Na Winfrida Mtoi, Dar es Salaam
Timu ya Simba imeendelea kugawa dozi baada ya leo kushinda mechi yake ya kwanza ya Kombe la Mapinduzi kwa kuichapa Chipukizi mabao 3-1.

Katika mchezo huo uliopigwa katika Uwanja wa Amaan, Zanzibar, Chipukizi ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 36 kupitia Fakhi Mwalimu kabla ya Meddie Kagere kuisawazishia dakika ya 45.
Kipindi cha pili Simba ilirejea na kasi ambapo Miraji Athumani aliyeibuka mchezaji bora wa mechi baada ya kufunga mabao mawili yaliyokamilisha ushindi huo.
Wanamsimbazi hao ambao wamekwenda Zanzibar wakiwa na mzuka wa kupata ushindi mnono katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuifunga FC Platnum ya Zimbabwe mabao 4-0 na kutinga hatua ya makundi, kesho watashuka dimbani tena kuikabili Mtibwa Sugar.