NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM
UONGOZI wa timu ya Stand United umewafungulia mashtaka mashabiki wa timu hiyo kwa kitendo kibaya walichokifanya cha kumvamia na kutaka kumpiga Kocha Mkuu Patrick Liewig juzi, baada ya kumalizika mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mwadui FC Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
Stand ilimaliza mchezo huo kwa kupokea kichapo cha mabao 2-0, kitendo kilichoamsha hasira za mashabiki na baadhi yao kumvamia kocha huyo.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Msemaji wa timu hiyo, Deo Kaji, alisema tayari wameshawafungulia mashtaka Polisi Kituo cha Kati mkoani humo mashabiki walioonekana kumvamia kocha.
“Hatujafurahishwa kabisa na kitendo hicho, tunatoa onyo kwa kitendo cha mashabiki kumvamia kocha kisirudiwe, hakuna aliyeyafurahia matokeo yale, lakini mbona sisi tulikuwa wavumilivu na kwanini wao wamfanyie fujo kocha, nashangaa kwanini wanashindwa kuelewa kama soka ni mchezo wenye matokeo ya aina tatu, kushinda, kushindwa na droo.
“Kwa utovu huo wa nidhamu waliouonyesha, tayari tumewashtaki wale walioonekana kumfuata kocha na tunaiacha sheria ichukue mkondo wake na hii iwe fundisho kwa wote,” alisema.
Akizungumzia mchezo huo, alisema wamepokea matokeo kwa masikitiko, hivyo wanahitaji kujipanga zaidi kwa ajili ya kupata ushindi kwenye mchezo ujao.