24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

JAJI MIHAYO AHOJI UBINAFSISHAJI HOTELI ZA WATALII

Na ASHA BANI -DAR ES SALAAM

MWENYEKITI wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Jaji Mstaafu Thomas Mihayo, amewahoji wadau wa utalii kama kulikuwa na ulazima wa kubinafsisha hoteli zote kubwa za kitalii.

Pia Jaji Mihayo alitaka kujua kama kuna uwezekano wa mashirika ya hifadhi za jamii kujenga hoteli mpya na za kisasa za aina hiyo ili kuvutia watalii.
Alisema maswali hayo ni kama changamoto kwa wadau wa utalii na yanahitaji majibu ili kusonga mbele.

Hayo aliyasema Dar es Salaam jana, wakati akiwahutubia wadau wa utalii kutoka Kanda ya Pwani, waliokutana Chuo cha Taifa cha Utalii kwa ajili ya kufanya mapitio ya Sera ya Utalii ya mwaka 1999, inayohitaji marekebisho ili kuendana na wakati uliopo.

Jaji Mihayo alisema katika sekta ya utalii kuna mambo mengi ambayo yanahitaji kuangaliwa kama changamoto, kwa namna moja ama nyingine yanaonekana madogo, lakini kiuhalisia yana umuhimu wa kukuza uchumi wa nchi.

Alisema wakati huu ambao Serikali inatoa fursa kwa wadau wa utalii kutoa maoni ya kuhuisha Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 1999, maswali hayo lazima yapatiwe majibu na ufumbuzi wa kudumu.
Alisema sera hiyo kwa mara ya kwanza iliandaliwa mwaka 1991 na kufanyiwa marekebisho mwaka 1999, ili kuendana na uchumi wa viwanda.

Jaji Mihayo alisema licha ya sera iliyopo kuonyesha mapungufu mbalimbali, lakini usimamizi wa Serikali umesaidia kuongeza mapato kutoka dola bilioni 1.7 mwaka 2012 mpaka dola bilioni 2.1 mwaka 2016.
Pia watalii wameongezeka kutoka watalii milioni 1.07 mwaka 2012 hadi watalii milioni 1.2 kwa mwaka 2016.

Alisema ili kuifanya Sekta ya Utalii kuwa endelevu, ni muhimu wadau hao wakajiuliza kama mitaala ya elimu inajumuisha ufahamu wa uhifadhi kuanzia elimu ya msingi, jambo ambalo ni muhimu kwenye maandalizi ya kizazi kitakachotangaza uhifadhi na utalii kwa ujumla kitaifa na kimataifa.
Kaimu Mkurugenzi wa Utalii kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Deogratius Mdamu, alisema utalii ni sekta yenye mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa taifa, ambapo mpaka sasa, asilimia 17 ya pato la taifa hutokana na sekta ya utalii.

Pia alielezea mchango wa sekta hiyo katika ajira, ambapo ina watu 1,500,000, ikiwa nyingine rasmi na zisizo rasmi pia.

Kwa mujibu wa Mdamu, hadi kufikia sasa wizara imefanikiwa kuwafikia wadau wa kanda ya kati, kanda ya ziwa, kanda ya magharibi, nyanda za juu kusini ambapo baada ya Pwani, watakwenda Kusini na Zanzibar, kabla ya kujumuisha maoni yote kwa ajili ya hatua zinazofuata.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles