29.4 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

Marekani inavyoiathiri Iran

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

KWA muda sasa, Serikali ya Marekani imeshikilia uamuzi wake wa kuliwekea vikwazo vya kiuchumi Taifa la Iran. Historia inaonyesha kuwa uhusiano wa nchi hizo kushirikiana ulianza kuvurugika mwaka 1979.

Wadukuzi wa siasa za kimataifa wanajua hiyo ni baada ya wanafunzi kuvamia Ubalozi wa Marekani nchini Iran na kuwashikilia mateka watu waliokuwamo ubalozini humo.

Haijasahaulika kuwa Marekani imewahi kuitaja Israel katika orodha ya maadui zake watatu, sambamba na Urusi, China na Korea Kaskazini. Hiyo ni baada ya kuihusisha Iran na mashambulizi ya mwaka 2012 na 2014 dhidi ya benki za Marekani.

Kubwa zaidi, Marekani haifurahishwi na kitendo cha Iran kusimamia msimamo wake wa kuendelea kuzalisha nyuklia, ingawa taifa hilo la Kiarabu linasisitiza kuwa ni kwa matumizi ya kawaida, ikiwamo kuzalisha umeme.

Hilo haliingii akilini Marekani na washirika wake wa Ulaya, nyuklia nchini Iran ni kwa matumizi ya uzalishaji wa silaha hatari za kivita na si vinginevyo.

Hata hivyo, licha ya viongozi wa Iran kusisitiza kuwa hawababaishwi na vikwazo vya Marekani, ukweli ni kwamba uchumi wa Taifa hilo la Asia umekuwa katika hali mbaya tangu msuguano wake na mabepari hao ulipoanza.

Wachambuzi wa siasa hawaoni namna uchumi wa Iran unaweza kuthibitisha kuwa haujaathiriwa na kile kinachoendelea kati ya mataifa hayo.

Hebu tujikumbushe kilichotokea mwaka 2015, ambapo Rais wao, Hassan Rouhani, alikubali kushirikiana na Marekani na nchi nyingine tano katika mpango wa kudhibiti shughuli za uzalishaji wa nyuklia.

“Mwaka mmoja baada ya makubaliano hayo yaliyoifanya Iran iondoshewe vikwazo, uchumi wa Iran ulipanda kwa asilimia 12.3,” inaeleza ripoti ya Benki Kuu ya Iran. 

Ikiwa ni sehemu ya unufaikaji wa kutokuwapo kwa vikwazo, mwanzoni mwa mwaka jana, Iran ilikuwa na uhakika wa kuzalisha mapipa ya mafuta milioni 3.8 kwa siku, huku ikiuza mapipa milioni 2.3.

Marekani ilipotangaza kurejesha vikwazo vyake mwaka jana, ikizilenga sekta za nishati, meli na fedha, lilikuwa pigo kubwa kwa Iran kwani uwekezaji wa nje ulishuka, hivyo kutikisa uwezo wa nchi hiyo kusafirisha mafuta.

Si tu kampuni za Marekani ziliweka ngumu kufanya biashara na Iran, pia ilizipa onyo kampuni za nchi nyingine zilizokuwa na ukaribu wa kibiashara na Taifa hilo.

Bahati mbaya kwa Iran ni kwamba sehemu kubwa ya mafuta waliyokuwa wakiuza yalikuwa yakinunuliwa na mataifa nane ambayo ni China, India, Japan, Korea Kusini, Taiwan, Uturuki, Ugiriki na Italia.

Wakati mwezi huu ukiwa wa mwisho kwa nchi hizo kuachana na Iran, amri iliyotolewa na Marekani, Ugiriki, Italia na Taiwan zilishajiweka kando mapema.

“Hali hiyo imesababisha Iran ipoteze kiasi kikubwa cha fedha kwani kufikia Machi, mwaka huu, usafirishaji wake wa mafuta ulikuwa mapipa milioni 1.1 tu kwa siku,” inaeleza ripoti ya Shirika la Kimataifa la Nishati lenye makao makuu yake mjini Washington (SVB Energy International).

Wakati nchi hizo tatu zikijitoa kabisa, Iran imepoteza pia wateja wake wakubwa, China na India, ambao licha ya kusisitiza kuwa wataendelea kuwa wateja, sasa ununuaji wao wa mafuta umeshuka na kufikia kati ya asilimia 39 na 47.

“Matokeo ya uamuzi huo ni kulishuhudia pato la ndani la Iran likishuka kwa asilimia 3.9,” inasema ripoti ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF). 

Inaelezwa kuwa kutokanana na hali hiyo, Serikali ya Iran imepoteza si chini ya Dola bilioni 10 katika sehemu ya vyanzo vyake vya mapato.

Kama hiyo haitoshi, ripoti ya IMF inaonyesha kuwa kufikia mwishoni mwa mwezi uliopita, vikwazo vya Marekani na marafiki zake vingeufanya uchumi wa Iran ushuke kwa asilimia 6 kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Kutokana na majanga hayo, thamani ya fedha ya Iran (rial), imeshuka kwa takribani asilimia 60 dhidi ya Dola ya Marekani, hiyo ni kwa mujibu wa mitandao ya kubadilisha fedha za kigeni.

Kufikia Aprili 30, mwaka huu, dola moja ilikuwa sawa na rial 143,000 na kutokana na hali hiyo mbaya kiuchumi, wananchi wengi wa Iran wanataka fedha za kigeni, wakiamini ndiyo ya kuaminika linapokuja suala la kuweka akiba.

Aidha, kuyumba huko hakujawaacha salama wananchi wa Iran, ambapo gharama za maisha zimepanda kwa kasi, kubwa ikiwa ni mfumuko wa bei ya vyakula kwa asilimi 31 kufikia mwaka jana, tofauti na ilivyokuwa mwaka juzi ilikuwa asilimia 9.

“(Mfumuko wa bei) unaweza kufikia asilimia 37 au zaidi mwaka huu ikiwa usafirishaji wa mafuta utaendelea kushuka,” inasisitiza ripoti ya IMF.

Ukiacha bidhaa zinazotoka nje, kushuka kwa thamani ya rial kumewafanya wananchi wa Iran washindwe hata kumudu zile zinazozalishwa nchini humo.

Mfano mzuri katika hilo bei ya nyama ya ng’ombe, ikielezwa kuwa kwa kipindi cha miezi 12 iliyopita, imepanda kwa asilimia 57, hivyo ni ngumu kwa wengi kumudu.

“Pia, ndani ya kipindi hicho, bei ya maziwa na mayai nayo imepanda kwa asilimia 37, kama ilivyo kwa mboga za majani asilimia 47,” inasema ripoti ya Shirika la Takwimu la Iran. 

Kukabiliana na hali hiyo, Serikali ya Iran imepiga marufuku kusafirisha mifugo nje ya nchi, wakiamini inaweza kuwa hatua nzuri ya kutokomeza tatizo la ongezeko la bei.

Ni changamoto kubwa kwani wananchi wengi wanataka fedha za kigeni, hivyo wamekuwa wakitumia njia mbalimbali kuuza mifugo yao nje ya nchi. 

Nje ya mkakati huo, pia Serikali ina mpango wa kuanzisha kadi maalumu kwa watu masikini, ambao ni zaidi ya milioni mbili,  ili waweze kuzitumia kupata nyama na mahitaji mengine ya msingi, zikiwamo huduma za afya, ambazo gharama zake zimepanda kwa asilimia 20 kuanzia mwaka jana tu.

Huku Irani ikiendelea kuitunishia misuli Marekani na mataifa ya Magharibi, wachambuzi wa siasa na wataalamu wa uchumi wanaamini mvutano huo unawaumiza zaidi wananchi.

“Uongozi wa Iran unajiamini lakini kilichopo ni kuwatesa wananchi juu ya kupanda kwa gharama za bidhaa kunakotokana na vikwazo vya kibiashara,” anasema Nozar Hashemzadeh, profesa wa uchumi Chuo Kikuu cha Radford nchini Marekani.

“Asilimia 99 ya wananchi wa Iran wanataka amani na Marekani, hivyo mazungumzo yangekuwa na faida kubwa kuliko vikwazo.”

Aidha, Rais wa Iran, Rouhani, amewahi kulizungumzia hilo lakini kwa bahati mbaya hakuonekana kukubaliana na hoja ya profesa Hashemzadeh. “Watu wa Iran hawatafyata kwa presha ya Serikali ya Marekani,”anasema Rais huyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles