24.4 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

SIMBA WANATIA HURUMA, KISA…

Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM

KWA hali iliyofikia klabu ya soka ya Simba inaonekana wazi kuwa wako tayari kufanya lolote, ilimradi wapate kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao, baada ya kusubiri kwa takribani misimu minne bila mafanikio.

Kilio  kikubwa kwa klabu hiyo ni kufuta kabisa hali ya kusakamwana na wapinzani wao wakubwa Yanga kuwa ni ‘wamatopeni’.

Kwa sababu hiyo, Kombe la Shirikisho,Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania unaotarajiwa kufanyika Septemba mwaka huu vimekuwa ni vichaka vya  klabu hiyo kutumia ili kufikia lengo lao hilo msimu ujao.

Tayari klabu hiyo imeenda mbali hadi kuingilia maamuzi ya Kamati halali za TFF zinapofanya uamuzi wake ilimladi tu kufanya ushawishi kwa wao kuonekana wanaonewa na kunyimwa haki zao wakati si kweli.

Kuna wakati Ofisa Habari wa klabu ya Simba, Haji Manara alilazimika kutokwa na povu wakati alipokuwa akijaribu kutuaminisha kwa kulishambulia shirikisho na baadae kusababisha  kufungiwa kujihusisha na soka pamoja na kutozwa faini ya milioni tisa kutokana na kitendo hiko.

Simba baada ya misimu minne kukosa ubingwa,  wamekosa uvumilivu na subira ya mchezo wa soka kwa  kuihusisha TFF na mipango ya kupanga klabu ipi ya kuwa Bingwa wa Ligi Kuu Tanzania wakati Ulaya na kwingineko duniani zipo klabu ambazo zimefikisha zaidi ya miaka 20 hazijachukua ubingwa wowote wa Ligi Kuu  licha ya ukongwe wao katika mchezo wa soka.

Soka si sawa na michezo mingine, soka linautaratibu wake wa kuwa bingwa wa msimu yaani unaweza kuwa bingwa kwa ziada ya pointi au utofauti wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Kinachoonekana sasa Simba kama wanachanganya siasa za vyama na mchezo wa soka ambao una tofauti kubwa ikizingatiwa ili kumpata mshindi ni lazima dakika 90 za mchezo zitumike kuamua ndani ya uwanja zaidi ya hapo ni bahati tu.

Ni jambo linalotia huruma sana kwa Simba kuendelea  kuishawishi TFF ili kuhakikisha timu hiyo inashiriki Kimataifa au uongozi uliopo sasa wa shirikisho hilo unaondoka madarakani kwenye uchaguzi ujao eti kwa gizo cha kulipwa fadhila kwa kuwa klabu hiyo ndio iliyowaweka madaraka.

Dhana hiyo ndio inayotafsiri mpango mkubwa wa Simba kuwa ni kucheza na akili ya Rais wa  TFF, Jamali Malinzi kwa kumtisha kumng’oa madarakani ili awape nafasi ya kucheza Kimataifa.

Imefikia hatua kwamba uongozi wa klabu hiyo kwa sasa kwenye vikao vyao wameacha agenda ya maendeleo ya klabu kwa kuzungumzia namna ya kutafuta ushindi ndani ya uwanja badala yake wanajadili zaidi suala la uchaguzi ujao na kumtisha Malinzi endapo atashindwa kuwapa nafasi ya kucheza Kimataifa nje ya uwanja.

Hata hili suala la kutangaza kufikisha  malalamiko yao Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) ya Shirikisho la Soka Kimataifa (FIFA) likiwamo la mchezaji wao aliyemaliza muda wake wa mkopo katika timu ya Kagera Sugar, Mbaraka Yusuphu, ni kumtia presha tu Malinzi na Kamati zake ili ipate kimuhemuhe na kufanya maamuzi ambayo si ya haki.

Ikumbukwe kuwa hivi karibuni Simba itakuwa na mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Mbao FC katika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma hivyo kwa hila hizi, TFF wakibabaika tu na kelele za Simba huenda Mbao wakakutwa na wasiyoyadhania ndani ya uwanja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles