31.2 C
Dar es Salaam
Saturday, December 2, 2023

Contact us: [email protected]

TACAIDS, UN-WOMEN wanavyonusuru Wanawake na saratani ya mlango wa kizazi

Na Faraja Masinde, Kagera

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Saratani ni mabadiliko ya ukuaji wa seli au chembechembe hai na yaweza tokea sehemu yoyote ya mwili (seli hukua na kuongezeka idadi kwa haraka sana).

Aidha, kuna aina nyingi ya za saratani ikiwamo ile ya mlango wa kizazi ambapo tafsiri ya Wizara hiyo inasema kuwa Saratani ya mlango wa kizazi (cervix) ni mabadiliko ya ukuaji wa seli za mlango wa kizazi.

Kwa mujibu wa wataalamu, aina hii ya saratani inaweza kusambaa na kuweza kushambulia kibofu cha mkojo, uke na sehemu ya chini ya utumbo mkubwa na baadaye figo, ini na sehemu zingine za mwili na kusababisha kifo.

Huku kwa Tanzania ndiyo saratani inayoongoza kusababisha vifo kwa wanawake wengi ambapo asilimia 70 huripoti wakiwa wamechelewa sana.

Visababishi vyake

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, miongoni mwa visababishi vya saratani hiyo ni kuanza kujamiana katika umri mdogo, kuwa na wapenzi wengi, kuwa na ndoa za mitala, kuzaa watoto wengi na uvutaji sigara.

Dalili za Saratani

Dalili za saratani ya mlango wa kizazi ni pamoja na kutokwa damu bila mpangilio au kutokwa damu baada ya kujamiana kwa wanawake, maumivu ya mgongo, miguu na au kiuno, kuchoka, kupungua uzito na kupungikiwa hamu ya kula.

Dalili nyongine ni kutokwa na uchafu kwenye uke wa majimaji, uliopauka wa rangi kahawia au wenye damu na kuvimba mguu mmoja huku dalili mbaya zaidi zinazoweza kujitokeza zikiwa ni kuishiwa damu, figo kushindwa kufanya kazi, kupatwa na fistula, na uvimbe wa tezi.

Kinga

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, kinga ya awali ni pamoja nakupata chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi (HPV vaccine), kubadili tabia, kuepuka ngono katika umri mdogo, kuepuka uvutaji wa sigara ikiwemo pia kuepuka kubeba mimba katika umri mdogo na kuwa na mwenzi mmoja mwaminifu.

Hata hivyo changamoto ni kwamba siyo wanawake wote wenye uwezo wa kuelewa dalili hizo na namna ya kujikinga na saratani hii ya mlango wa kizazi.

Hii ni kutokana pengine na ukosefu wa elimu, uzembe, changamoto za kifedha na sababu nyingine na hivyo kujikuta kwamba taifa likipoteza watu wengi kila mwaka sababu ya saratani hii ya mlango wa kizazi.

Changamoto hiyo ndiyo inaisukuma Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) kwa kushirikiana na Asasi ya Kiraia ya Akina Mama Wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi mkoani Kagera (AMWAVU) chini ya ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Uwezeshaji wa Wanawake (UN-WOMEN) kuja na mradi wa kuhamasisha wanawake wanaoishi na virusi vya ukiwmi (WVVU) kupima saratani ya mlango wa kizazi na kupata matibabu stahiki mapema katika mkoa wa Kagera.

Judith Luande ni Afisa Jinsia kutoka Tacaids, ambapo anafafanua sababu za mradi huo kuanzia mkoani Kagera.

Afisa Jinsia kutoka Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Judith Luande, akifafanua jambo| Picha na Maktaba.

“Lengo la mradi huu wa saratani ya malango wa kizazi kuanzia Kagera ni kwasababu tunaona kwamba wanawake wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi wako katika hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizi ya ugonjwa huu.

“Ukiangalia umri wa maambukizi nimakubwa kwa wanawake walio kati ya umri wa miaka 35 hadi 49. Na pia ukiangalia maambukizi ya saratani ya mlango wa kizazi unaona kwamba wanawake wengi wako kati ya umri wa miaka 30 hadi 50.

“Hivyo, tukaona kuna uhusiano mkubwa kati ya maambukizi ya VVU na ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi na ndio sababu kuu ya kuanzia mkoani Kagera kufuatia kuwa na takwimu za juu za maambukizi ya VVU,” anasema Judith.

Kwa nini saratani ya mlango wa kizazi?

Judithi anasema kuwa kwa kuzingatia kuwa yeye ndiye Afisa Jinsia anayeratibu maswala ya jinsia katika tume ya kudhibiti Ukimwi, TACAIDS wakaona ni vyema kuzingatia hilo ili kuweza kupunguza vifo vinavyotokana na saratani ya mlango wa kizazi.

“Hiyo ndio sababu tukafikiria kuanzisha mradi ambao unalenga kuhamasisha wanawake kujitokeza kufanyiwa uchunguzi kwa sababu sisi tume wajibu wetu ni kuhamasisha jamii iweze kupata matibabu, eneo la tiba ni la wizara ya afya.

“Hivyo, tukaona kwamba ni vyema tutafute wadau tufanye nao kazi katika mtazamo huo, tuliandika mradi na ndipo tukapata wafadhili ambao ni UN-WOMEN wakatufadhiri,” anasema Judith.

Kwa nini Kagera

Judith anasema kuwa kutokana na takwimu za hali ya maambukizi ya virusi vya ukimwi kuuweka mkoa wa Kagera kwenye mikoa yenye idadi kubwa ya maambukizi, ndiyo sababu iliyowasukuma kuanzia mkoani humo.

“Iko bayana kwamba kwa mujibu wa takwimu za kitaifa juu ya maambukizi ya VVU, mkoa wa Kagera umekuwa na idadi ya juu ya maambukizi na hii ndiyo sababu tukaanzia huku.

“Kwani pia takwimu zinaonyesha kuwa maambukizi ya ugonjwa huu wa saratani ya mlango wa kizazi upo kwa kiwango kikubwa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa,” anasema Judith.

Takwimu za hali ya maambukizi nchini za mwaka 2020 zinaonyesha kuwa maambukizi ya VVU kwa mkoa wa Kagera ni asilimia 6.5.

“Pamoja na kwamba katika Afrika, nchi za Afrika Mashariki zinaongoza kwa aina hii ya saratani lakini Tanzania ina kiwango kikubwa cha maambukizi huku mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwa kwenye hatari zaidi ikiwamo Kagera.

“Kwa hiyo kutokana na ukweli huo, tukaona ni vyema tuanzie hapa, sisi kama waratibu tukaona kwamba tuangalie ni nani ambaye ana afua au muingiliano ambazo zina mlengo huo, tukakuta kwamba kwa Kagera kuna Asasi ya AMWAVU ambayo lilikuwa tayari,” anasema Judithi na kuongeza kuwa:

“Lakini pamoja na kuangalia kwamba kuna mtando wa wanawake wanaoishi na virusi vya Ukimwi katika mkoa wa Kagera, tuliangalia mbele zaidi tukaona kwamba wale wasichana wa rika balehe na wanawake wadogo je, wako wapi?

“Tukabaini kuwa ni vyema katika mradi huu tuzingatie kuangalia pande zote mbili za wanawake ambao ni watu wazima (30-49) lakini pia tuzingatie hawa walio miaka ya 30 kurudi chini au 25 kurudi chini pamoja na wasichana wadogo, tuanze kuwajengea uwezo wa kujitambua juu ya aina hii ya saratani na namna ya kujikinga,” anasema Judith.

Kagera kuwa mkoa wa mfano

Aidha, katika maneno mengine, Judithi anasema kuwa mradi huu unafanyika wilayani Bukoba ukiwa ni wa majaribio lengo ni kufikia maneo yote ya mkoa wa Kagera.

“Tunatekeleza mradi huu hapa Kagera kama sehemu ya majaribio huku tukitarajia baadae tuweze kwenda na mikoa mingine. Kwa hapa Kagera ni imani yetu kuwa tutakapoweza kupata rasilimali za kutosha tutaenda mkoa mzima katika halmashauri nyingine zote,”anasema.

Nini sababu

Judith anafafanua kuwa pamoja na mambo mengine, bado mila hatarishi na desturi za eneo husika imekuwa ni chanzo cha kuenea kwa maambukizi na kusisitiza kuwa jamii inapaswa kuamka na kuhakikisha kuwa inakuwa salama.

“Ukiangalia sanasana ni mila hatarishi na desturi za maeneo husika ndizo zinaweza ikawa ni chanzo kikubwa pamoja na maswala ya ukatili wa kijinsia ndio maana tumeona kwamba twende kwa mtazamo wa kijinsia tuangalie hilo eneo la saratani ya mlango wa kizazi.

“Pia tutaendelea kuangalia sababu ambazo ni mila na desturi hatarishi na tumeandaa majadiliano ambapo watu wanajadili na kuainisha hizo mila hatarishi ili kuziondoa katika ngazi ya jamii,” anahitimisha Judith.

Mratibu wa Programu za Ukimwi na Jinsia kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia uwezeshaji wa Wanawake, (UN-WOMEN), Jacob Kayombo, anaihimiza jamii hususan wanawake kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.

“Hivi karibuni tumeanza program nyingine za kuhamasisha jamii kushiriki katika maswala ya upimaji wa saratani ya mlango wa kizazi.

“Kimsingi tunaowahamasisha ni wakina mama tukiwa na malengo ya kuwapa elimu na baadaye kuwajengea uwezo wa kuona kuwa wanapaswa kwenda kupima na kutambua hali zao ili kwa wale ambao wanakuwa na dalili za awali za saratani ya mlango wa kizazi wapate matibabu na kwa wale wengine ambao wanaweza wakawa pia hata kwenye dalili ambazo zinakuwa ni za juu zaidi wapate pia matibabu.

“Lakini kwa wale ambao wanakuwa hawana dalili za saratani hii waweze kupata elimu endelevu lakini pengine kuelimishwa zaidi namna gani ambavyo wanaweza wakaepukana na saratani ya mlango wa uzazi,” anasema Kayombo.

Kayombo anafafanua zaidia kuwa UN Women ni shirika la Umoja wa Mataifa ambalo lina wajibu na dhamana ya kuhamasisha maswala ya usawa wa kijinsia duniani lakini pia ni kwa namna mbalimbali linashughulika na maswala ya uwezeshaji wa akina mama.

“Katika shirika letu, tuna maeneo mengi ya uwezeshaji wa kina mama, lakini tunaporudi katika sekta ya afya, hasa hapa nchini Tanzania tunashughulika na program za Ukimwi pamoja na saratani ya mlango wa uzazi.

“Programu hii ya saratani ya mlango wa kizazi haina muda mrefu sana lakini kwa upande wa Ukimwi tumekuwa tukifanya kazi kwa miaka kadhaa na TACAIDS. kwa kipindi cha kuanzia mwaka jana (2020) ndio tuliona sasa kutokana na taarifa tulizozipata kutoka kwa wenzetu wa tume na kitengo cha saratani ya mlango wa kizazi.

“Lakini pia kutoka kwa wadau mbalimbali ilionyesha kwamba kuna uhitaji sasa sisi pamoja na yale tunayoyafanya katika kuhamasisha uingizaji wa maswala ya kijinsia katika udhibiti wa Ukimwi au muitikio wa Ukimwi kitaifa kwamba ilionekana ni vizuri sasa tuchangie kama sehemu ya kuhamasisha jamii kuweka programu ya maswala ya saratani ya mlango wa uzazi,” anasema Kalyombo.

Mratibu wa Programu za Ukimwi na Jinsia kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia uwezeshaji wa Wanawake, (UN-WOMEN), Jacob Kayombo.

Anafafanua kuwa kwa sababu hiyo, serikali pamoja na wadau walikuwa tayari wametoa taarifa na wameona kwamba katika eneo la mkoa wa Kagera kulikuwa ana uitaji mkubwa na ndio sababu ya kampeni hiyo kuanzia mkoani humo.

“Uhitaji mkubwa mkoani Kagera unatokana na ukweli kwamba kuna maambukizi ya VVU kwa kiasi ambacho siwezi kusema ni kikubwa sana kwa taifa, lakini hatuwezi tukasema kimetosha kwa jitihada ambazo zinafanywa katika kupunguza maambukizi katika taifa letu.

Kayombo anasema, sababu yakuwapo na mahusiano makubwa kati ya saratani na VVU miongoni mwa wanawake ilionekana pia saratani ya mlango wa kizazi imeshamiri kwa kiasi fulani miongoni mwa wanawake wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi katika maeneo ya Ukanda wa Ziwa Victoria ikiwemo mkoa wa Kagera.

“Ndio maana ikaonekana ni vizuri tuungalie mkoa wa Kagera kipekee inawezekana ikawa ni sehemu ya kuanzia ili baadae tufike mikoa mingine lakini tunadhani kwamba kwa rasilimali tulizonazo tuliona tutaweza kufanya vizuri tukianza mkoa huu.

“Sambamba na hayo mkoa huu umekaa vizuri kwenye upande wa miundombinu ya kiutawala na kiuongozi pamoja na uwekezaji ambao umeshafanya katika sekta ya afya.

“Kwani tayari kuna uongozi ambao unaongozwa na Mkuu wa mkoa pamoja na timu yake ambayo imefanyakazi nzuri ya kuhamasisha watu kuwa na muitikio mzuri katika maswala ya afya,”anasema Kayombo.

Aidha, Kayombo anakiri kuwa uhusiano mzuri baina ya wadau na mkoa ndio imekuwa nyenzo nyingine muhimu ya kuanzia mkoani humo.

“Hii imesaidia hata kuonyesha kwamba hata tunapoenda katika jamii hatupati shida sana kama unaenda mahala ambapo hakuna uhamasishaji. Kitu kingine kizuri katika mkoa huu ni hamasa inayotokana na kazi za asasi za kijamii. Na kwa sasa tunafanya kazi na asasi ya AMWAVU ni asasi ambayo inashughulika na inaongozwa na wamama wanaoishi na virusi vya Ukimwi.

“Tumeanza sisi UN Women kutoa fedha kwa serikali kupitia TACAIDS ambayo imekaa na AMWAVU pamoja na uongozi wa mkoa wa Kagera wameratibu ni namna gani ambavyo wanaweza wakaelekeza utekelezaji wa kazi hizi ikiwa na maana ni makundi gani wanayafikia, kwa utaratibu gani na wanafikaje katika jamii,” amesema Kayombo.

Mkoa wajipanga

Rebeca Gwambasa ni Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Kagera ambapo anasema kuwa Wanawake 30,907 mkoani humo   wanatarajiwa kufanyiwa uchunguzi kwenye kampeni hiyo kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Moses Machali.

Rebeca anasema kutokana na watu wenye maambukizi ya Ukimwi kushambuliwa zaidi na saratani, mkoa huo unatarajia kuwafanyia uchunguzi wa mlango wa kizazi wanawake 600 wenye maambukizi ya ukimwi kupitia mradi maalumu unaowalenga wanawake hao na kuwapatia matibabu.

“Kupitia mradi huu uliofadhiliwa na UN Women tunatarajia kuwafikia wanawake wengi zaidi, wanawake wengi hawana taarifa juu ya saratani hivyo kupitia mradi huu itakuwa rahisi kuwapata na kujua wapi watapata huduma,”anasema Rebeca.

Rebeca anasema tayari wanawake 13, 000 sawa na asilimia 35 kufikia mwezi Agosti wenye umri kuanzia miaka 30 hadi 50 wamefanyiwa uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi.

Kwa mujibu wa Rebeca takwimu zilizopo hadi sasa mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia hali inayochangia ongezeko la wagonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi.

“Watu wengi wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia wanaambukizwa virusi vya ukimwi, hivyo wanapopata maambukizi inakuwa ni rahisi kwao kupata saratani ya mlango wa kizazi sababu kinga yao ya mwili inakuwa chini,” anasema Rebeca.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles