31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Maura amwelezea Mkapa ukali, upole, ucha Mungu

RATIFA BARANYIKWA, DAR ES SALAAM

ALIYEKUWA Mwandishi wa habari wa  Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, Maura Mwingira, amesema amepokea taarifa za kifo cha kiongozi huyo kwa mshtuko kwa sababu hakukuwa na taarifa za kuumwa na hapo kabla alionekana kwenye vikao vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dodoma akiwa na afya njema.

Maura anaandika historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kuteuliwa kuwa mwandishi wa Rais tangu nchi ipate uhuru mwaka 1961, amefanya kazi na Mkapa tangu mwaka 1998 hadi 2005 kiongozi huyo alipomaliza muda wake.

“Mimi nimebahatika kuwa   kufanya kazi na Mkapa kutoka mwaka 1998-2005  nilipomaliza kipindi hicho nilimfahamu kwa karibu Mzee Mkapa.

Amemwelezea kiongozi huyo kama mtu aliyekuwa mkali kwa yeyote aliyekwenda kinyume na majukumu ya kazi.

“Lakini anayethamini, mwenye kusamehe, mwenye hofu ya Mungu, mwalimu na mtu aliyewapenda Watanzania kwa dhati”.

Maura ambaye alisema hata kabla hajateuliwa kwenye nafasi hiyo alikuwa hafahamiani na Mkapa, na huenda alimchukua kwa sababu ya bidii yake ya kuandika makala wakati huo akiwa Idara ya Habari Maelezo,

anasema katika kipindi chote alichofanya kazi na Mkapa amejifunza mengi na mengine yamemfanya awe hivyo alivyo leo. 

Maura kwa sasa yupo Wizara ya Katiba na Sheria na hapo kabla aliwahi kuhudumu katika utawala wa Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kama Mwandishi wake wa habari msaidizi kabla ya kumuhamishia New York Marekani kwenye ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.

Anasema Mkapa alikuwa baba na kiongozi ambaye ukifanya vizuri anathamini.

Katika hilo anasema Mkapa ambaye naye kwa fani alikuwa Mwandishi wa Habari alikuwa ni mwelewa, na mwalimu mzuri.

Kwa mujibu wa Maura, Mkapa alipenda kusoma sana vitabu, hakuwa mtu wa soga.

“Alinifanya hata mimi nipende kusoma  kuna wakati alinipatia kitabu nadhani cha Mwandishi wa kwanza wa Rais wa Marekani Bill Clinton”

TASWIRA YAKE VYOMBO VYA HABARI 

Alipoulizwa kuhusu taswira ya Mkapa  kuchukia waandishi wa habari wa ndani ya nchi, Maura alisema si kweli kama  kiongozi  alikuwa hawapendi au havipendi vyombo vya habari.

Alisema Mkapa alikuwa anawapenda sana waandishi wa habari isipokuwa alikuwa anachukizwa na baadhi kutofanya utafiti, uchambuzi wa kina, kutosoma na kujiandaa kabla ya mkutano.

“Alikuwa karibu na waandishi hata safari za nje nadhani yeye ndiye alianzisha kusafiri na waandishi hata zile za mikoani, changamoto ilikuwa wakati tukiitisha press conference ( mkutano na vyombo vya habari) tulikuwa tunauliza maswali ambayo hatujafanya utafiti, hatujasoma, hatujiandai vizuri.

Kuhusu kupenda vyombo vya habari vya nje; Maura alisema si mara zote alikuwa anazungumza na vyombo vya habari vya nje na si kweli kama alikuwa anavipendelea vyombo  hivyo.

Pamoja na hilo Maura alisema Mkapa alikuwa haendi kula chakula cha jioni pasipo kusikiliza taarifa ya habari.

“Kwa sababu yeye pia alikuwa ni  Mwandishi wa Habari, likitokea kosa pia alikuwa anapiga simu kwenye chumba cha habari, alikuwa anasoma sana magazeti hadi barua za wasomaji na wakati mwingine anakwambia Maura mtafute huyu,”.

UKARIBU NA MUNGU

Kuhusu ukaribu na Mungu alisema kila Jumapili Mkapa alikuwa hapendi kukosa kwenda kanisani.

“Alikuwa mcha Mungu, Jumapili hata ikitukuta tuko mikoani hatuanzi safari bila kwenda Kanisani kwanza, hiyo ilitujenga kiimani, lakini pia aliwajali na kuwapenda Watanzania.

UKALI KWENYE KAZI, MPOLE, MCHESHI 

Maura alisema Mkapa alikuwa mkali kwenye kazi hasa kama umekosea tofauti na hapo alikuwa mpole, mcheshi na mtu mwenye vichekesho.

Alisema Mkapa pia alikuwa ni kiongozi ambaye alikuwa mwelewa na anayesamehe.

Alitolea mfano wakati alipofanyiwa upasuaji wa nyonga, gazeti moja lilipofuatilia taarifa hiyo, siku ya pili lilikuja na kichwa cha habari cha ajabu tofauti na alivyoeleza.

“Hilo gazeti lilikuwa la Jumapili alipomaliza kukutana na wageni aliniita akaniuliza nimeona gazeti nini kimetokea? Nikamweleza  akaniambia unajua wamekuharibia sana? Nikamwambia naomba msamaha, akasema nenda kafanye kazi, kwa kiongozi mwingine ungefukuzwa kazi,”  alisema Maura.

Alisema pamoja na kwamba ana vitu vingi vya kukumbuka kwa Mkapa lakini kitendo cha kumpa fursa ya mwanamke  wa kwanza, kilitoa hamasa kwa wanawake wengine waandishi wa habari kuteuliwa kwenye nafasi hiyo kama akina Penzi Nyangumi, Irene na wengine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles