Na Veronica Romwald – Dar es Salaam
MABALOZI wa nchi 17 za Bara la Afrika waliopo nchini, wameridhishwa na huduma za kisasa za kiuchunguzi, upasuaji na matibabu dhidi ya maradhi ya moyo zinazofanywa na Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).
Wamesema sasa wapo tayari kutibiwa katika taasisi hiyo na kwamba wataenda kuzishawishi nchi zao zianze kuleta wananchi wake kutibiwa maradhi hayo nchini.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa mabalozi hao, Balozi wa Zimbabwe nchini, Edzai Chimonyo, alipozungumza kwa niaba ya wenzake walipofanya ziara kwenye taasisi hiyo hivi karibuni.
“Kwa kweli tumeridhika na jinsi Serikali ya Tanzania ilivyofanya uwekezaji katika taasisi hii, tupo tayari kuanza kutibiwa hapa na tutazishawishi nchi zetu zianze kuleta wananchi wake kupata matibabu hapa JKCI.
“Kwa sababu uwekezaji uliofanywa ni mkubwa, tumejionea vifaa zikiwamo mashine za kisasa na za kiwango cha juu. Kwa msingi huu ni vizuri tutibiwe Tanzania kuliko kwenda India maana huduma zinazotolewa hapa tunaona ni sawa na zile zile tunazozifuata huko,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi, alisema hadi sasa wameshahudumia watu zaidi ya 50,000 ambapo 6,500 walilazwa kwa matibabu katika taasisi hiyo.
“Tumeweza kuwafanyia upasuaji na uchunguzi zaidi ya watu 800, tumeshawafanyia upasuaji watoto wawili wa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Septemba 8, mwaka huu tutawafanyia wengine watatu,” alisema.
Profesa Janabi alisema pia wanatarajia kuwafanyia upasuaji watoto zaidi ya 70 kwa kushirikiana na wataalamu wenzao wa nchini Marekani na Italia.
“Kuna watoto wapatao 500 wanasubiri huduma ya upasuaji. Tunaanza na hawa 70 Agosti 9 hadi 19, mwaka huu, tutatumia njia ya upasuaji pasipo kufungua kifua… kwa siku tutaweza kuwafanyia watoto 11 hadi 12.
“Nawasihi watu wajitokeze kuchangia damu maana ni changamoto kwetu ili tufanyie upasuaji huu, matibabu ni gharama kubwa ukimpeleka mgonjwa nje ya nchi.
“Kwa mfano ile betri tuliyoweka kwa yule mtu mzima mweye miaka zaidi ya 60, tumemfanyia upasuaji kwa Sh milioni 30 na hiyo ni gharama ya ununuzi wa mashine pekee, angetibiwa nje tungetumia zaidi ya Sh milioni 100,” alisema.
Mabalozi waliotembelea taasisi hiyo ni wa nchi za Kenya, Msumbiji, Afrika Kusini, Sudan, Rwanda, Misri, Zimbabwe, Zambia na Malawi.