Tamwa yataka usawa Uchaguzi Serikali za Mitaa

0
615

MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM

CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), kimevitaka vyama vya siasa kutoa fursa kwa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwakani.

Akizungumza katika ziara ya viongozi ya Tamwa ya kijitambulisha na kuimarisha ushirikiano, Mwenyekiti wa Tamwa Joyce Shebe, alisema wanawake wana nguvu katika uongozi hivyo vyama vya siasa vitoe fursa hiyo kwa usawa.

Alisema hali hiyo itasaidia wanawake kuingia kwenye ngazi za maamuzi badala ya kugeuka kuwa watazamaji wa nafasi za uongozi.

“Kuelekea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na ule Uchaguzi Mkuu wa mwakani, Tamwa tunashauri kwa vyama kutoa nafasi kwa wanawake. Kwani wana nguvu kubwa na waonyeshwe njia za kupita badala ya kuachwa nyuma,” alisema Shebe.

Pia alishauri kuwapo kwa usawa katika uongozi ndani ya vyumba vya habari kati ya wanawake na wanaume kama njia ya kulinda misingi ya usawa wa kijinsia.

“Nimetembea maeneo mengi, hapa MTANZANIA mko vizuri, tumeona usawa, wapo wanawake ambao ni wahariri, wakuu wa vitengo, lakini pia hili na maeneo mengine wanatakiwa kuiga mfano huu mzuri.

“Na hili mnaondoa ile dhana kwamba wanawake hawawezi, lakini kwa kukuta mhariri mwanamke ni kielelezo tosha sasa mnaenzi kwa vitendo usawa wa jinsia ambao sisi Tamwa tumekuwa tukipigia kelele miaka mingi,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Rose Ruben, alisema sasa umefika wakati kwa jamii kutambua kuwa sauti za wanawake zinatakiwa kusikika, ikiwamo kupewa nafasi katika vyombo vya habari.

Akizungumzia masuala ya usalama wa watoto, alisema kuwa Tamwa imekuwa ikiendesha mradi wa watoto, ikiwamo kupinga udhalilishaji, ubakaji na ulawiti kama njia ya kuwakinga.

“Suala la ulinzi wa watoto ni la jamii yetu na kutokana na umuhimu huo, sisi Tamwa tuna mradi wa habari za watoto ambao tunautekeleza katika Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.

“Lakini pia tumekuwa tukipinga na hata kutaka hatua zichukuliwe, hasa kwa wanaobaka na kudhalilisha watoto wa kike na hata kulawiti, pia si utamaduni wa nchi yetu,” alisema Rose

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here