NA JENNIFER ULLEMBO, DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa timu ya Simba, Dylan Kerr, amesema kwa sasa anaweza kutembea kifua mbele baada ya kikosi chake kuanza kukaa katika mstari ulionyooka katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Jeuri ya Mwingereza huyo imekuja baada ya Simba kuonyesha kiwango cha hali ya juu katika mchezo wao dhidi ya Azam, uliokwisha kwa sare ya mabao 2-2, huku mshambuliaji wao, Danny Lyanga, aking’ara vilivyo.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Kerr alisema awali walipokuwa kambini visiwani Zanzibar, alitamani kumuona mchezaji huyo akionyesha ubora wake katika mechi za ligi.
“Unajua mwalimu huwa anafarijika anapoona wachezaji wakitekeleza maelekezo aliyowapa, Lyanga na wachezaji wengine walijituma na kila mtu ameshuhudia jinsi tulivyowatoa jasho Azam, ambao ni vinara wa ligi.
“Najua hatujaanza na kasi kubwa, lakini matumaini yangu makubwa ni kuona mapambano zaidi katika mechi zijazo na kila mchezaji akitumia nafasi yake kuisaidia timu kufikisha malengo,” alisema Kerr.
Alieleza kuwa mchezaji huyo ambaye amewahi kuichezea DC Motema Pembe ya Congo DRC, atakuwa msaada mkubwa katika kikosi chake.
Kerr aliwataka mashabiki na wadau wa timu hiyo kutarajia mambo makubwa zaidi, huku akiwataka wachezaji kuhakikisha wanapambana kufa au kupona kuwania ubingwa wa ligi.
Mchezaji huyo ambaye ni raia wa Tanzania, alisajiliwa na Simba mwanzoni mwa Ligi Kuu msimu huu, lakini alishindwa kuitumikia timu hiyo kutokana na Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kuchelewa.