24.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 8, 2021

Kinana, Makamba wana jambo

Na GRACE SHITUNDU-DAR ES SALAAM

KIZA kinene kimetawala kuhusu kuhojiwa kwa makatibu wakuu wawili wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana.

Hadi kufikia jana, si Kinana wala Makamba aliyefika kuhojiwa na Kamati ya Maadili na Nidhamu ya CCM tofauti na kauli ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula anayeongoza kamati hiyo, kwamba makada wake wote watatu waliotakiwa kuhojiwa kwa makosa mbalimbali ya kimaadili wengehojiwa ndani ya wiki hii.

Hadi sasa kamati hiyo imemuhoji Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani, Bernard Membe  ambaye aliwekwa kwenye kundi moja la kuhojiwa na Kinana na Makamba. 

Yusuf Makamba

Kushindwa kufika huko kwa Kinana na Makamba kuliibua taarifa nyingine mpya jana kwamba viongozi hao wastaafu wamegoma kufika kuhojiwa.

Taarifa hizo ambazo zilianza kusambaa mitandao ya kijamii kabla ya MTANZANIA Jumapili kuzifuatilia kwa watu wa karibu na viongozi hao, zilikwenda mbali na hata kudai kuwa viongozi hao wa zamani wa CCM walikuwa tayari hata ikiwezekana kuondoka ndani ya chama hicho.

Uamuzi wa kutaka makada hao wahojiwe ulifikiwa Desemba 13 mwaka jana, baada ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) kuketi na kuagiza waitwe baada ya kutuhumiwa kwa makosa mbalimbali ya kimaadili, msingi ukiwa ni mgogoro kati yao na chama hicho pamoja na mwenyekiti wao.

Taarifa ambazo MTANZANIA Jumapili limezipata, zinaeleza kuwa Kinana na Makamba ambao inasemekana kwamba wote wako nchini, wamegoma kuhojiwa kwa kile ambacho kinaelezwa hawako tayari kudhalilishwa.

Inaelezwa kuwa hoja kubwa ni kwamba hawawezi kuhojiwa ama kudhalilishwa na watu ambao wameingia CCM juzi juzi.

Kwamba watakuwa tayari kuzungumza iwapo kitaitwa kikao kitakachowahusisha viongozi wakuu wa zamani, wakiwamo wenyeviti na makamu wenyeviti wastaafu wa chama hicho.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, ingawa hawajaandika barua ya kuondoka CCM, inaelezwa kama ikibidi watafanya hivyo na hasa ikiwa kikao hicho cha viongozi wastaafu hakitaitwa.

MTANZANIA Jumapili iliwasiliana na mzee Makamba kwa njia ya simu ya kiganjani ambapo licha ya kusema kuwa yupo Lushoto mkoani Tanga, lakini alikataa kuzungumza chochote kuhusu kuhojiwa kwake.

Tofauti na kauli yake ya siku za nyuma kwamba akiitwa atafurahi na atakuwa tayari kwenda kuhojiwa, jana Makamba alionekana kuwa mkali kidogo huku akiongea kwa hamaki. 

“Nimekwambia mimi sina shida na waandishi kwa sasa, mimi nipo Lushoto huku, hizo habari sizitaki, kama nitakuwa nina shida ya waandishi nitawatafuta mwenyewe, kwa sasa andikeni habari za mvua,” alisema Makamba.

Mwandishi alipomuuliza iwapo kama mvua hizo ndizo zilizomzuia kutofika Dodoma kuhojiwa na Kamati ya Nidhamu na Maadili au amekataa kuhojiwa kama taarifa nyingine zinavyoeleza, alijibu; “Nimesema sitaki waandishi kwa sasa, niacheni nipumzike.”

Juhudi za kumpata Kinana ziligonga mwamba baada ya MTANZANIA Jumapili kudokezwa kuwa ana mawasiliano tofauti na yale yanayofahamika kwa sasa.

MANGULA

Jana baada ya kuhutubia kongamano la miaka 43 ya kuzaliwa kwa CCM, alipofuatwa na waandishi wa habari, Mangula alikataa kuzungumzia kuhusu kuhojiwa kwa Kinana na Makamba.

Hata katika kongamano hilo Mangula alijikita kuzungumzia mambo mengine tofauti na hilo, kuhusu wagombea, rushwa na uchaguzi.

MTANZANIA Jumapili liliwasiliana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole kuhusu siku ambayo Kinana na Makamba watahojiwa ambapo alisema michakato yote baada ya uamuzi wa NEC ni ya ndani.

“Utaratibu wa chama baada ya Halmashauri Kuu ya Taifa kukutana Desemba mwaka jana Mwanza na kuagiza makada watatu waitwe kuhojiwa, baada ya pale yote yatakayoendelea ni michakato ya ndani.

“Halafu baada ya chama kuamua mimi (Polepole) ndiye nitakayekuja kueleza hatma yao,” alisema Polepole. 

Kwa siku mbili mfululizo hadi jana, waandishi wa habari walipiga kambi ziliko ofisi za CCM mkoani Dodoma, lakini hakuna yeyote kati ya Makamba wala Kinana aliyefika kuhojiwa.

Kwa upande wake, Membe baada ya kuhojiwa kwa takribani saa tano Alhamisi wiki hii, aliahidi kufichua kidogo kidogo alichohojiwa na kushauri ndani ya kamati hiyo.

Juzi Membe alionekana kuanza kutekeleza ahadi hiyo kwa kufichua kidogo kidogo muhtasari wa kile alichohojiwa na kushauri.

Kupitia ujumbe wake aliouandika kwenye mtandao wa Twitter, mwanasiasa huyo alieleza maeneo matatu pasipo kuyafafanua ambayo  yalitumika kujibu hoja na kutoa ushauri kwa kamati hiyo ambayo ni haki, uchaguzi na uhusiano wa kimataifa.

Zaidi alisema alijibu hoja za kamati hiyo bila kuyumba wala kuyumbishwa.

“Nimerejea salama kutoka Dodoma. Namshukuru Mungu kwa ujasiri alionipa wa kwenda mbele ya Kamati ya Maadili na Nidhamu na kujibu hoja mbalimbali bila woga, bila kuyumba wala kuyumbishwa. Naamini wameupokea ushauri nilioutoa kuhusu uhuru, haki, uchaguzi na uhusiano wa kimataifa,” alieleza Membe kupitia ujumbe wake huo.

Alhamisi baada ya kuhojiwa, Membe ambaye alionekana mchangamfu na mwenye furaha,  alisema safari hiyo ya kwenda Dodoma ilikuwa ni ya manufaa makubwa sana kwake, chama na kwa taifa, akiahidi mengine yatakuwa yanapatikana kidogo kidogo baada ya kushiba. 

TAARIFA MPYA

MTANZANIA Jumapili liliwasiliana na Membe kufahamu yaliyojiri baada ya kuhojiwa na hasa baada ya kuweka ahadi ya kutoa taarifa kidogo kidogo ambapo alijibu kwa kifupi; “Tusubiri wazee wawili wahojiwe kwanza.”

Wakati Membe akijibu hivyo, taarifa nyingine zinaeleza kuwa mahojiano kati yake na kamati hiyo hayakuwa mepesi kama watu wengi wanavyodhani.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, pamoja na Membe kusema alishauri kamati hiyo, lakini naye alibanwa kwa hoja kali kuhusu tuhuma zinazomkabili.

KILICHOWAPONZA 

Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ilishauri kuhojiwa kwa makada hao baada ya kuvuja kwa sauti zao katika mitandao ya kijamii, wakifanya mawasiliano kwa njia ya simu huku wakisikika kukizungumzia vibaya chama hicho na Mwenyekiti wake, Rais Dk. John Magufuli. 

Sauti hizo ziliwahusishaa pia wanachama wengine; Nape Nnauye, January Makamba na Wiliam Ngeleja ambao walipewa onyo baada ya kuomba radhi kwa Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Magufuli na kusamehewa. 

Hii ilikuwa ni tofauti kwa Membe, Kinana na Makamba ambao wao hawakuchukua hatua ya kuomba msamaha au kuzungumzia chochote kuhusu sauti hizo.

Tofauti na Membe, kabla ya kuvuja sauti, makatibu wakuu hao wa wastaafu waliandika taarifa kwa Baraza la Wazee wa CCM wakilalamikia mambo mbalimbali, ikiwamo kudhalilishwa kwa mambo ya uongo na mtu anayejitambulisha kama mwanaharakati na mtetezi wa Serikali.

Katika taarifa hiyo, viongozi hao walidai kuwa wamezingatia Katiba ya CCM toleo la mwaka 2017 ibara ya 122, na kwamba waliwasilisha maombi yao wakiwasihi wazee hao wa chama watumie busara zao kushughulikia jambo hilo ambalo walidai kuwa linaelekea kuhatarisha umoja, mshikamano na utulivu ndani na nje ya chama.

Pia walidai kuwa wametafakari kwa kina kabla ya kutoa taarifa kuhusu kile walichodai kuwa ni uzushi na kwamba mara kwa mara Watanzania wamekuwa wakijiuliza kwamba mtu huyo anatumwa na nani.

ADHABU 

Endapo makada hao watatu watakutwa na hatia, kuna adhabu ambazo watakumbana nazo.

Kwa mujibu wa kanuni za uongozi na maadili za CCM toleo la 2017, kuna adhabu tatu kwa wanachama wanaofika mbele ya kamati hiyo na kutiwa hatiani.

Katika kanuni hizo kifungu cha 5(2) kinasema; wanachama wanaovunja maadili ya chama kama yalivyoainishwa katika Katiba ya CCM na kanuni za CCM wanachukuliwa hatua za kuwarekebisha na kama itashindikana kuwarekebisha ni kuwaondoa katika chama au katika uongozi.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
168,538FollowersFollow
527,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles