23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Shule nyingine yaungua moto Manyara

Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Manyara, Francis Massawe.
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Manyara, Francis Massawe.

Na BEATRICE MOSSES – MANYARA

MATUKIO ya kuteketea kwa moto mabweni ya wavulana katika shule za sekondari zilizoko Kanda ya Kaskazini yanazidi kushika kasi.

Juzi, moto uliteketeza bweni la Shule ya Sekondari ya Wavulana Aldersgate, iliyopo wilayani Babati, Mkoa wa Manyara.

Kuteketea kwa bweni hilo ni mwendelezo wa matukio ya aina hiyo baada ya shule kadhaa kuteketea katika mikoa ya Arusha na Manyara.

Tukio la hivi karibuni ni la Shule ya Sekondari Mulbadaw iliyopo wilayani Hanang, ambayo mabweni yake yaliteketea kwa moto na kuharibu mali zote za wanafunzi shuleni hapo.

Katika tukio la Shule ya Sekondari ya Wavulana Aldersgate, moto ulitokea juzi saa tatu usiku wakati wanafunzi wakiwa madarasani.

Hata hivyo, taarifa zilizopatikana kutoka kwa walimu na wanafunzi ambao hawakutaka kutaja majina yao, zinasema inawezekana chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme.

Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Manyara, Francis Massawe, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema moto huo ulizimwa na kikosi cha zimamoto baada ya muda mfupi tangu ulipoanza kuwaka.

“Hata hivyo, tutawahoji walinzi wawili wa shule hiyo pamoja na patroni wa shule hiyo kwani hao ndio tunaoamini watatoa picha halisi ya tukio hilo,” alisema Kamanda Masawe.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule hiyo, Dillo Fredson, alisema tukio hilo limewasikitisha kwa kuwa limetokea katika kipindi ambacho baadhi ya wanafunzi wanajiandaa na mtihani wa taifa.

“Kuhusu thamani ya mali zilizoungua, bado tunaendelea kufanya uhakiki ili tuweze kuzijua na baadaye tutakaa na bodi ya shule kuona tunafanyaje,” alisema Mwalimu Fredson.

Ili kukabiliana na matukio ya moto, alisema wanaangalia uwezekano wa kubadilisha mfumo wa umeme kwa kufunga nyaya za sola ambazo haziwezi kusababisha madhara yoyote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles