29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

Siasa za upinzani zilivyomjeruhi, kumponya Tendega

Na ARODIA PETER- DODOMA

NENO demokrasia asili yake ni Ugiriki, likiwa na maana ya utawala wawatu. 

Neno hilo lilianza kutumika kuanzia karne ya 5 kabla ya Kristo (KK) likielezea mtindo wa utawala uliotumika katika Ugiriki, kinyume cha aristokratía, yaani “utawala wa masharifu”.

Kwenye demokrasia, watu wa jamii fulani wanamchagua kiongozi wao ingawa kuna njia nyingi za kumchagua kiongozi husika. Hata hivyo mchakato kamili kwa kawaida huitwa kushiriki uchaguzi.

Kama hivi ndivyo, basi demokrasia katika nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania zina safari ndefu kufikia maana ya dhana nzima ya demokrasia.

Katika kitabu cha Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alichokiandika mwaka 1962 kiitwacho tujisahihishe, Mwalimu anasema: “Kosa jingine linalotokana na ubinafsi tunalifanya wakati wa kuchagua viongozi.

“Wakati mwingine hufanywa na wanachama, hufanywa na viongozi wenyewe na viongozi wa watu hawana budi watokane na watu bila hila, vitisho, rushwa, ujanja wa aina yoyote au hawaiwezi ile kazi wanayochaguliwa kuifanya” mwisho wa kunukuu.

Ni ukweli usiopingwa kwamba kwa vyovyote vile, Mwalimu katika maandishi yake anajaribu kuonya hila zozote zinazofanywa katika chaguzi kwamba si dhana halisi ya demokrasia.  

Katika makala haya, tutaangalia mafanikio na changamoto mbalimbali alizopitia Mbunge wa Viti Maalumu, Mkoa wa Iringa, Grace Tendega (Chadema), katika harakati zake za kushiriki na kugombea nafasi mbalimbali za kisiasa kwa njia ya demokrasia.

Katika mahojiano maalumu na MTANZANIA Jumapili, Tendega ambaye kitaaluma ni mwalimu mwenye Shahada ya Uzamili anasema siasa inahitaji uvumilivu, kujitoa ili kufikia malengo.

Kabla ya kuwa mbunge wa viti maalumu, Tendega amepitia changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi baada ya yeye kuamua kugombea ubunge kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo –Chadema, katika uchaguzi mdogo wa Kalenga, baada ya kufariki dunia aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Mahamudu Mgimwa (CCM) mwaka 2014.

Baada ya kifo hicho, ulifanyika uchaguzi mdogo ambao ulikuwa na ushindani mkali kati ya vyama viwili yaani Chadema na CCM huku vurugu, vitisho tuhuma za wizi wa kura vikishamiri.

Hata hivyo kabla ya kujiunga na Chadema na kushiriki uchaguzi huo mdogo, Tendega aliwahi kugombea ubunge katika jimbo hilo mwaka 2015 akiwakilisha Chama cha Jahazi Asilia.

Akizungumzia namna alivyojiunga na chama hicho kidogo cha siasa, anasema awali hakuwa amejiandaa kugombea lakini alitiwa moyo na Taasisi ya British Council, awali alishiriki mafunzo yao kuhusu mbinu na namna ya wanawake wanavyoweza kushiriki uchaguzi na kuingia kwenye uongozi wa kisiasa.

Anasema wakati British Council wanamshawishi kugombea mwaka 2015, muda wa kampeni ulikuwa umekaribia na vyama vikubwa kama CUF, CCM na Chadema tayari vilikwishapata wagombea wao. Hivyo ili kutimiza matakwa ya kisheria ya Tume ya Uchaguzi (NEC), inayotaka anayegombea sharti awakilishwe na chama cha siasa aliamua kujiunga na Jahazi Asilia.

Akielezea uchaguzi huo, Tendega anasema awali hakuna aliyedhani kwamba atatoa ushindani, lakini kadri kampeni zilivyopamba moto ndivyo watu walizidi kumuelewa akiwemo baba yake mzazi ambaye alikuwa anagombea udiwani kupitia  CCM wakati huo.

“Licha ya vurugu na mikwara ya hapa na pale ya CCM nilipata uungwaji mkono na wananchi walinipigia kura nyingi, na ninaamini nilishinda uchaguzi huo ingawa NEC haikunitangaza, badala yake ilimtangaza mgombea wa CCM na mimi nikawa mshindi wa pili huku nikiviacha nyuma vyama vingine shindani, anasema Tendega.

Aidha, harakati zake hazikuishia hapo kwani aligombea tena kwenye uchaguzi wa marudio na kushika nafasi ya pili. Mgombea wa CCM aliyeshinda kwenye uchaguzi huo ni Godfrey Mgimwa anayeongoza jimbo hilo hadi sasa.

Tendega anasema baada ya kumalizika uchaguzi huo wa marudio, alirudi kazini hata hivyo mwajiri wake wakati huo, Taasisi ya Elimu Mkoa wa Iringa alimtilia vikwazo na vitisho, kwa shinikizo la kutaka aache kazi.

Kutokana na shinikizo hilo Tendega anasema alilazimika kuachia kibarua chake cha utumishi wa umma na moja kwa moja aliendelea kushiriki siasa na baadaye alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake wa Chadema Taifa (BAWACHA).

Baada ya wadhifa huo, alianza kujenga mtandao wa wanawake wa Chadema kuanzia ngazi za chini na ndiyo sababu katika Uchaguzi Mkuu uliopita wa mwaka 2015 chama hicho kilikuwa na uungwaji mkono mkubwa wa wanawake kila kona nchini.

“Hiyo ndiyo ilikuwa ndoto na lengo langu mahsusi, kukipeleka chama kwa wanawake mijini na vijijini, na hilo tulifanikiwa kulitekeleza sawa sawa nikiwa na viongozi wenzangu wa BAWACHA.

“Kwa kiwango kikubwa hata mikutano ya kampeni katika uchaguzi mkuu uliopita zilitawaliwa kwa kiasi kikubwa na wanawake waliohamasika kushiriki siasa na mwamko huo umeendelea kuwa mkubwa licha ya kuwa tumezuiwa kufanya siasa na utawala uliopo madarakani.

“Hivi tunavyozungumza katika chaguzi zinazoendelea za ndani na nje ya chama, wanawake wanajitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali, jambo ambalo naona ndiyo ilikuwa ndoto yangu ya siku nyingi, kuona wanawake wanashiriki siasa bila woga. 

“Na hili linatupa moyo sana kwamba siku si nyingi vyombo vya maamuzi vitashikwa na wanawake ambao kwa hulka ni wachapazi, wabunifu na si mafisadi.

Anaongeza kusema;“Wewe mwandishi unaona, wanawake ndiyo wakopaji na warejeshaji wazuri wa mikopo katika taasisi za fedha na mikopo, kwa ujumla wanawake ni waaminifu na pale watakapokuwa wameingia na kushiriki katika vyombo vya maamuzi kama Bunge na katika halmashauri mbalimbali nchini mchango wao utakuwa mkubwa kwa Taifa,”anasisitiza Tendega.

Mwanasiasa huyo anatoa wito kwa wanawake nchini kote bila kujali vyama vyao kuendelea kushiriki siasa kwani ndiyo watapata nafasi za kuleta mabadiliko ya kisera na kisheria kwa manufaa ya jamii ya nzima.

Aidha, amewakumbusha wanawake wa Chadema kutobweteka na nafasi walizonazo katika baraza hilo, bali wajiandae kugombea nafasi za ndani ya chama hicho.

Ingawa yeye hakuweka wazi nafasi anayotarajia kugombea, lakini amesema anafikilia kugombea moja ya nafasi za juu kabisa za chama hicho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles