25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Viapo viongozi wa umma kufuatiliwa

Mwandishi Wetu -Dodoma

NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mary Mwanjelwa, ameiagiza Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kufuatilia kama viongozi wanafanya kazi kwa mujibu wa viapo vyao.

Alitoa agizo hilo jana jijini hapa alipotembelea ofisi za sekretarieti hiyo kwa lengo la kufahamiana na watendaji na kuangalia utendaji kazi wao.

Alisema ni lazima sekretarieti hiyo ifuatilie utekelezaji wa matamko na viapo vinavyotolewa na viongozi wa umma na kuhakikisha inachukua hatua kali kwa viongozi wanaokwenda kinyume cha matamko yao.

“Eneo la ufuatiliaji wa matamko na viapo kwa viongozi wa umma lina pengo kwa sababu wapo viongozi wanaosoma matamko na kula kiapo cha ahadi ya uadilifu, lakini maisha yao ni tofauti na viapo walivyokula.

“Sekretarieti ya maadili hamtakiwi kuishi na kufanya kazi kwa mazoea, fuatilieni viongozi wanaokula viapo kama wanafanya kazi kwa mujibu wa viapo vyao, tokeni nje ya ofisi zenu ili mjue ukweli na uongo wa maisha ya viongozi,” alisema Mwanjelwa.

Alisisitiza kuwa kazi nzuri ya kiongozi wa umma inatakiwa kuendana na maadili na kwamba hata kama kiongozi anafanya kazi nzuri kiasi gani, kama matendo yake ni ya ovyo, kiongozi husika anakuwa wa ovyo. Katika hatua nyingine, amewataka watumishi wa sekretarieti hiyo kufanya kazi kwa uzalendo, kuwa waadilifu na kuepuka kufanya kazi kwa mazoea.

“Chapeni kazi, twende na kasi ya mabadiliko yaliyopo leo, kuweni wavumilivu, changamoto zilizopo lazima mkabiliane nazo,” alisema. Kamishna wa Sekretarieti hiyo, Jaji mstaafu Harold Nsekela, alidai kuwa ofisi yake imeanzisha mchakato wa ujazaji wa fomu za tamko la rasilimali na madeni kwa viongozi wa umma kwa njia ya mtandao.

“Mfumo huu una lengo la kuwasaidia viongozi wa umma zaidi ya 16,000 kujaza tamko hili na kuliwasilisha kwetu wakiwa mahali popote kwa kutumia Tehama bila kufika katika ofisi zetu wala kutuma taarifa zao kwa njia nyingine ikiwamo posta,” alisema.

Jaji Nsekela alisema tangu mwaka 2017 sekretarieti hiyo imezindua matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa menejimenti ya taarifa za kimaadili (EMIS) ili kurahisisha uchambuzi na upatikanaji wa taarifa za kimaadili zinazosaidia katika utoaji wa uamuzi na kuepuka mfumo wa zamani wa kutumia karatasi.

Mfumo huo una uwezo wa kukusanya, kuchakata, kutunza taarifa na kumbukumbu mbalimbali kuhusu malalamiko ya ukiukwaji wa maadili na kufanya uchunguzi wa awali wa malalamiko.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles