De Bruyne aweka rekodi kufuzu Euro

0
559

GLASGOW, SCOTLAND

KIUNGO wa timu ya Ubelgiji, Kevin De Bruyne, ameweka rekodi ya kipekee ya kuwa mchezaji wa kwanza kupiga pasi tatu za mwisho kwenye mchezo mmoja wa kufuzu fainali ya michuano ya Euro.

Juzi timu hiyo ilishuka dimbani katika mchezo wa kufuzu fainali za Euro mwaka 2020 dhidi ya Scotland ambapo Ubelgiji ilifanikiwa kushinda mabao 4-0.

De Bruyne alikuwa kwenye kiwango cha hali ya juu huku akipiga pasi za mabao matatu pamoja na kufunga bao moja, hivyo kuingia kwenye historia mpya ya kuwa mchezaji wa kwanza kupiga pasi nyingi za mwisho kwenye mchezo mmoja.

Alianza kutoa pasi ya kwanza katika dakika ya tisa ambapo mshambuliaji wao Romelu Lukaku anayekipiga klabu ya Inter Milan alipachika bao kabla ya kufanya hivyo dakika ya 24 alipopiga pasi ya pili na bao likifungwa na Thomas Vermaelen.

Dakika ya 32, De Bruyne alipiga pasi nyingine ya bao lililofungwa na beki anayekipiga Tottenham, Toby Alderweireld, kabla ya yeye mwenyewe kupachika bao dakika ya 82.

Ushindi huo wa juzi unawafanya Ubelgiji kuwa mchezo wao wa sita katika kundi lao kushinda michezo yote hivyo kuwa vinara wa kundi I wakifuatiwa na Urusi ambao wameshinda michezo yote na kufuzu kushiriki fainali.

Katika michezo 14 waliocheza Scotland dhidi ya Ubelgiji wamekuwa wakipata wakati mgumu wa kushinda wakiwa wameshinda mchezo mmoja, wakatio sare mara mbili na kufungwa mara 11. Mara ya mwisho kushinda ilikuwa Oktoba 1987 kwa ajili ya kufuzu Euro 1988.

De Bruyne sio mara yake ya kwanza kuhusika kwenye mabao katika ushindi dhidi ya Scotland. Mchezaji huyo amehusika katika jumla ya mabao saba ya kuifunga Scotland kati ya michezo minne aliyocheza dhidi ya wapinzani hao akifunga mabao mawili na kutoa pasi tano za mwisho.

Kiungo huyo wa Manchester City, tayari ameanza kuuonesha moto wake kwenye msimu huu baada ya kucheza michezo minne ya Ligi Kuu England akifunga bao moja na kutoa pasi tano za mwisho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here