30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Siku ya Wanawake: Samia ameonesha dhamira kuongeza usawa wa kijinsia

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Lengo namba tano la Maendeleo Endelevu (SDG’s) linahimiza juu ya kuwepo kwa usawa wa kijinsia ili kuhakikisha jamii inashiriki kikamilifu kwenye maendeleo ya taifa.

Tanzania kama zilivyo nchi nyingine imeendelea na jitihada za kuhakikisha usawa wa kijinsia unakuwepo katika nyanja mbalimbali.

Machi 8 kila mwaka Dunia huadhimisha Siku ya Wanawake ambayo hutumika kutafakari mafanikio yaliyopatikana, changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake na namna ya kujikwamua.

Makala haya yanaangazia mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan katika kuongeza usawa wa kijinsia.

Rais Samia amekuwa akiwatambua na kuwajali wanawake kwa kuhakikisha changamoto zao zinatatuliwa.

Jitihada ambazo Serikali imefanya katika kuongeza usawa wa kijinsia ni kuunda wizara mahususi ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu inayoweka kipaumbele eneo la usawa wa kijinsia.

Kuteuliwa kwa Kamati ya Taifa ya Ushauri yenye wajumbe 25 na Rais Samia wakijumuishwa wataalam wa sekta mbalimbali kutoka Tanzania Bara, Zanzibar.

Vilevile kuundwa kwa programu ya kizazi chenye usawa Tanzania inayotekelezwa na wizara za kisekta kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Julai 2021/22 hadi Juni 2025/26 yenye mkakati madhubuti unaolenga kuleta mabadiliko ya ubora wa maisha ya wanawake na wasichana wa Kitanzania kwa kuimarisha haki na usawa wa kiuchumi pasipo kuwaacha nyuma wanaume na wavulana kwa kuwajengea uelewa ili waweze kushiriki kwenye maendeleo ya taifa.

Kuteuliwa kwa maofisa viungo kuanzia ngazi ya halmashauri, sekretarieti za mikoa na wizara wenye jukumu la kusimamia utekelezaji wa haki na usawa wa kiuchumi kwenye maeneo yao.

Jitihada zingine ni kukabiliana na vitendo vya ukatili, unyanyasaji na kuwainua wanawake wapate uwezo wa kiuchumi wa kuzihudumia familia zao.

Mathalani hadi kufikia mwaka 2022 Serikali imekopesha Sh bilioni 63.4 kwa vikundi 26,733 vya wanawake ambavyo vinajumuisha wanawake 938,802, vijana 10,741 na wenye ulemavu 1,270.

Rais Samia pia ameongeza idadi ya wanawake katika nafasi za maamuzi ambapo amekuwa akitoa fursa mbalimbali za uongozi kwa wanawake na kuimarisha uwiano katika teuzi anazozifanya kitendo ambacho kimeongeza idadi ya wanawake katika uongozi.

“Uteuzi wa wanawake  utaondoa dhana ya kuwa kuna nafasi ambazo wanawake hawawezi kuzishika,” alisema Rais Samia katika moja ya mikutano yake.

Itakumbukwa pia Rais Samia alielekeza kuundwa kwa kikosi kazi ambacho kilipokea maoni na mapendekezo kisha kupendekeza mabadiliko yanayoweza kufanywa kuelekea mwaka 2025.

Moja ya mambo ambayo yalifanyiwa kazi na kikosi kazi hicho ni suala la ushiriki wa wanawake na makundi maalumu katika siasa na demokrasia ya vyama vingi vya siasa pamoja na suala la rushwa na maadili katika siasa na uchaguzi.

Kumekuwa na ushiriki mdogo wa wanawake katika nafasi za uongozi na kutoa maamuzi kutokana na sababu mbalimbali kama vile mila kandamizi desturi na mitazamo hasi dhidi ya wanawake, kukosekana kwa mifumo rasmi na wezeshi ya kikatiba, kisheria na kisera na ukatili wa kijinsia hasa rushwa ya ngono.

Takwimu zinaonyesha idadi ya wabunge wanawake wa kuchaguliwa ni 24 kati ya 264 (asilimia 9.1) wakati viti maalumu ni 113 (asilimia 29) na kufanya idadi ya wabunge wanawake kufikia 141 (asilimia 37) kati ya wabunge wote 393.

Kwa upande wa madiwani wa kuchaguliwa wanawake ni 204 (asilimia 3.8) wakati wa viti maalumu ni 1,407 (asilimia 26.2) kati ya madiwani 5,353.

Katika Serikali za Mitaa wenyeviti wa vijiji wanawake ni 246 (asilimia 2.1) wakati wenyeviti wa vitongoji ni 4,171 kati ya 62,612.

Mapendekezo yaliyotolewa katika Kikosi Kazi yaliwezesha kupelekwa kwa miswada ya sheria za uchaguzi ambayo tayari imepitishwa na Bunge na sasa inasubiri kusainiwa na Rais Samia ili kuwa sheria kamili.

Katibu wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Jokate Mwegelo.

Katibu wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Jokate Mwegelo, anasema Rais Samia ni kielelezo cha mafanikio ambayo mwanamke anaweza kuyafikia na kuwataka wanawake waige mfano huo kwa kujitokeza kwa wingi kugombea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Anasema wameweka mikakati ya kuwasaidia wanawake watakaoteuliwa na chama kugombea nafasi mbalimbali na kuhakikisha wanashinda kwa kishindo.

“Tutahakikisha kama kuna mwanamke anagombea anapitishwa na chama na anakwenda kushinda, tutakesha kwenye mitaa, vijiji. Usijione mnyonge, usijione uko peke yako, jeshi la mama Samia litakushika mkono kuhakikisha kile unachokitazamia unakipata.

“Hii ni fursa yetu kinamama kugombea lakini akijitokeza mwenzetu anagombea tusimkatishe tamaa, tumpigie kura, tumtie moyo kwa sababu kadiri tunavyokuwa na viongozi wengi wanawake maendeleo ya haraka yanapatikana,” anasema Mwegelo.

Anavyotazamwa Kimataifa

Mratibu wa Masuala ya Jinsia wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya wanawake (UN Women), Karen Giath, anasema Tanzania imepiga hatua katika kuongeza usawa wa kijinsia chini ya uongozi wa Rais Samia.

Anasema miswada ya sheria za uchaguzi iliyopitishwa hivi karibuni itaongeza ushiriki wa wanawake na kuwapa nguvu ya kushiriki katika uchaguzi.

Mratibu huyo anasema mwaka huu wanawake bilioni 2 katika nchi 15 duniani Tanzania ikiwemo wanatarajia kufanya uchaguzi na kutaka waungwe mkono kuongeza ushiriki wao katika ngazi za maamuzi na kuhakikisha lengo namba tano la maendeleo endelevu linafakiwa.

Mchambuzi Mwandamizi wa Mipango kutoka Ubalozi wa Canada, Taslim Madhani, anasema Tanzania imepiga hatua katika usawa wa kijinsia hasa katika masuala ya elimu, uongozi na maamuzi lakini bado kuna kikwazo katika kufikia usawa wa kweli.

“Lazima tuwawezeshe wanawake na mabinti, tuendelee kupigania kesho tunayoitaka kwa mama zetu na mabinti zetu,” anasema Madhani.

Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP,) Lilian Liundi, anasema licha ya Serikali kuonyesha dhamira ya kuongeza usawa wa kijinsia lakini bado kuna changamoto nyingi.

Anashauri Serikali kupanga mikakati mipya ili kuwezesha wanawake na makundi mengine yaliyoko pembezoni kushiriki katika maendeleo ya taifa ambayo ni jumuishi na endelevu.

“Bado kuna changamoto nyingi zinazowakwamisha wanawake na makundi mengine yaliyoko pembezoni kushiriki katika maendeleo ya taifa ambayo ni jumuishi na endelevu.

“Safari ya kufikia usawa wa kijinsia maendeleo endelevu na jumuishi inahitaji kutafakari na kupanga mikakati mipya ili kuwa na jamii yenye usawa,” anasema Liundi.

Rais Samia anatajwa kuwa kinara wa haki na usawa kiuchumi katika utekelezaji wa jukwaa la kizazi chenye usawa ambalo lengo ni kuwezesha usawa wa wanawake na wanaume kushiriki kikamilifu kwenye masuala ya uchumi kwa ustawi wa familia na taifa kwa ujumla.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake 2024 inasema; Wekeza kwa wanawake kuharakisha maendeleo ya taifa na ustawi wa jamii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles