22.7 C
Dar es Salaam
Saturday, July 13, 2024

Contact us: [email protected]

Ukawa kinara umeya Dar

Pg 1Patricia Kimelemeta na Veronica Romwald, Dar es Salaam

HATIMAYE kitendawili  cha kumpata Meya wa Jiji la Dar es Salaam kiliteguliwa jana, baada ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kushinda nafasi hiyo dhidi ya hasimu wao kisiasa, Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ukawa wameshinda nafasi hiyo kupitia kwa mgombea wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na  Diwani wa Kata ya Vijibweni, Isaya Mwita.

Kuchaguliwa kwa meya wa upinzani  kumeandika historia ya upinzani kuongoza jiji hilo tangu  Tanganyika (Tanzania) ilipopata uhuru  Desemba 9,1961.

Kabla ya kufanyika uchaguzi huo jana, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Theresia Mmbando aliwahakikishia wajumbe kuwa uchaguzi  utakuwa huru na haki, huku akiwasihi kuwa watulivu ili kuepusha vurugu kama zilizotokea awali.

Baada ya kauli hiyo, wajumbe wote walikubaliana kwa kauli moja kupiga kura ya siri, lakini masanduku ya kura yote lazima yawe wazi ili kila mmoja aweze kutumbukiza karatasi, huku wananchi wakishuhudia.

Msimamizi wa uchaguzi huo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Sara Yohana alilazimika kutoa maelekezo ya upigaji kura.

Ilipofika saa 5:20,Sara  alianza kutoa maelezo na kutaja idadi ya wajumbe halali wa uchaguzi huo.

Alisema jumla ya wapiga kura ni 163, Kinondoni ikiwa na wajumbe 54,badala ya 58 kwa sababu wajumbe wanne hawakufika.

Kwa upande wa Ilala,wajumbe walikuwa 53 badala ya 56 ambapo wajumbe watatu hawakufika, huku Temeke ikiwa na  wajumbe 48 kati ya 49 ambapo mmoja hakuwapo. Wakati kura zinapigwa wajumbe wanane hawakuwemo ukumbini.

Saa 5:30, upigaji kura ulianza kwa mkurugenzi kuita jina moja moja mpaka walipomalizika.

Ukawa watumia kalamu zao

Licha ya wajumbe kutangaziwa kuwa wameandaliwa kalamu za kupigia kura,  wajumbe wa Ukawa waliamua kutumia kalamu zao maalumu, huku wenzao wa CCM wakitumia kalumu iliyokuwa imeandaliwa.

MATOKEO KUTANGAZWA

Matokeo yalianza kutangazwa saa 6:30 mchana ambapo msimamizi wa uchaguzi, huo Sara  alisema  kura halali zilikuwa 151 na zilizoharibika ni 7.

Alimtangaza mgombea wa Chadema, Isaya Mwita kuwa mshindi baada ya kupata kura 84 na mpinzani wake kutoka CCM, Yusuph Yenga akipata kura 67.

HALI ILIVYOKUWA

Wafuasi wa Chadema walijitokeza tangu saa moja asubuhi katika viwanja vya Karimjee, ingawa walilazimika kuishia nje ya geti kwa sababu walioruhusiwa kuingia ni wale waliokuwa na mwaliko maalum. Hata hivyo walivumilia na kusubiri matokeo.

Saa 2:00 asubuhi, viongozi na madiwani kadhaa CCM na Ukawa walianza kuwasili.

Askari polisi waliovalia sare na wengine kiraia, waliendelea na kazi zao za kuhakikisha eneo lote linakuwa salama.

Saa 4:30, wabunge waliwasili akiwamo, John Mnyika (Kibamba), Saed Kubenea (Ubungo) na Halima Mdee (Kawe).

KATIBU TAWALA  AITWA ‘JECHA’   

Saa 3:35 Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Mmbando aliwasili  eneo hilo na aliposhuka kwenye gari, wafuasi wa Ukawa walianza kumzomea kwa kumwita ‘Jecha’ ‘Jecha’.

Jecha ni Mwenyeiti wa Tume ya Taifa Uchaguzi Zanzibar (ZEC), ambaye amekuwa maarufu baada ya kufuta Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana na kutangaza uchaguzi wa marudio Machi 20, mwaka huu ambapo mgombea urais wa CCM, Dk. Ali Mohamed Shein aliibuka mshindi kwa kupata asilimia 91.

LOWASSA AWASILI

Saa 10:10 aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa aliwasili katika eneo hilo, akiwa kwenye gari lenye namba T 771 DEA.

Wafuasi wa chama hicho walipomwona walilisogelea  gari hilo, huku wakiimba kwa furaha wakisema ‘Rais… rais… rais’ huku wengine wakiimba ‘kama sio juhudi zako Lowassa na umeya tungepata wapi, huku wengine wakipiga vigelegele.

Tofauti na mengine, gari la Lowassa liliruhusiwa kuingia ndani na moja kwa moja kiongozi huyo aliingia ukumbini kushuhudia mchakato wa uchaguzi.

Dakika chache baadaye, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe naye aliwasili eneo hilo.

CCM WAITWA ‘JIPU’

Baada ya kumaliza kupiga kura, baadhi ya viongozi wa CCM walianza kuondoka mmoja baada ya mwingine dakika chache kabla ya kutangazwa mshindi.

Viongozi hao, ni pamoja na Naibu Spika wa Bunge, Dk.Tulia Akson na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa wakifuatiwa na mgombea wa umeya kupitia CCM, Yenga.

Hata hivyo, viongozi hao walionja joto la wafuasi wa upinzani ambao waliwaita ‘majipu’

Dakika chache baadaye wafuasi hao  walitangaziwa kuwa Ukawa walikuwa tayari wameshinda ambapo walianza kupiga ngoma ya mdundiko, huku wakiwa wamenyanyua juu mabango yenye ujumbe mbalimbali.

Moja ya mabango hayo lilisomeka “mmebana, mmeachia, Isaya ndio habari ya mjini, Vijibweni, Kigamboni tuna imani naye. Lingine lilisomeka, Isaya ndiye Rais wa jiji la Dar es Salaam… magamba hamna chenu”.

Saa 7:47 mchana, msafara wa magari kuelekea makao makuu ya Chadema, Kinondoni ulianza, huku baadhi ya wanachama wakitembea kwa miguu wakishangilia.

Kwa mara ya kwanza,meya mteule alikuwa tayari ameandaliwa gari aina ya Nissan Patrol lenye namba za usajili SM 10401 na kuondoka kwenye viwanja hivyo kuelekea makao makuu ya chama hicho.

MEYA ANENA

Akizungumza baada ya kutangazwa kuwa mshindi, Mwita aliwashukuru wajumbe waliompigia kura na kudai kuwa, atakuwa kiongozi wa wote bila ya kujali itikadi za vyama.

“Nafasi niliyoipata ni kubwa, ninaamini nitafanya vizuri kwa sababu nitashirikiana na viongozi wote bila ya kujali itikadi ya vyama ili kuhakikisha naleta maendeleo kwa wananchi,”alisema Mwita.

MBOWE

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisifu uchaguzi huo kuwa ulikuwa huru na haki na hakukuwapo na migongano iliyokuwa inajitokeza kipindi kilichopita.

“CCM walifanya vurugu ili kuhakikisha halmashauri hiyo haiendi Ukawa, mwisho wa siku wameshindwa, tutaendelea na mkakati wetu wa kuleta mabadiliko kwa wananchi ili kuhakikisha wanapata maendeleo,”alisema Mbowe.

Jiji la Dar es Salaam linaundwa na manispaa tatu, ambapo manispaa mbili zinaongozwa na Ukawa na moja inaongozwa na CCM.

Manispaa zinazoongozwa na Ukawa ni Kinondoni na Ilala, wakati CCM inaongoza Manispaa ya Temeke.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles