24 C
Dar es Salaam
Thursday, July 25, 2024

Contact us: [email protected]

TANZANIA KUTOA TAARIFA ZA KIBIASHARA KWA WANACHAMA

Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

WIZARA ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, imesema itahakikisha Tanzania kwa kushirikiana na nchi wanachama za Jumuiya za Afrika inakuwa katika mfumo wa pamoja wa kutoa taarifa za kibiashara ili ziweze kujitangaza na kuchangia pato la taifa.

Hayo yalielezwa juzi na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Adolf Mkenda, wakati akizungumza na waandishi wa habari  juu ya mkutano wa kimataifa wa kujadili namna ya kuweka mfumo mzuri wa utoaji wa taarifa za kibiashara katika Bara la Afrika.

Alisema kuwepo na taarifa sahihi za kibiashara na zinazofanana katika Jumuiya za nchi za Afrika kutasaidia kukuza soko na hata biashara kufanyika kwa usahihi.

Alisema kusipokuwa na mfumo wa taarifa, Bara la Afrika litaendelea kuwa chini kibiashara, licha ya kwamba lina idadi kubwa ya watu.

“Licha ya Bara la Afrika kuwa na idadi kubwa ya watu na rasilimali nyingi, lakini mchango wake katika biashara duniani hauzidi asilimia 3, huku asilimia 14 tu ya biashara zikifanyika ndani ya nchi zilizopo katika Bara la Afrika, ikilinganishwa na asilimia 70 katika Bara la Ulaya.

“Kutokana na hali hiyo, inaonyesha kiwango chetu cha kufanya biashara wenyewe kwa wenyewe bado ni kidogo,  hivyo tunapaswa kujiwekea mifumo thabiti itakayokuza biashara  hizo,’’ alisema Prof. Mkenda.

Katibu Mkuu huyo alisema kupitia mkutano huo uliofadhiliwa na Umoja wa Afrika na Shirika la Misaada la Watu wa Marekani (USAID) na kuwakutanisha watu wengi kutoka katika nchi mbalimbali za Bara la Afrika, watajadiliana mambo mengi, ikiwamo kuangalia namna ya kukusanya taarifa pamoja na uwepo wa mfumo mzuri wa utoaji wa taarifa hizo za kibiashara na wafanyabiashara.

Alisema suala la biashara katika nchi ni jambo la muhimu, kwani unapokuwa nayo inachangia kuwavutia wawekezaji wengi kuja kuzalisha nchini.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Biashara cha Umoja wa Afrika, Nadir Merah, alisema mkutano huo ambao utakuwa wa siku tatu, pia utajadili namna ya kupata fedha za biashara na kuboresha miundombinu ya ufanyaji wa biashara Afrika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles