwa zilifanyika duniani kukabili ukoma, tangu mwaka 2006 Tanzania tulifanikiwa kukabili na kuutokomeza ukoma, tulishautokomeza. “Lakini bado kuna baadhi ya halmashauri zina idadi kubwa ya wagonjwa, hivyo kwa tafsiri mpya ya WHO maana yake ni kwamba bado tupo kwenye hatari, pamoja na nchi nyingine 22, bado tuna wagonjwa zaidi ya 1,000 kwa mwaka.

“Katika kipindi cha takriban miaka saba tulipata wagonjwa wapya wapatao 2,000, kwa mwaka 2018 pekee tulipata wagonjwa wapya 1,933,” alibainisha. Dk. Kamara ambaye pia ni Mratibu wa Taifa wa Kudhibiti Ugonjwa wa Ukoma (NTLP), alisema Serikali imeweka mikakati madhubuti kuudhibiti ugonjwa huo nchini.

Alisema inahakikisha inakata mnyororo wa maambukizi kutoka kwa mgonjwa kwenda kwa asiye na ugonjwa. “Kwanza lazima tuwapate wagonjwa, tuwaingize kwenye mfumo wa matibabu, na wale ndugu wa karibu tunawapa dawa kinga,” alisema.

Alisema ukoma ni ugonjwa wa kuambukiza unaoenezwa na vimelea vya bakteria aitwaye kitaalamu Mycobacterium leprae.

Mshauri wa Mambo ya Afya wa Shirika lisilo la Kiserikali la GLRA kutoka nchini Ujerumani, Kasasi Mayogu alisema mara nyingi bakteria huyo anapoingia mwilini hukaa katika sehemu za baridi. “Kwa miaka 60 sasa GLRA tunashirikiana na Serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya ukoma,” alisema.

Alisema wanayo matumaini kuutokomeza kwani dawa kinga inayotumika inaonesha mafanikio.

“Imethibitishwa na WHO inaitwa kitaalamu Rifampicin Single Dose (SDR), tulitoa Morogoro (Mvomero na Kilombero), Lindi (Liwale) na maeneo mengine, tunawapa dozi moja tu wale ambao wanaishi na ugonjwa, lakini hawajaonesha dalili. “Kwa hatua hii Tanzania ni nchi ya kwanza Afrika kutoa dawa kinga hii,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles