20.5 C
Dar es Salaam
Saturday, August 20, 2022

Sumaye: Kifo cha Mkapa kinasitikisha

MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM 

WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye ambaye alifanya kazi kwa miaka 10 yote na Rais wa awamu ya tatu, Benjamin  Mkapa, amesema kifo cha kiongozi huyo ni cha kusikitisha.

Alisema mara ya mwisho kukutana na Mkapa ilikuwa zaidi ya wiki moja iliyopita kwenye vikao vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Dodoma kwa ajili ya kupitisha wagombea urais wa chama hicho.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi jana kwa njia ya simu, Sumaye alisema Taifa limempoteza kiongozi mahiri ambaye viongozi wengine walikuwa wanakwenda kwake kuchota hekima na maarifa.

Akizungumzia miaka 10 ya uongozi wake, alisema Mkapa aliikuta nchi kwenye mazingira magumu na aliiacha kwenye mazingira mazuri, uchumi ukiwa umeimarika.

“Kupitia sera yake ya ukweli na uwazi, alijitahidi kuimarisha uchumi na alikuwa na utaratibu wa kila mwezi kulieleza Taifa kuhusu hali ya nchi ilivyo na inakoelekea,”.

Sumaye ambaye alikuwa Waziri Mkuu katika utawala wa Mkapa kutoka  mwaka 1995  hadi 2005 alisema wakati wa  utawala wa kiongozi huyo hata gharama za maisha zilikuwa hazipandi kwa kuwa alidhibiti uchumi vizuri.

“Wakati wa Mkapa ziliwekwa sera rafiki  kwa wawekezaji na wafanyabiashara, sekta binafsi zilipewa kipaumbele, na haya mambo yalikuwa  nyuma ya mafanikio yetu kiuchumi japo changamoto zilikuwepo”.

Alipoulizwa ni mambo gani mazuri na magumu anayoyakumbuka, Sumaye alisema ni mengi na ni vigumu kuorodhesha moja moja.

“Katika utawala kuna vitu vingi, kwa mfano nimekueleza kuhusu hali ya uchumi ilibadilika sana, sasa katika mafanikio kuna machungu kwa mfano kwa upande wa watumishi wa umma tulipunguza watu sana na kulikuwa na malalamiko, lakini uchumi uliimarika.

Sumaye mbali na kusifia utawala bora wa Mkapa pia anakumbuka mabadiliko mengi yaliyofanyika ambayo nyuma yake yalikuwa na mchango kwenye uchumi ikiwamo  uamuzi wa kubinafsisha mashirika ya umma.

Akizungumzia utendaji kazi kati yake  na Mkapa, Waziri Mkuu huyo alisema   ni  mtu ambaye alikwenda naye vizuri katika uongozi.

“Ni mtu aliyekuwa hakuingilii katika majukumu ya kazi zako, alikuwa anakuacha ufanye kazi zako mwenyewe bila kukuingilia.

Alipoulizwa kuhusu taswira ya ukali na maamuzi magumu aliyokuwa nayo Mkapa, Sumaye alisema;

“Ni kweli alikuwa mtu mkali na mwenye hasira lakini alikuwa hakasiriki ovyo tena bila sababu.

“Kama utafanya yale aliyoelekeza au yale yanayohitajika alikuwa si mkali alikuwa ni mtu ambaye anajua wapi lazima awe mkali.”

Alipoulizwa iwapo kama anakumbuka kuna siku alimfokea kwa kufanya jambo tofauti Sumaye alijibu; “hiyo sikumbuki, haijawahi kutokea.”

Sumaye ambaye katika Uchaguzi Mkuu  wa mwaka 2015 alihama CCM na kuhamia chama cha upinzani cha Chadema kabla ya mwaka jana kurejea tena ndani ya chama hicho, alipoulizwa iwapo uamuzi huo ulimkasirisha bosi wake huyo wa zamani alisema anaamini hakufurahi.

Alisema japo hawajawahi kukutana na kuzungumza juu ya jambo hilo lakini uamuzi wa yeye kuhamia upinzani anaamini haukumfurahisha si tu Mkapa bali hata wazee wengi wa CCM na walijua kwamba wakati anaondoka si kwamba alikuwa amekichukia chama hicho bali mwenendo wa baadhi ya mambo wakati huo.

Alipoulizwa iwapo Mkapa alimwita kuzungumzia jambo hilo hata baada ya kuonekana katika moja ya kampeni wakati huo akiwaita wapinzani ni malofa, Sumaye alisema hajawahi kumwita hata mara moja.

Hata alipoamua kurudi CCM, Sumaye alisema hakupata kukutana na Mkapa kwa ajili ya kuzungumzia juu ya jambo hilo.

“Hakuniita, hatukulizungumza, hata nilipotoka upinzani niliita waandishi wa habari na nikazungumza kila  kitu lakini hatujawahi kuzungumza juu ya jambo hilo.

Alipoulizwa kama walipokutana Dodoma hivi karibuni alipata wasaa wa kuketi naye pamoja na kuzungumza mambo mawili, matatu, Sumaye alisema; “Hatukukaa pamoja”.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
199,058FollowersFollow
551,000SubscribersSubscribe

Latest Articles