Sven awashtukia nyota wake

0
671

Theresia Gasper – Dar es Salaam

KOCHA Mkuu wa Simba, Sven VanderBroeck, amesema licha ya kupata matokeo katika mechi zao za Ligi Kuu Tanzania Bara, wachezaji wake wanaonekana kuwahi kuchoka sana.

Simba juzi iliendeleza wimbi la ushindi baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Namungo FC, katika mchezo wao wa Ligi Kuu Bara, uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Timu hiyo kwa sasa inakabiliwa na mchezo dhidi ya Mbeya City, Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo, VanderBroeck, alisema licha ya mchezo kuwa mgumu walipambana ndani ya dakika 90 na kumaliza mchezo wakiwa na pointi tatu.

“Tumepambana japo tulikosa mabao mengi, lakini hata hivyo leo baadhi ya wachezaji hawakuwa vizuri na ndio maana nikafanya mabadiliko,” alisema.

Alisema licha ya wapinzani wao kusawazisha bao hawakuweza kukata tamaa zaidi ya kuendeleza mashambulizi na kupata bao dakika za majeruhi.

VanderBroeck alisema baada ya mchezo huo amebaini baadhi ya kasoro hivyo ataenda kuzifanyia kazi kabla ya mchezo unaofuata.

Alisema mipango yao ni kuendelea kupata ushindi kwa kila mchezo kwani kwa sasa kila timu wanayokutana nayo inaonekana kupambana na kufanya mchezo kuwa mgumu.

Baada ya ushindi wa juzi Simba imeendelea kujikita kileleni katika msimamo wa ligi wakijikusanyia pointi 44 baada ya kucheza michezo 17 na kushinda 14 huku sare zikiwa mbili na kupoteza mara mbili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here