23.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 8, 2024

Contact us: [email protected]

Siasa za BBI zawekwa pembeni kuomboleza kifo cha Moi

Na ISIJI DOMINIC 

WAKENYA, wana Afrika Mashariki, Waafrika na dunia kwa ujumla waliamshwa kwa habari za kushutukiza, Jumanne ya Februari 4, baada ya Rais Uhuru Kenyatta akiwa safarini kuelekea Marekani kutangaza kifo cha Rais mstaafu wa awamu ya pili, Daniel Toroitich Arap Moi. 

Mzee Moi aliyekuwa na umri wa miaka 95, alifariki akiwa karibu na familia yake wakati anapata matibabu katika Hospitali ya Nairobi jijini Nairobi. Kutokana na cheo kikubwa alichokuwa anakishikilia enzi za uhai wake, msiba wake umekuwa wa kitaifa na mazishi yake yatapewa heshima yote ya kitaifa ikisimamiwa na serikali. 

Kwa siku tatu kuanzia jana, mwili wa rais huyo mstaafu ambao ulikuwa umehifadhiwa katika Chumba cha Maiti cha Lee, umewekwa kwenye majengo ya Bunge ili kuwapa fursa wananchi kutoa heshima zao za mwisho. 

Misa ya kitaifa kumuombea marehemu imepangwa kufanyika Jumanne katika Uwanja wa Nyayo kabla mwili kusafirishwa nyumbani kwake Kabarak katika kaunti ya Nakuru kwa mazishi siku inayofuata. 

Malkia Elizabeth II akihutubia katika dhifa ya kitaifa pamoja na Rais Moi, katika ziara ya siku nne ya Malkia nchini Kenya mwaka 1983.

Imekuwa kawaida kwa wanasiasa kutumia siku za mwishoni mwa wiki kuandaa mikutano wanayodai ni kuhamasisha umma kuhusu ripoti ya jopo kazi iliyopachikwa jina la Building Bridges Initiative (BBI).  

Ni ripoti ambayo licha ya kila mwanasiasa kuikubali inaleta taswira mpya ya Kenya, ni dhahiri wamekuwa wakitofautiana namna inavyopaswa kutekelezwa na kipi kiongezwe kabla ya kuanda ripoti ya mwisho ya BBI. 

Wanasiasa wanaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto, wanamshutumu kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, wakidai amegeuza mikutano ya kuhamisha BBI kuwa ya kisiasa na kujifanyia kampeni kuelekea uchaguzi mkuu 2022. 

Mkutano wa kwanza wa BBI ulifanyika kaunti ya Kisii na kuhudhuriwa na wanasiasa wengi kutoka vyama mbalimbali vinavyomuunga mkono Raila huku ule wa pili uliofanyika kaunti ya Kakamega ukishuhudia kiongozi wa ANC, Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford-Kenya, Moses Wetangula wakihudhuria. 

Awali wawili hao walitarajiwa kuwapo kwenye mkutano tofauti uliopangwa kufanyika Mumias lakini ukatibuliwa na Jeshi la Polisi. Mudavadi na Wetangula waliruhusiwa kuhutubia halaiki ya watu waliojitokesha kwenye Uwanja wa Bukhungu na kutangaza hadharani kuungo mkono BBI. 

Mkutano wa BBI ulihamia kaunti ya Mombasa na safari hii wanasiasa wanaomuunga mkono Ruto wakiongozwa na Kiongozi wa Waliowengi Bunge la Seneti, Kipchumba Murkomen, walihudhuria na alipopewa nafasi kuongea alitangaza kuunga mkono BBI na pia kufanyika kwa kura ya maoni.       

Baada ya Mombasa, mkutano wa BBI ulihamia kaunti ya Kitui ambapo kuliibuka vurugu baada ya Mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria, anayemuunga mkono Ruto kulazimisha kwenda kukaa jukwaa kuu. Katika mkutano huo, wanasiasa hao wa mrengo wa Tangatanga hawakuruhusiwa kuhutubia. 

Mzee Moi akikutana na Waziri Mkuu wa India, Indira Gandhi, uwanja wa ndege Nairobi Septemba 1981.

Wikendi hii, mkutano wa BBI ulikuwa ufanyike kaunti ya Makueni lakini ukafutwa kufuatia kifo cha Mzee Moi kwa sababu isingekuwa jambo la busara taifa linaomboleza huku wanasiasa wengine mawazo yao yapo kwenye siasa za BBI. 

Seneta wa Kitui, Enoch Wambua, alisema waandaji waliamua kufuta mkutano huo ili kuwa pamoja na Seneta wa Baringo, Gideon Moi, ambaye amempoteza baba yake.

“Tulipanga mkutano wa kuhamasisha BBI maeneo ya Wote kaunti ya Makueni ambapo Seneta wa Baringo alitakiwa kuwa miongoni mwa wageni katika tukio hilo na kutokana na kile ambacho kimetokea na kwa heshima ya Mzee Moi, tumeshauriana na kiongozi wetu, Kalonzo Musyoko na kukubaliana tuhairishe mkutano huo hadi tarehe nyingine,” alisema Wambua. 

Seneta huyo wa Kitui aliwataka wanasiasa wenzake kusitisha majadiliano yote ya kisiasa hadi atakapozikwa rais mstaafu.

Naye Seneta wa Makueni, Mutula Kilonzo Jr, alisisitiza umuhimu wa siasa kuwekwa pembeni na familia kupewa muda kumuomboleza mzee wa boma.

“Ni maombi yetu tuache shughuli zote za siasa, tumeamua kuhairisha mkutano wetu eneo la Wote ili wiki hii itumike kumuomboleza Mzee Moi na hivyo familia iwe angalau na amani na utulivu hadi tutakapompumzisha mzee,” alisema Seneta Mutula. 

MOI ALIVYOTEUA BARAZA LAKE LA KWANZA LA MAWAZIRI

Utawala wa Mzee Moi mara mwingi uliwashangaza marafiki zake wa karibu na kupigwa na butwaa uamuzi wake. Wengi waliokuwa karibu na Rais Mstaafu Moi walidhani mawazo yao ndiyo yatakua maamuzi yake. 

Daniel arap Moi akiwa pembeni ya Rais mteule Mwai Kibaki wakati wa hafla ya kumwapisha, Desemba 2002, na huu ndio ulikuwa mwisho wa utawala wa miaka 24 ya Moi madarakani

Mfano mzuri ni namna alivyoteua baraza lake la kwanza la mawaziri miezi chache baada ya kuapishwa kuwa rais wa pili wa Kenya, kufuatia kifo cha Hayati Mzee Jomo Kenyatta Agosti 22, 1978 akiwa usingizini katika Ikulu ya jiji la Mombasa. 

Moi ambaye baadhi ya wandani wa Mzee Kenyatta walimuona atakuwa tu rais wa muda alianza mkakati wa kulisuka baraza lake la mawaziri ili kuendana na mfumo wake wa siasa. 

Jumanne ya Novemba 28, 1979 ikiwa ni wiki chache baada ya kuapishwa, Moi alijitokeza katika Ikulu ya Nakuru na orodha yake mpya ya mawaziri watakaohudumu katika serikali yake. Hata hivyo, haikuwa kazi rahisi uteuzi wa mawaziri kwa sababu kiongozi huyu alikuwa na jukumu la kuhakikisha usawa katika baraza lake litakalojumuisha wanaomkosoa, marafiki na makundi yaliyotengwa ili kuepuka lawama. 

Hivyo, Moi anayefahamika kama ‘profesa wa siasa’ aliwapa kazi makundi matatu tofauti kupendekeza mawaziri huku kila kundi likiamini ndilo pekee linalofanya jukumu hilo muhimu. Historia inaonyesha kundi la kwanza liliundwa na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu, Charles Njonjo na waziri msaidizi, G.G. Kariuki. 

Kundi la pili liliundwa na aliyekuwa Makamu Rais, Mwai Kibaki na Katibu Mkuu J.A. Gethenji huku kundi la tatu likijumuisha Nicholas Biwott ambaye ni mshirika wa karibu wa muda mrefu wa Moi. Ile wikendi kabla ya kutaja baraza la mawaziri, Moi alikutana na makundi yote matatu katika nyakati tofauti ili kujadili orodha waliopendekeza kabla ya kurudi Ikulu ya Nakuru kutafakari orodha ya mwisho. 

Moi ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha KANU, alifanya mkutano wa siri na aliyekuwa mkuu wa usalama, James Kanyotu, kujadili kwa kina orodha zote tatu. Wakati wanajadili, Kanyotu aliwaagiza vijana wake kupitia mafaili ya kila aliyependekezwa kwa ajili ya usalama. 

Zoezi hilo lilipomalizika, Moi aliwaita Ikulu Kibaki, Njonjo na Biwott na kuanza kusoma orodha ya wateuli wa wizara mbalimbali na wote watatu walibaki na mshangao namna baadhi ya majina waliopendekeza kupuuzwa.   

Akichoma moto shehena kubwa ya pembe za ndovu zenye thamani ya dola milioni 3 ili kuonesha msimamo wake juu ya vita dhidi ya ujangili mwaka 1989.

Moi aliongeza wizara 12 mpya na miongoni mwa wizara hizo ni Nishati, Viwanda, Uchukuzi na Mawasiliano, na Mazingira na Maliasili. Baadhi ya waliokwemo kwenye orodha ya kwanza ya mawaziri ni Henry Kosgei (Nishati), Jonathan arap Ng’eno (Maji), Robert Ouko (Mambo ya Nje), Joseph Kamotho (Elimu ya Juu) na Elijah Mwangale (Kazi). Changamoto ilikuwa kwa majina matatu ambayo makundi hayo matatu yalipendekeza kwa nafasi ya mawaziri katika Ofisi ya Rais. Kila kundi kilipendekeza jina lake wakiamini hiyo ni nafasi nyeti. 

Hata hivyo, Moi alichanganya orodho hiyo na kuhakikisha kila kiongozi wa kundi amewakilishwa. Biwott na G.G Kariuki walitajwa mawaziri katika ofisi ya rais huku Kibaki akibaki makamu wa rais na kuongezewa jukumu lingine la waziri wa fedha, na Njonjo akiwa mwanasheria mkuu.

Wanahistoria wamebaini takribani asilimia 35 ya baraza la kwanza la mawaziri la Moi liliundwa na Wakikuyu na Wajaluo ni asilimia 10 huku asilimia 55 iliyobaki ilitengwa kwa makabila mengine. 

HISTORIA ‘FIMBO YA NYAYO’ 

Hayati Mzee Kenyatta kila alipokuwa akitembea alikuwa hakosi mkia wa ng’ombe, naye marehemu Mzee Moi ilikuwa ni rungu maarufu Fimbo ya Nyayo. 

Fimbo hiyo iliyokuwa ishara ya mamlaka, uongozi na umoja wa taifa ilitengenezwa kwa kutumia pembe ya ndovu na dhahabu, Moi naye hakukosa kutembea nayo katika shughuli zozote ndani na nje ya nchi.

Ofisa Habari wa Mzee Moi kwa zaidi ya miaka 40, Lee Njiru, anakumbuka namna mwaka 1981 rais huyo mstaafu alivyokataa kujitokeza katika shughuli ya Malkia nchini Australia bila fimbo yake baada ya kuvunjika vipande viwili.

Anasema fimbo mpya ilibidi itumwe Australia kabla ya kuanza mkutano wa Jumuiya ya Madola uliofanyika jijini Melbourne.

Fimbo hiyo ilivunjika Los Angeles nchini Marekani wakati Moi alipotembelea baada ya kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa jijini New York.

“Peter Rotich (msaidizi wa Moi) alilazimika kuleta fimbo mpya wakati Moi akiwa bado Honolulu, Hawaii kabla hajaelekea Australia kwa sababu Mzee alitaka kusalimia watu kutumia fimbo hiyo,” alisema Njiru.

Umaarufu wa Fimbo ya Nyayo ulisababisha Kwaya wa Kariakor Friends kuitungia wimbo ikisifu fimbo hiyo kumsaidia Moi kuongoza nchi kuhakikisha amani inadumishwa, uchumi unadumishwa na mapambano dhidi ya ukabila na ugaidi. 

Aidha, fimbo hiyo ilikuwa maarufu hadi ikalazimika kutumika katika nyuma ya noti ya KSh 20 na 100 huku picha ya Moi ikiwa mbele. Fimbo hiyo inaaminika ilikuwa ishara ya maono ya Moi kwa Wakenya vijana katika miaka ya 1970 na 80 kusimama na kufika kilele cha mafanikio yao chini ya utawala wake. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles