26.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 30, 2021

Mufti awatuliza Waislamu dhidi ya aliyechana Quran

 Na AMINA OMARI 

MUFTI wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir amewataka Waislamu nchini kuwa watulivu wakati vyombo vya sheria vikiendelea kuchukua hatua dhidi ya mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Daniel Elimringi aliyechana Quran.

Akielezea kitendo hicho kilichofanywa na Daniel, Mufti alisema hakihusiani na mitazamo yoyote ya kidini.

Kauli hiyo ya Mufti imekuja baada ya juzi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo  kuagiza kusimamishwa kazi kwa Daniel ambaye alikuwa kitengo cha biashara.

Pamoja na hilo, tayari mtumishi huyo amekwishafikishwa mahakamani na inaelezwa yuko mahabusu baada ya kunyimwa dhamana.

Akitoa tamko kuhusu tukio hilo, Mufti alisema kitendo hicho ni udhalilishaji wa maneno ya Mungu na zaidi kinasababisha maudhi kwa Waislamu na kuleta mfarakano miongoni mwa jamii.

“Niwaombe Waislamu kuendelea kuwa na subira na uvumilivu huku wakisubiri kauli za viongozi wao wa Bakwata ambao wanafuatilia kwa ukaribu kesi iliyoko mahakamani kwa sasa,” alisema Mufti Zubeir.

Alitumia fursa hiyo kuwataka Waislamu nchini kuzingatia mafundisho ya dini yao kudhibiti hasira zao kwa kuwa na subira kwa kuwa watapata thawabu kubwa.

Aliwataka waumini wa dini hiyo kuendeleza umoja na mshikamano miongoni mwao na waumini wa dini nyingine na kuacha kuchukua kitendo hicho kama sehemu ya chokochoko za kidini.

“Niwapongeze Serikali kwa kuchukua hatua za haraka na muhusika kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kwani hatua hiyo inaonyesha namna Serikali yetu ilivyokuwa na msimamo wa kuhakikisha dini haziwi chanzo cha kutugawa,” alisema Mufti Zubeir.

Pia aliiomba Serikali kuendelea kuyadhibiti matukio ya uvunjifu wa amani kwa misingi ya dini ili yasiweze kuleta mianya ya ukosefu wa amani.

Kuhusu kauli mbalimbali zinazoendelea kutolewa katika maeneo mbalimbali nchini, Mufti Zubeir alisema kuwa kauli yake ni ya mwisho, hivyo asingependa kuona tukio hilo linaendelea kuwa mjadala.

“Tuwaachie vyombo vya kimahakama jambo hilo kwa sasa na sisi kama taasisi tutaendelea kufuatilia kesi hiyo ili kuhakikisha haki inatendeka,” aliongeza Mufti.

Kwa upande wake, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa, alisema kuwa utulivu wa waumini wa Kiislamu ni matokeo ya kazi nzuri inayofanywa na mabaraza za amani yaliyoko maeneo mbalimbali nchini.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,509FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles