30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Samia ataka fikra za Karume zienziwe

KHAMIS SHARIF-ZANZIBAR                                                                            

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amewataka Wazanzibari kuenzi kwa vitendo fikra za maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa za muasisi wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, ili ziweze kuwa endelevu.

Kuhusu fikra za maendeleo katika uchumi, alisema wananchi wanapaswa kuzidumisha ili kuhakikisha rasilimali za nchi zinalindwa kwa manufaa ya jamii na taifa.

Samia alitoa kauli hiyo wakati akifungua kongamano la pili la kumbukumbu ya Rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, lililofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere  Bububu nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Alisema fikra za Hayati Karume zilikuwa zina lengo la kuondoa dhuluma na kuleta usawa kwa wananchi wa Zanzibar na Watanzania hatua ambayo inapaswa kuungwa mkono kwa kila Mzanzibari.

Akizungumzia kuhusu fikra za kijamii, alisema inapaswa kuendelezwa kwa kutoa huduma bure katika sekta ya elimu kama alivyotangaza katika kipindi cha mwaka 1964 ambapo pia alifanya katika eneo la huduma za afya.

“Rais Karume pia aliamini katika misimamo ya fikra za kuwaunganisha Wazanzibari katika nyanja ya kisiasa ambapo baada ya mapinduzi kufaulu aliondoa mfumo wa vyama vya siasa na kuanzisha mfumo wa chama kimoja kwa lengo la kuondoa hali ya kibaguzi kati yetu,” alisema.

Katika hatua nyingine, Samia, alisema Rais Karume alikuwa na fikra za kuleta umoja, utu na heshima kwa Wazanzibari na alikuwa kiongozi ambaye anakemea vitendo vya dhuluma ambapo alihakikisha kila mwananchi anapata haki sawa na mwingine.

“Rais Karume alihimiza umoja na muungano wetu hivyo tunatakiwa tuuenzi kwa vitendo kwa kuimarisha muungano ulioko lakini pia alikuwa hana maamuzi ya peke yake bali yeye alikuwa anashauriana na Baraza la Mapinduzi na Baraza la wazee la ASP na inavyosemekana alikuwa anakutana nao mara kwa mara ofisi ya chama Kisiwandui,” alisema.

Aidha, Samia aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), inayoongozwa na Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, kwa kuendeleza kwa vitendo fikra hizo ikiwemo utoaji wa huduma za elimu na afya bure.

Mapema akimkaribisha Makamu wa Rais Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Steven Wasira, alisema lengo la kongamano hilo ni kuenzi fikra na falsafa ya kiongozi huyo wa kwanza wa Zanzibar.

“Kongamano hilo ni la makusudi kumuenzi na kumtukuza kwa kile alichokifanya kwa kupigania na kuleta maendeleo ya Zanzibar kwa ujumla,” alisema Wasira.

Akizungumza katika kongamano hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Ayoub Mohammed Mahmoud, alisema fikra za Hayati Rais Karume bado zinapaswa kuenziwa na kuheshimiwa kutokana na msingi wa kuheshimu utu na uhuru wa kila Mzanzibari.

Aliongeza kuwa hayati Karume alikuwa na dhamira ya kuendeleza maendeleo ya Zanzibar ambapo katika kipindi cha mwaka 1970 hadi 1975, aliweza kujenga majengo 72 ya ghorofa kwa kipindi cha miaka mitano tu na kwamba hali hiyo ni ishara ya fikra za maendeleo katika nyanja ya kijamii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles