25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

SOKA LA TANZANIA NI KIVUTIO KINGINE CHA UTALII

Na ZAINAB IDDY

WAKATI tukiamini mbuga za wanyama, milima na makumbusho ya Taifa ndivyo vivutio vikuu Tanzania,ukweli ni kuwa si vibaya tukaingiza na soka  ambalo kila kukicha limekuwa na masuala mapya yanayodidimiza mchezo huo.

Hii inatokana na kila kukicha kwenye soka kuzaliwa mambo yasio na tija, huku lengo likiwa ni kuwanufaisha wachache tu.

Kama unakumbuka hivi karibuni kulitokea utata katika suala la kadi tatu za njano za beki wa Kagera Sugar, Mohamed Fakhi ambazo awali Simba walishinda rufaa na kupewa pointi zao, lakini baadaye Kagera waliomba suala hilo kupitiwa upya ndipo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) walipolipeleka Kamati ya Katiba,Sheria na Hadhi za Wachezaji  iliyoamua kuzirudisha pointi hizo kwa Kagera,  japo  walikiri Fakhi anakadi tatu za njano.

Ukiachana na hilo limekuja suala la wapi panastahili kufanyika fainali za Kombe la FA, linaloandaliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kati ya Mbao FC dhidi ya Simba, jibu la kwanza lilitolewa na Rais wa Shirikisho hilo Jamal Malinzi kuwa itachezeshwa droo kabla ya kuja kuamua mechi itachezwa Jamhuri mkoani Dodoma Mei 28 mwaka huu.

Hivi kwa wanaofuatilia masuala ya soka ulimwenguni, kuna ambaye hajui fainali za kombe la dunia zinafanyika wapi, fainali za Uefa zinafanyika wapi au lile kombe la FA pale England fainali zake zitafanyika wapi? iweje fainali za FA za Tanzania hazikujulikana mapema kabla  ya  kuchezwa mechi za nusu fainali

Napata shaka uwezo wa viongozi wetu waliokuwepo ndani ya TFF  katika masuala ya soka,  kwani iweje hadi nusu fainali ya kwanza kati ya Simba na Azam kisha ile ya Mbao na Yanga, haujajulikana uwanja upi utachezwa fainali za mashindano hayo, mbona mwaka jana hakukuwa na suala la kutafuta uwanja?

Ukiachana na mambo ya FA, lipo lile la mchezaji wa African Lyons, Venance Ludovick kuachiwa kutoka kifungoni.

Sio vibaya mchezaji huyo kuw huru, lakini ni muda gani umepita tangu Yanga walipokata rufaa ya kupinga kucheza kwake kwa madai usajili wake haukukamilika , jibu ni zaidi ya miezi mitatu sasa.

Wahusika ndani ya TFF, walishajiuliza mchezaji huyo katika miezi hiyo yote alikuwa anafanya nini kulinda kipaji chake au kwa kuwa hachezi timu zenye maslahi na shirikisho Simba au Yanga.

Ni zaidi ya michezo 15 ya Ligi Kuu amekosa kucheza, je kifungu gani kilitumika kumruhusu hivi sasa ambacho hakikutumika kumuweka huru, mara baada ya kukatiwa rufaa au kamati  ilamua tu kumpotezea muda,  majibu sahihi yatatoka ndani ya TFF.

Tukirudi nyuma kidogo mechi ya mwisho ya Ligi Kuu msimu uliopita kati ya Ndanda FC na Yanga, ilichezwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, badala ya ule wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara sababu kubwa ilielezwa Wanajangwani waliongea na Ndanda kutaka wabadili uwanja.

Suala hili lilizaa mambo mengi  ikiwemo madai ya kuibeba Yanga , kwani Azam waliomba mechi zao  Simba na Yanga kuchezwa kwenye dimba lao la Chamanzi walikataliwa, hili ndio soka la Tanzania na ndio maana tunasema kivutio kipya kwa wageni wetu.

Ifike wakati basi Wizara ya Maliasi na Utalii chini ya Waziri Jumanne Maghembe,  wafahamishwe kuwa kuna kivutio kipya kwenye idara yake ambacho sina shaka itaweza kuingiza kipato kikubwa kutokana na figisu figisu zilizomo ndani yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles