24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

TAMKO LA TRUMP KUINGILIA KIJESHI VENEZUELA LASHUTUMIWA

BUENOS AIRES, ARGENTINA

JUMUIYA ya Uchumi ya Nchi za Amerika Kusini (Mercosur), imemshutumu Rais wa Marekani Donald Trump kwa tamko lake la kufikiria kuchukua hatua za kijeshi kumaliza mzozo wa kisiasa nchini Venezuela.

Argentina imesema mashauriano na diplomasia ndizo njia pekee za kuendeleza demokrasia Venezuela.

Wizara ya mambo ya nje ya Venezuela imesema tamko la Trump lilikuwa la uchokozi na kuikosea heshima nchi hiyo na kwamba linatishia kuvuruga uthabiti Amerika Kusini.

Maandamano yaliyokumbwa na ghasia ambayo yamekuwa yakiendelea tangu Aprili mwaka huu yamesababisha vifo vya watu 120 nchini humo.

Bunge jipya shirikishi la Rais Nicolas Maduro, ambalo lina mamlaka ya kuifanyia marekebisho Katiba pamoja na uwezo wa kubatilisha maamuzi ya Bunge la kawaida linalodhibitiwa na upinzani, limeshutumiwa na wengi.

Mercosur, ambayo hujumuisha Argentina, Brazil, Paraguay na Uruguay  iliisimamisha uanachama cha Venezuela wiki iliyopita.

Nchi nyingine za Amerika Kusini pia zimemshutumu Trump, zikiwemo Mexico, Colombia na Peru, na kueleza kwamba tamko lake hilo linaenda kinyume na kanuni za Umoja wa Mataifa.

Hata hivyo, Peru imekuwa mkosoaji mkubwa wa Serikali ya Rais Maduro.

Ijumaa iliyopita Peru ilimfukuza Balozi wa Venezuela baada ya Serikali ya Venezuela kutoa jibu lisiloridhisha kwa Mercosur ikijitetea kuhusu Bunge shirikishi.

Rais wa Peru Pedro Pablo Kuczynski alitoa wito kwa Maduro kujiuzulu na kumuita dikteta.

Ijumaa jioni, Trump aliwaambia wanahabari kuwa Marekani ina njia nyingi za kushughulika na Venezuela, ikiwemo kuingilia kijeshi itakapobidi.

“Watu wanateseka huko na wanafariki dunia,” aliongeza.

Hivi karibuni Marekani ilimuwekea vikwazo Maduro ikimuita dikteta.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles