25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 29, 2021

Staili ya kuaga mwili wa Moi Kenya yazua mjadala

NAIROBI, KENYA

WAKENYA jana walikusanyika katika majengo ya Bunge kuuaga mwili wa rais mstaafu, Daniel Toroitich arap Moi.

Mwili huo uliwasili katika Bunge kutoka chumba cha kuhifadhi maiti cha Lee Funeral jijini Nairobi mapema jana.

Kama alivyoagwa Rais wa kwanza wa Kenya, mzee Jomo Kenyatta mwaka 1978 ambapo mwili wake uliwekwa juu ya meza pasipo jeneza, ndivyo ulivyoagwa mwili wa Moi jana.

Pamoja na hayo, hatua ya kuweka mwili juu ya meza pasipo jeneza imezua mjadala, huku baadhi wakiona kama hajapewa hifadhi inayostahili.

Wengi kwenye mitandao ya kijamii walikuwa na maswali mengi kuhusu hasa staili ya kuweka mwili huo juu ya meza pasipo jeneza na zaidi iwapo picha za mwili huo kusambazwa kama ni sawasawa.

Neno ‘bad taste’ lilionekana kutawala mijadala ya wengi na wengine wakiona picha hizo hazileti maadili mazuri kwa utamaduni wa kiafrika.

Hatua hiyo ilimlazimisha Mkuu wa Majeshi wa zamani wa Kenya, kufafanua akisema ni utamaduni ambao walirithi kwa wakoloni.

Kuagwa kwa mwili wa Moi kunajiri baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuwasili kutoka nchini Marekani.

Alikuwa ni mtu wa kwanza kuutazama mwili huo akiwa ameongozana na mkewe pamoja na Mkuu wa Majeshi, Meja Jenerali Samuel Mwathethe.

Uhuru alipokewa na Naibu Rais wake William Ruto na mkuu wa majeshi Mwathethe huku usalama ukiimarishwa.

Awali Ruto aliwasili katika majengo ya Bunge saa tatu na dakika 50 akiandamana na maofisa wa Serikali.

Viongozi mbalimbali nao waliuaga mwili wa Moi kabla ya kufuatia msururu mrefu wa Wakenya waliojitokeza kwa shughuli hiyo.

Kabla ya mwili huo kufika bungeni, msafara wa gari lililokuwa likiusafirisha mwili huo kutoka chumba cha Lee ulipitia Barabara ya Alley na kuingia Kenyatta Avenue kabla ya kuingia barabara ya Bunge ambapo gwaride la kijeshi lilipigwa kutoa heshima.

Moi ambaye aliaga dunia siku ya Jumanne akiwa na umri wa miaka 95, atazikwa nyumbani kwake huko Kabarak katika Kaunti ya Nakuru Februari 12 na Wakenya watakuwa na siku tatu za kuuaga mwili wake kutoka jana hadi kesho.

Serikali ilitangaza siku ya Jumanne Februari 11 kuwa siku kuu kwa raia kushiriki katika ibada ya mazishi ya mwili wa kiongozi huyo wa zamani.

Ikulu ya Kenya imemtaja mzee Moi kama kiongozi aliyeendelea kulitumikia taifa hilo na Afrika, hata baada ya kuondoka madarakani kwa kuwafundisha viongozi wa Kenya na nje.

Zaidi walimtaja kama mtu aliyeendelea kushiriki kwenye maendeleo ya miradi mbalimbali na kazi za misaada akiihubiri amani, upendo na umoja barani Afrika na duniani.

Mzee Moi aliiongoza Kenya kuelekea kurudisha mfumo wa vyama vingi na katika vipindi vingine vingi vya changamoto.

Kipindi kimojawapo cha changamoto ni kile kilichofanikisha kumalizika kwa mchakato wa kukabidhi madaraka kwa amani Desemba mwaka 2002.

Wakati huo, mchakato kama huo ulikuwa nadra kufanyika Afrika, na hivyo kuiweka Kenya kuwa mfano barani Afrika na nje ya bara tangu wakati huo.

“Haiba yake inaishi Kenya hata leo. Filosofi ya nyayo kuhusu ‘amani, upendo na umoja’ ilikuwa wimbo wake kipindi chake kama kiongozi wa nchi na Serikali,” Ilieleza taarifa ya Ikulu.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,301FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles