27.3 C
Dar es Salaam
Monday, December 4, 2023

Contact us: [email protected]

Shule 110 Ludewa kupata vitabu vya mitaala mipya

Na Mwandishi Wetu, Njombe

Shule 110 za Msingi wilayani Ludewa mkoani Njombe zinatarajiwa kununuliwa vitabu mbalimbali vya mitaala mipya ili kukuza kiwango cha elimu na kuondokana na changamoto ya wanafunzi kumaliza shule bila ya kutumia vitabu ambapo wakati mwengine hulazimika kupakua mtandaoni.

Ahadi hiyo imetolewa juzi na mbunge wa jimbo la Ludewa, Joseph Kamonga wakati alipokua akizungumza na walimu wakuu wa shule za misingi zilizopo jimboni humo ambapo walijadili changamoto mbalimbali zinazowakabili zikiwemo za kielimu ili kuweza kuzitafutia ufumbuzi.

Wakizungumza katika mkutano huo walimu walieleza changamoto zinazowakabili na kupelekea kushika nafasi ya mwisho ikiwemo kutokuwa na vitabu vya kufundishia, wazazi kuwashawishi watoto kufanya vibaya mitihani yao,utoro uliokithiri kwa wanafunzi.

Suzana Kibena ni mwalimu mkuu wa shule ya msingi Ikalo ambaye alinieleza mbunge huyo changamoto ya vitabu na kudai kuwa kwa miaka mitatu mfululizo darasa la nne na la saba wamekuwa wakifanya mitihani ya taifa kwa kusoma bila kutumia kitabu cha sayansi.

Kibena alisema serikali imekuwa ikiwasisitiza kupakua vitabu hivyo mitandaoni kitu ambacho kwa upande wao inawawia vigumu kutokana na kufanya hivyo kunahitaji gharama na wao hawana fedha za kupakulia vitabu hivyo.

“Tunaambiwa tupakue vitabu mtandaoni na kuvitumia kwa wanafunzi ilihali vitendea kazi hatuna, kama kopyuta, printer na vinginevyo na ukisema uende stationary nako kunahitajika hela ya kufanya hivyo, sisi tunaitoa wapi?,” alihoji Kibena.

Akizungumza baada ya kusikiliza changamoto hizo mbunge huyo alisema kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa Halmashauri, Wise Mgina pamoja na walimu kuweka mkazo katika suala la kutokuwepo kwa vitabu ambapo aliahidi kununua vitabu hivyo.

“Changamoto zenu nimezipokea na ninaahidi kushirikiana nanyi katika kuzitatua ili muweze kufundishia katika mazingira mazuri na watoto wa wapiga kura wangu waweze kupata elimu bora na itakayowawezesha kufanya vizuri na kukuza kiwango cha elimu wilayani kwetu nitanunua vitabu pia nitalifuatilia swala hili wizara ya elimu ili kujua kwanini vitabu hivyo havipo,”alisema Kamonga.

Naye Afisa Elimu wa Shule za Msingi wilayani Ludewa,  Daniel John, alimuomba mbunge huyo kuzungumza na wananchi wake waache tabia vya kuwanyanyasa na kuwadhalilisha walimu kwakuwa walimu hao wanafanya kazi kubwa sana ya kuwafundisha watoto wao.

“Nazungumza haya kwa uchungu Sana! kuna baadhi ya wananchi wamekuwa wakiwazalilisha walimu wangu na kuwanyanyasa pasipo sababu ya msingi, walimu tunawafundisha watoto wao katika mazingira magumu halafu bado na wazazi wanatuongezea matatizo, tafadhari sana Mheshimiwa mbunge naomba uzungumze na wananchi wako waache kuninyanyasia walimu wangu,” alisema John.

Aidha kwa upande wa mwenyekiti wa chama cha walimu Tanzania (CWT) Mkoa wa Njombe, Shabani Ambindwile, akimuwakilisha katibu mkuu CWT taifa amewasisitiza walimu wakuu hao kuwa na ushirikiano na walimu wao na kujenga upendo kati yao ili kuhakikisha shule zao zinafanya vyema.

Ambindwile alisema pamoja na kujenga upendo kati yao pia wanapaswa kutowavumilia walimu wazembe kwani kutokana na uzembe wao nipelekea kuleta matokeo hasi katika shule zao halafu yanapikuja matokeo mabaya analaumiwa mwalimu mkuu.

“Mimi wakati nafundisha nikiona mwalimu mzembe nilikuwa namtupa kwenye stadi za kazi huko kutamfanya ajifunze na kuongeza juhudi katika kufundishia, japo sina maana nanyi mkafanye hivi Ila hakikisheni hamuwafumbii macho walimu wa aina hiyo,” alisema Ambindwile.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles