23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

SINGIDA YAIGOMEA SIMBA, ZATINGA ROBO FAINALI

Na THERESIA GASPER,DAR ES SALAAM


SIMBA imelazimishwa bao 1-1 na Singida United katika mchezo wa mwisho wa kundi C wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati ‘Kombe la Kagame’, uliochezwa jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Bao la Simba lilifungwa  dakika ya 15 na Meddie Kagere, wakati Danny Lyanga aliisawazishia Singida United dakika ya 35.

Matokeo hayo yanaifanya Simba na Singida United kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

Simba imemaliza michezo yake ikiwa kinara wa kundi C baada ya kufikisha pointi saba, sawa na Singida iliyomaliza katika nafasi ya pili, lakini zikitofautiana wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Simba ilizindua kampeni zake kwa kuichapa Dakadaha ya Somalia mabao 4-0 kabla ya kuitungua APR ya Rwanda mabao 2-1.

Singida kwa upande wake, iliibamiza APR mabao 2-1 kabla ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Dakadaha.

APR inakamata nafasi ya tatu ikiwa na pointi tatu baada ya jana kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Dakadaha iliyomaliza michezo yake ikiwa mkiani, huku ikiwa  haina pointi.

Simba ilikuwa ya kwanza kulifikia lango la Singida United  dakika ya pili, lakini mkwaju wa Nicholaus Gyan ulipanguliwa na kipa wa Singida United, Manyika Peter.

Dakika ya 11, Dany Lyanga alipoteza nafasi ya kuiandikia bao Singida United,  baada ya mkwaju wake kupaa juu ya lango la Simba, akiunganisha  pande la Boniface Maganga.

Dakika ya 15, Meddie Kagere aliiandikia Simba bao la kuongoza baada ya kuunganisha krosi ya Jamali Mwambeleko.

Dakika ya 35, Lyanga aliisawazishia  Singida United kwa kufunga bao la staili ya ‘tiki-taka’, baada ya kutokea piga nikupige kwenye lango la Simba.

Dakika ya 59, Kocha wa Singida alifanya mabadiliko, alimtoa Eliuter Mpepo na kumwingiza Benedict Aymerick kabla ya dakika ya 69 kufanya mabadiliko mengine, alitoka Tibar John na kuingia Amara Diaby.

Dakika ya 85, Simba ilifanya mabadiliko, alitoka Jamal Mwambeleko na kuingia Mohamed Hussen, huku Singida  akitoka Kenny Ally na kuingia Nizar Halfan.

Pamoja na mabadiliko yaliyofanywa na kila upande, dakika 90 za pambano hilo zilimalizika kwa sare ya bao 1-1.

Simba: Deogratus Munishi, Nicholaus Gyan, Jamali Mwambeleko, James Kotei, Pascal Wawa, Mzamiru Yassin, Said Ndemla, Mwinyi Kazimato, Meddie Kagere, Mosses Kitandu na Mohamed Rashid

Singida United: Manyika Peter, Boniface Maganga, Salum Chuku, Kennedy Juma, Salum Kipaga, Yussuph Kagoma, Kenny Ally, Dany Lyanga, Eliuter Mpepo, Habib Kiyombo na Tibar John.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles