30 C
Dar es Salaam
Monday, September 27, 2021

Simba, Yanga zasubiri barua

Na WINFRIDA MTOI, DAR ES SALAAM

KLABU za Simba na Yanga, zinasubiri barua rasmi kujua siku gani Ligi Kuu Tanzania Bara itarejea ili kuanza mipango ya kuwarejesha wachezaji wao kambini.

Hali hiyo inatokana na kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli juzi aliposema anafikiria kuruhusu ligi nchini ziendelee.

Kauli hiyo iliifanya Kamati ya Bodi ya Ligi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kukutana na kujadili hatma ya ligi na kuadhimia kuirejesha, lakini mechi zikichezwa bila mashabiki.

Kutokana na maadhimio hayo, MTANZANIA lilitaka kujua msimamo wa timu za Simba na Yanga ambazo ndizo zenye mashabiki wengi, lakini viongozi wake walishindwa kutolea ufafanuzi kwa madai ya kusubiri taarifa rasmi.

Akizungumzia suala hilo, Meneja wa timu ya Simba, Patrick Rweyemamu, alisema hajasikia kauli rasmi kutoka Bodi ya Ligi, hivyo kama benchi la ufundi wanasubiri uamuzi kutoka uongozi wa juu klabu hiyo pale utakapopokea barua.

Alisema endapo barua itafika ya kuwaeleza ni lini mechi za ligi hiyo zitaanza kuchezwa, anaamini watakutana na kuweka mikakati ya maandalizi.

“Kauli tuliyosikia ni ile ya Rais Magufuli, kuwa anafikiria kuruhusu ligi iendelee, lakini hiyo ya Bodi Ligi kutoa tamko rasmi kusema ligi inarudi sijazipata, mimi sipo ofisini muda huu najua kama wametangaza lazima barua tutaipata na viongozi wetu wa juu watapanga nini tufanye,” alisema.

Kwa upande wa Yanga, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Hassan Bumbuli, alisema wanasubiri batua kutoka TFF, ndipo waeleze mikakati yao.

Alisema mambo yote ya kocha na utaratibu wa wachezaji kurudi kambini, yatajadiliwa na uongozi baada ya kupata barua rasmi kuwa ligi inarejea, lakini kwa sasa hawawezi kuzungumza chochote.

“Subiri tupate barua rasmi, mipango yote tutaweka wazi kuwa wachezaji watarejea lini na program nyingine za mechi,” alisema.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,348FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles