23.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 10, 2022

Sumatra CCC yakosoa sheria ya barabarani

Nicholous Kinyariri
Nicholous Kinyariri

CHRISTINA GAULUHANGA NA TUNU NASSOR, DAR ES SALAAM

BARAZA la Watumiaji Huduma za Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra CCC), limeikosoa Sheria ya Barabarani ya mwaka 1973 na ile ya Bima ya mwaka 2009, zinazosimamia ulipwaji fidia kwa waathirika wa ajali za barabarani kuwa zimepitwa na wakati.

Pia limesema sheria hizo si rafiki, hazimsaidii mwananchi wa kipato cha chini pindi anapopata matatizo ya ajali kwa sababu ya matakwa ya sheria.

Akizungumza na MTANZANIA jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Elimu wa Sumatra CCC, Nicholous Kinyariri, alisema Sheria ya Bima haitamki wazi gharama za kulipwa fidia waathirika wa ajali za barabarani, jambo ambalo limekuwa likichangia waathirika wengi kukosa haki zao.

Alisema sheria hizo zimekuwa zikihitaji vielelezo, vikiwemo cheti cha mahakama, taarifa ya hospitali inayoonyesha ripoti ya daktari kuonyesha kiwango cha athari kwa mlengwa wa ajali hiyo, mchoro wa ajali, tiketi, taarifa za polisi na kitabu cha majina ya wasafiri waliokuwepo ndani ya gari lililopata ajali kama ni la abiria.

“Changamoto za ulipwaji fidia kwa waathirika wa ajali ni kukosekana kwa vielelezo vya ajali husika na hii inatokana na sheria zilizopo, jambo ambalo wengi wamekuwa wakipoteza haki zao kwa kuepuka usumbufu,” alisema Kinyariri.

Kinyariri alisema pia makampuni mengi yanayotoa huduma za bima ya ajali yana ofisi katika jiji la Dar es Salaam pekee, hali ambayo inawanyima fursa waathirika wengi kufuatilia bima zao pindi wanapopata ajali kwa kuhofia umbali wa maeneo wanayoishi.

“Yapo makampuni mengi ya bima, lakini ndani ya jiji la Dar es Salaam, hivyo kama mtu amepata ajali Mkoa wa Pwani na yeye anaishi Mbeya au mkoa mwingine wowote anaona mbali kufuatilia malipo ya fidia ya ajali yake kwakuwa atatakiwa kukusanya vielelezo Pwani na kuvipeleka makao makuu ya mashirika ya bima ambapo hutumia gharama nyingi,” alisema Kinyariri.

Alisema ofisi yao imepokea mafaili 76 ya waathirika wa ajali ambao wanadai fidia, lakini hadi sasa waliopata ni watano tu, ambao ndio walikidhi vigezo.

Kinyariri alisema ifike wakati sheria hizo zizingatie weledi wa dereva kwa kumbana kuonyesha uzoefu wake katika kuhudumia wasafiri, hasa waendeshao mabasi ya abiria.

“Yapo matatizo mengi ambayo yanaonyesha ipo haja ya kufanya mabadiliko ya sheria na wananchi kuwezeshwa kufahamu umuhimu wa kudai haki yao ya bima pindi wanapopata ajali, hali inayochangia kila kukicha wengi kupoteza haki zao za kulipwa fidia,” alisema Kinyariri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,395FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles