23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Usirekebishe ndoa kwa kutengeneza tatizo

HESHIMA ni kitu kikubwa kwa mwanamume yeyote. Mwanamume anapojisikia hana heshima tena anaweza kufanya chochote kama namna ya kujihami. Katika simulizi la George na mkewe Neema, tunajifunza kwamba George alitumia pombe kama namna ya kutatua tatizo la kujiona hana thamani kwa mke wake, familia yake, majirani, ndugu na marafiki wengine. Ingawa hakuwa mnywaji mwanzoni,  kuna namna kwenye pombe kunamkutanisha na watu wanaomwelewa.

Walevi wenzake wanampa faraja ambayo watu wengine kazini kwake, mtaani kwake, kwenye familia yake, kanisani, wameshindwa kumpa.

Unaweza kumlaumu kwa kunywa pombe na kutokutumia akili, lakini ukweli ni kwamba moyo wake una majeraha ya mfululizo wa shutuma kutoka kwa mke wake Neema. Kama mke mwenye matarajio yake, Neema alitamani kuona George anafanya kama wanavyofanya wanaume wengine. Neema alitamani kuona George anapambana na maisha kutunza familia yake.

Pamoja na nia yake njema, Neema hakujua namna nzuri ya kumshauri George. Wanaume wengi waliolelewa kwenye mfumo dume uliokomaa hawapendi kuambiwa cha kufanya hasa kama kuna namna wamekosea. Kichwa cha mwanamume kama George kinatafsiri ushauri kama  dharau. 

Bahati mbaya, baada ya Neema kushindwa kumsaidia George, anaamua kutumia watu wengine akiamini wakizungumza na George watamsaidia. Lakini kinyume na matarajio yake, kitendo cha Neema kumsema mume wake kwa ndugu wa pande zote mbili, kinamfanya George alijisikie kudharauliwa. Kuanzia hapo George alianza kujiona kama mtu asiye na heshima. Hakuelewa inakuwaje mke wake anakuwa mwepesi kumsema kwa kila mtu? George akakata tamaa na maisha na kuamua kutumia pombe kama namna ya ‘kupunguza mawazo’.

Pombe ikawa ufumbuzi uliozalisha tatizo jingine. Mke wake kuona mume wake amekuwa mlevi, anaanza kumtukana mbele ya watoto, anamsema kwa wazazi, ndugu, jamaa na marafiki. Ingawa yeye anadhani kwa kufanya hivyo anamsaidia George kujirekebisha, kwenye macho ya George kitendo hicho kinaendelea kusisitiza mawazo yake kwamba mke wake anamdhalilisha kwa makusudi. Tunachokiona hapa ni kwamba unapotafuta ufumbuzi wa tatizo kwenye ndoa yako, jitahidi ufumbuzi huo usizalishe tatizo.

Ingawa ni kweli George ni mlevi na tusingependa alewe, lakini ulevi unaonekana kumsaidia kujisikia mwanamume tena. Marafiki anaokutana nao kilabuni wanamsaidia kujiona hajapungukiwa kama watu wengine wanavyofanya. Katika kulithibitisha hilo, mazungumzo yangu na George hayakumlaumu hata kidogo.

Nilijitahidi kuonesha kumwelewa. Nilipofanya hivyo na George akaniamini, akageuka kuwa rafiki yangu. Nilijaribu kumweleza kwa nini ninafikiri hata mimi ningekuwa kwenye mazingira yake huenda ningekuwa mlevi kuliko yeye, alilia machozi.

Nikamweleza, hata ingekuwa mimi, mwanamke akinisema mbele za watoto wangu, akanisema kwa ndugu zangu, huenda ningekuwa na hasira kuliko alizonazo yeye, George alinyamaza kimya. Kwa mara ya kwanza, George akajisikia amepata rafiki anayemwelewa. Tukawa marafiki wa karibu. 

Urafiki wangu na George ulilenga kumsaidia kurudisha uanaume wake aliohisi ameanza kuupoteza. Nilimweleza kwa nini ninaamini yeye ni mtu makini. Sikumwambia kwa lengo la kumfurahisha. Nilimaanisha. Nilimkumbusha kwamba ninamfahamu vizuri sana.

George wa leo sio George wa zamani ninayemfahamu mimi. Nilimweleza mambo mengi aliyoyafanya kabla hajaanza kunywa pombe. Nilimpongeza kwa uamuzi wake wa kuamua kwenda kusoma. George hakuficha furaha yake kuona ninaunga mkono uamuzi wake. George akawa mtu wa kunitafuta mara kwa mara. Urafiki wetu ulikolea.

Pamoja na sababu nyingine, kubwa ni kule kufahamu ninamwelewa. Ingawa sikuwahi kumshauri kuacha pombe, George aliacha pombe mwenyewe. Urafiki wetu ukawa mbadala wa pombe. 

Wakati huo huo, niliongea na mke wake. Nilifikiri Neema alihitaji kubadili namna anavyoongea na George. Nilimtazamisha kwamba hakuwa na sababu ya kumdhalilisha mume wake hata kama ni kweli kuna makosa anafanya.

Neema alihitaji kuelewa hulka ya mwanamume wa aina ya George. Unapomkemea hutatui tatizo. Neema hakunielewa kirahisi. Lakini baada ya majadiliano ya muda mrefu, na kuona kuwa George ameacha pombe, Neema alianza kuelewa mchango wake kwenye tatizo analoliona kwa George. 

Tukakubadiliana kwamba kuanzia wakati huo, Neema hataongea anapokuwa na hasira. Badala ya kuwaambia watu matatizo ya ndoa yake, Neema aelewe kwamba ndoa ni ya kwake yeye na mume wake.

Hakuna mtu mwingine anaweza kunusuru ndoa yao. Nilimtazamisha kwamba pamoja na ulevi wake, bado George ni mume wake. Badala ya kumshutumu, tulizungumza namna gani anaweza kubadilisha lugha yake kwa mume wake. Kwa nini asianze kutambua mazuri aliyonayo mume wake? Kwa nini asiwe mwepesi kuomba msamaha kwa makosa aliyowahi kufanya? Tulielewana. 

Baada ya majuma kadhaa George akawa mtu mwingine. Hanywi tena pombe. Hatumii tena fedha bila  mipango. Furaha ya ndoa yao imerudi. Kwa nini? Wote wawili, George na mke wake Neema wamejifunza namna bora ya kutatua matatizo yao bila kutengeneza matatizo mengine. Umejifunza kitu? Kakifanyie kazi.  

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles