25.2 C
Dar es Salaam
Monday, August 15, 2022

Simba SC, TP Mazembe ni vita ya washambuliaji

BADI MCHOMOLO, DAR ES SALAAM

MCHEZO wa kwanza wa hatua ya robo fainali wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Simba SC na TP Mazembe kutoka DR Congo, unatarajiwa kupigwa leo kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Hii ni hatua ngumu zaidi kuliko zile zilizopita, hivyo kila timu inajua hilo na ndiyo maana maandalizi yake yanakuwa tofauti kidogo.

Hatua zilizopita kitu kikubwa ambacho kilikuwa kinaangaliwa ni idadi ya pointi ili kuweza kuingia hatua inayofuata, lakini hatua hii mbali na idadi ya pointi, lakini kikubwa ambacho kinaangaliwa ni idadi ya mabao baada ya kukutana.

Hapa timu zinakutana mara mbili, mchezo wa nyumbani na ugenini, hivyo akiba ya mabao ina maana kubwa sana kuweza kufanikisha timu kuingia hatua ya nusu fainali.

Simba SC inaanzia nyumbani, hivyo lazima ihakikishe inatumia nafasi hiyo ya nyumbani, hasa kunufaika na nguvu watakayopewa kutoka kwa mashabiki. Lakini kuelekea mchezo huo, nini Simba SC wanatakiwa kukifanya ili waweze kuibuka na ushindi.

Safu ya ulinzi

Kocha wa Simba, Patrick Aussems, lazima ahakikishe safu yake ya ulinzi inakuwa makini zaidi, ikiwezekana iwe tofauti kabisa na ilivyokuwa katika michezo ya awali dhidi ya Nkana FC, JS Saoura, Al Ahly na AS Vita.

Pamoja na Simba kufanikisha kufika katika hatua hiyo ya robo fainali, lakini safu ya ulinzi ilikuwa na mapungufu madogo madogo ambayo yangeweza kuwafanya wasifike hapo endapo wangekutana na washambuliaji makini.

Kwa hatua hii, lazima beki wa kati, Pascal Wawa awe na maelewano mazuri na Erasto Nyoni au Jjuuko Murshid, pamoja na mabeki wengine, kuhakikisha wanakuwa makini kuanzia pembeni na katikati.

Endapo watakuwa na umoja katika idara hiyo, kuna uwezekano mkubwa wa kuwazuia wapinzani hao katika Uwanja wa Taifa wasiwe na madhara yoyote na waondoke bila bao.

Kikubwa wasiwaruhusu wapinzani hao kumiliki mipira katika eneo la hatari, kwa kuwa wakifika katika eneo hilo wanakuwa hatari na wanaweza kufanya lolote.

Washambuliaji

Hakuna shaka na ubora wa safu ya ushambuliaji ya Simba SC ambayo inaundwa na John Bocco, Medie Kagere na Emmanuel Okwi.

Hao kila mmoja anatakiwa kuwa na deni la kuhakikisha anaondoka na bao, kwa kuwa mchezo huo unahitaji idadi ya mabao ili kuwa akiba katika mchezo wa marudiano.

Kila mshambuliaji anatakiwa kutafuta bao zaidi ya moja na anatakiwa kuwa kwenye ubora wake zaidi ya vile ambavyo mashabiki wamekuwa wakiwazoea kuwaona.

Lango la TP Mazembe muda wote linatakiwa kuandamwa na washambuliaji wenye kiu ya mabao, kwa kufanya hivyo, kuna uwezekano mkubwa wa kuondoka na idadi ya mabao kuanzia matatu.

Mbali na washambuliaji kuwa kwenye jukumu hilo, lakini kila mchezaji anatakiwa kucheza katika kilele cha ubora wake na ikiwezekana kila mmoja amalize uwezo wake ili kuhakikisha mabao yanakuwa mengi.

Washambuliaji wa TP Mazembe ambao wanatakiwa kuchungwa na walinzi wa Simba SC ni pamoja na Ben Malango, Robert Mbelu, Jackson Muleka, Chiko Ushindi, Deo Kanda na Tresor Mputu.

Inategemea na wachezaji gani wataanza katika kikosi chao cha ushambuliaji, lakini nyota hao wamekuwa wakiunda safu yao ya ushambuliaji.

Mputu ni mmoja kati ya wachezaji wakongwe katika kikosi hicho, amekuwa na uwezo mkubwa wa kuisaidia timu hiyo kufanya vizuri, hivyo anatakiwa kuchungwa kwa kiasi kikubwa.

Katika hatua ya makundi kwenye michuano hiyo, TP Mazembe walionekana kuwa bora, hasa katika ufungaji, waliweza kuibuka na ushindi wa mabao 8-0 dhidi ya Club Africain.

Ubora na uzoefu wa Mazembe kwenye michuano hiyo usiwape wasiwasi Simba SC kuelekea mchezo huo wa leo, kikubwa ni kutumia vizuri uwanja wa nyumbani.

Viungo

Ili timu ya Simba SC iweze kutawala katika eneo la hatari la TP Mazembe, lazima kuwepo na viungo bora ambao watakuwa na uwezo wa kuunganisha safu ya ulinzi na ushambuliaji.

Hivyo, viungo hao lazima wawe na ubunifu wa hali ya juu, hasa kwa kuwachezesha washambuliaji wao, Okwi, Bocco na Kagere.

Hakuna wasiwasi mkubwa na viungo wa Simba SC, Clatous Chama, Jonas Mkude, James Kotei, Haruna Niyonzima, Hassan Dilunga na Mzamiru Yasin, inategemea nani wataanza.

Hawa ni viungo ambao wanaweza kulikamata dimba na kuwafanya wapinzani wasitambe na wasiwasogelee walinzi wao.

Kikosi cha TP Mazembe kina wachezaji wanne ambao ni raia wa nchini Zambia, hivyo Chama anaweza kuwa na msaada mkubwa wa kuwasaidia Simba SC kuweza kuwakamata wapinzani.

Zambia ni moja kati ya nchi barani Afrika ambazo zinatoa wachezaji wengi ambao wana uwezo wa kucheza nafasi ya kiungo pamoja na ulinzi, hivyo TP Mazembe ina wachezaji watatu ambao wanacheza nafasi ya kiungo, Nathan Sinkala, Lamisha Musonda na Rainford Kalaba.

Wachezaji hao wanajuana vizuri na Chama, hivyo inaweza kuwa faida kwa Simba kupenyezewa taarifa kutoka kwa kiungo wao huyo ambaye amekuwa kwenye ubora wa hali ya juu, hasa katika michuano hiyo.

Kwa upande mwingine, Simba wanatakiwa kusahau rekodi za TP Mazembe pale walipokutana mwaka 2011 kwenye michuano hii.

Katika mchezo wao wa awali, Simba walikuwa kwenye uwanja wa nyumbani, lakini walikubali kichapo cha mabao 3-2, huku mchezo wa marudiano kule nchini DR Congo, Simba ikipokea kichapo kingine cha mabao 3-1.

Rekodi haina ulazima kwenye soka, kikubwa ni ubora wa timu kwa kipindi hicho. Wakati Simba inapoteza michezo hiyo miwili mwaka 2011, mchezaji wa pekee wa Simba ambaye amebaki ni Okwi, hivyo TP Mazembe inakutana na Simba mpya, Simba nyingine na si ile ya mwaka 2011, lakini pia Mazembe hawa si wale ambao walishinda michezo yote miwili.

Mashabiki

Huu ni mchezo ambao utakuwa na ushindani katika safu ya ushambuliaji, hivyo mashabiki wa Simba wanatakiwa kujitokeza kwa wingi kama ilivyo katika mchezo dhidi ya AS Vita, Nkana FC, Al Ahly na JS Saoura.

Wingi wa mashabiki unachangia kwa kiasi kikubwa kuwapa nguvu wachezaji wote, hivyo mashabiki wa Simba watawameza wale wa TP Mazembe kwa kuwasapoti wachezaji wao. Kila la heri Simba SC.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,763FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles