26.8 C
Dar es Salaam
Saturday, September 7, 2024

Contact us: [email protected]

Spika ang’oa wabunge watano

Kamati-za-Bunge-kizaazaa*Ni Ndassa, Dk. Chegeni, Dk. Mwanjelwa, Lugola na Mlata

*Bashe, Zitto wajiuzulu, wabunge wengine 22 wapanguliwa

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amefanya mabadiliko ya baadhi ya wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge, huku akiwaondoa wenyeviti na makamu wenyeviti watano katika kamati walizokuwa wakiziongoza.

Katika mabadiliko hayo yaliyowagusa jumla ya wabunge 27, Spika Ndugai, ametoa maelekezo ya kujazwa kwa nafasi zilizoachwa wazi za wenyeviti na makamu wenyeviti walioguswa na panga pangua hiyo na kusititiza utekelezaji wa maagizo yake kuanza mara moja.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Ofisi ya Bunge, Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano ya Umma, uamuzi wa  Spika umezingatia mahitaji mapya na changamoto zilizojitokeza baada ya kuundwa kwa Kamati za Bunge hapo Januari mwaka huu.

Taarifa hiyo ilieleza kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa Spika ya kuteua wabunge na kuunda kamati za Bunge, alizingatia kanuni ya 116 (3) ya kanuni za Bunge kuwaondoa viongozi watano wa kamati na kwamba kamati ambazo zitaathirika na uamuzi wake zitapaswa kufanya uchaguzi wa viongozi walioondolewa kwa mujibu wa kanuni ya 116 (10).

Wenyeviti walioguswa la rungu la mabadiliko yaliyofanywa na Spika Ndugai ni Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Mlata (CCM) ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini aliyehamishiwa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira,  Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM), ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji na Mitaji (PIC), aliyehamishiwa kamati ya Katiba na Sheria.

Mwingine ni Mbunge wa Viti Maalumu, Dk. Mary Mwanjelwa (CCM),  ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ambapo amejikuta akihamishiwa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira.

Makamu wenyeviti walioondolewa kwenye kamati zao ni Mbunge wa Busega, Dk. Raphael Chegeni (CCM), ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii pamoja na Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), ambaye aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).

Sambamba na hao, wabunge wengine 22 nao wamehamishwa kutoka kamati walizokuwa kwenda kamati nyingine  na taarifa za Bunge ambazo gazeti hili limezipata zimeeleza kuwa mabadiliko hayo yamelenga kuwaondoa waliokuwa wakilalamikiwa kuhusu mienendo yao ya kikazi kwenye kamati walizokuwa huku wengine wakihamishwa kwa ajili ya kwenda kujenga taswira mpya ya kamati zinazonyooshewa vidole.

Panga pangua hiyo ya Kamati za Bunge iliyofanywa na Spika Ndugai, imekuja siku mbili baada ya gazeti hili kuwa la kwanza kuripoti kuhusu tuhuma za ufisadi dhidi ya baadhi wabunge wakiwemo viongozi wa kamati pamoja na uwezekano wa kuwepo kwa mabadiliko ya wajumbe na viongozi wa kamati hizo yaliyofanyika jana.

Gazeti hili liliripoti kuwa ripoti ya uchunguzi wa mwenendo wa wabunge iliyofikishwa mezani kwa Spika, iliwatuhumu viongozi wa kamati ambao ni Mlata, Ndassa, Dk. Mwanjelwa, Dk. Chegeni na Lugola pamoja na baadhi ya wabunge kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Kutokana na hali hiyo Spika Ndugai, alilazimika kufanya kikao na wabunge hao ambapo pamoja na mambo mengine aliwaeleza jinsi majina yao yanavyohusishwa na tuhuma hizo na kuwataka kuwafikishia ujumbe kwa wajumbe wa kamati zao kwa kuwataka kujisahihisha kutokana na  baadhi ya wajumbe wa kamati hizo kudaiwa kutumia jina la Bunge vibaya.

Aidha, gazeti la MTANZANIA lilikariri taarifa za kibunge zilizoeleza kuwa taasisi zilizofikiwa na wabunge wanaotuhumiwa kuombwa rushwa kuwa ni Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).

Hata hivyo, walipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo, Mlata, Dk. Mwanjelwa na Lugola walikanusha kuhusika nazo huku wakieleza kuwa alichofanya Spika baada ya kuwaita ofisini kwake ni kuwapa maelekezo ya kikazi na kuwatuma kufikisha ujumbe wa kujisahihisha kwa wajumbe wa kamati zao.

Kwa upande wake Dk. Chegeni alisema hafahamu jambo lolote kuhusu kashfa hiyo na kutilia shaka uwezekano wa kuwepo mkakati wa kuichafua kamati yake.

Bashe, Zitto wajiuzulu

Muda mfupi baada ya Ofisi ya Bunge kutoa tangazo la kupanguliwa kwa Kamati za Bunge, wabunge wawili ambao ni wajumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM) na Zitto Kabwe wa Kigoma Mjini (ACT – Wazalendo), walimwandikia barua Spika ya kuomba kuachia ngazi kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zilizoelekezwa kwenye kamati yao.

Katika barua yake ya Machi 22, mwaka huu Bashe alimwandikia Spika akieleza kuwa kuna tuhuma nzito zilizochapishwa katika vyombo vya habari zikieleza kuwepo kwa ufisadi katika kamati za Bunge jambo ambalo linaweza kuharibu sifa ya kamati za Bunge, Bunge na wabunge binafsi hivyo uchunguzi wa kina ufanyike na hatua kali zichukuliwe dhidi ya watakaobanika kuhusika.

“Ninajiuzulu ujumbe wa kamati ninayohudumia sasa ili kupisha uchunguzi. Bunge litaje wahusika hata nikiwa mimi ili kutunza heshima ya kamati na taasisi. Ni vigumu kuhudumia wakati umma unaitizama kamati kama corrupt, ili niweze kutimiza wajibu wangu ni vizuri kujiridhisha, uhusika wa kamati na namna tulivyohusika,” ilisomeka sehemu ya barua hiyo ya kujiuzulu ya Bashe.

Wakati Bashe akiandika hayo, Zitto katika barua yake ya Machi 22, mwaka huu aliyoipa kichwa cha maneno ‘tuhuma za ufisadi dhidi ya Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii,’ aliandika kuwa ameamua kujiuzulu ujumbe wa kamati anayohudumia ili kupisha uchunguzi dhidi ya vitendo vya ufisadi vya baadhi ya wabunge vilivyoripotiwa na gazeti la MTANZANIA.

“Tuhuma hizi ni nzito sana na zinaweza kuharibu kabisa sifa ya Bunge na kamati zake, kwa vyovyote vile tuhuma hizi zimeharibu sifa ya wabunge binafsi. Kwa barua hii naomba Bunge liagize uchunguzi wa kina na kuchukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayekutwa kahusika.

“Kumekuwa na tuhuma za mara kwa mara dhidi ya wabunge nyakati tofauti. Kufanyika uchunguzi na kuchukua hatua ni chanzo cha mwendelezo wa tuhuma za namna hii. Nashauri kuwa safari hii jambo hili lichukuliwe kwa uzito unaostahili,” alisema Zitto katika barua yake kwenda kwa Spika.

Kamati yagomea kazi

Katika mwendelezo huo wa kuachia ngazi, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Dk. Chegeni naye jana aliwasilisha dokezo la kamati yake ofisini kwa Spika lililoeleza kuwa kamati yake iliyokutana jana katika ukumbi wa Saadan uliopo Jengo la LAPF, Kijitonyama baada ya kumaliza majukumu yake ya kibunge ilijadili tuhuma za rushwa ilizoelekezewa.

Dokeza hilo lilieleza kusikitishwa na tuhuma hizo na kwamba wajumbe waliazimia kulitaka Bunge kufanya uchunguzi wa tuhuma hizo na kwamba kuanzia leo, wanasitisha kufanya kazi yoyote ya kamati hadi uchunguzi utakapokamilika.

Kwa upande mwingine katika mitandao mbalimbali ya kijamii, mijadala mikali kuhusu mienendo isiyoridhisha ya baadhi ya wabunge ilitawala.

Mjadala mzito

Mmoja wa wachangiaji katika mitandao hiyo aliandika kuwa taarifa za baadhi ya wabunge kujihusisha na vitendo vya rushwa ni za muda mrefu na kukumbushia kashfa ya aina hiyo iliyoibuliwa bungeni Juni 13, 2012 ikiwahusisha baadhi ya wabunge wa Bunge la 10 kushiriki vitendo hivyo wakiwa katika shughuli za kamati huko Handeni mkoani Tanga.

Katika andishi lake hilo alieleza mwendelezo wa kashfa za rushwa dhidi ya wabunge, wapo waliopata kukamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na kufikishwa mahakamini lakini hadi sasa bado ni wabunge.

Mchangiaji huyo anaandika kushangaa jinsi Bunge linavyoshindwa kufuata mila, desturi na utamaduni wa mabunge ya Jumuiya ya Madola ambayo wabunge wake waliopata kukumbwa na kashfa za rushwa walivuliwa nyadhfa zao na kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zao.

“Kuna haja ya tatizo hili kulibeba serious kwa sababu kwa mujibu wa kanuni za Bunge, Spika anafanya maamuzi kwa mujibu wa katiba, sheria, kanuni, maamuzi ya maspika waliopita na uzoefu wa mabunge ya Jumuiya ya Madola.

“Kwa uzoefu huo, mwaka 2005 India ilifukuza wabunge 11 kwa tuhuma za rushwa na kuacha mahakama iendelee nao na kuanzia mwaka 1624 hadi sasa Uingereza imekwishafukuza wabunge wengi sana,” aliandika mchangiaji huyo.

Taarifa za TAKUKURU

Hata hivyo jana Taasisi za Kuzuia na Kupamba na Rushwa nchini (Takukuru), ilimuhoji mmoja wa wenyeviti wa kamati kutokana na kuhusishwa na tuhuma za rushwa.

Kutokana na hali hiyo MTANZANIA ilipomuuliza Mkurugenzi wa TAKUKURU, Kamishna Valentino Mlowola, kuhusu taarifa hizo, alisema kwamba hawezi kuzungumzia suala hilo na kutaka atumiwe maswali ambayo angeyajibu kwa ufasaha.

“Swali hilo ninaomba niandikie maswali nitayajibu kwa ufasaha na kwa wakati,” alisema Kamishna Mlowola.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles