25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

SHEIKH KHALIFA KHAMIS AKAMATWA NA POLISI

NA Asha Bani


MWENYEKITI wa Taasisi ya Imamu Bukhary, Sheikh Khalifa Khamis, amekamatwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na kuhojiwa kwa saa tisa.

Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, Sheikh Khalifa alifika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam jana saa nne asubuhi na kuhojiwa kwa muda mrefu, huku ikiwa haifahamiki hasa sababu za kushikiliwa kwake.

Taarifa zilizolifikia MTANZANI jana jioni zilidai kuwa polisi walikuwa wamepanga kumchukua sheikh huyo kwa ajili ya kwenda kupekua nyumbani kwake. Hata hivyo hadi tunakwenda mtamboni saa mbili usiku alikua bado anashikiliwa polisi.

Kwa nyakati tofauti jana Sheikh Khalifa mwenyewe alizungumza na gazeti hili kwa simu na kudai kuwa alipofika kituoni alielezwa na polisi kwamba ameitwa kuhojiwa kuhusu tuhuma za uchochezi.

Alisema kwamba alihojiwa kuhusu kuunga mkono kauli ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, juu ya masheikh wa uamsho na hatua yake ya kuwataka waumini wa dini ya kiislamu kuungana kutetea haki za Waislamu waliopo katika magereza mbalimbali nchini.

“Wameniuliza mambo ya kumuunga mkono Lowassa na pia waliniuliza kwanini niliwataka Waislamu nchini kuungana kuwatetea Waislamu waliopo kizuizini kwa makosa ya kubambikwa.

“Hadi sasa niko hapa polisi bado nasubiri ni nini kitaendela kama wataniachia au watanibakisha hapa hatujajua,” alisema.

Msemaji wa Jeshi Polisi

Akizungumza na gazeti hili kwa simu jana jioni, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Barnabas Mwakalukwa, alisema kwa muda huo alikua hana taarifa za kuhojiwa kwa sheikh huyo.

“Mimi hadi sasa katika dawati langu sina taarifa ya kuhojiwa kwa sheikh Khalifa ila ninachojua kama kaitwa Central Polisi mwenye himaya yake ni RPC wa Ilala,’’alisema Mwakalukwa.

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala (RPC) Salum Hamduni saa 12 jioni, alisema hana taarifa zozote kuhusu kukamatwa kiongozi huyo wa dini.

Alichosema Sheikh Khalifa

Baadhi ya mambo aliyoyasema Sheikh Khalifa katika mkutano wake na waandishi wa habari jumapili ya wiki hii.

“Tunaiomba Serikali iweke wazi kwa nini hairuhusiwi kwa sheikh au mtu yeyote aliyewekwa ndani gerezani  kuonwa na zaidi ya mtu mmoja hadi siku 14 zipite, yaani akija mkewe au ndugu yake leo kuonana naye  ipite siku 14 ndio aje ndugu yake mwingine kumuona hayo mambo hayapo na hayamo katika sheria.

“Tunampongeza Lowassa kwa kuona kwamba jamii miongoni mwa Watanzania inadhaliliska  na haitendewi haki na kama yeye aliyasema maneno haya kwa kutafuta faida za kisiasa hayo ni maneno yake lakini aliyoyasema ni haki na kweli,” alisema sheikh Khalifa.

Kauli ya Lowassa 

Akiwa katika futari iliyoandaliwa na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara, Lowassa alitaka serikali iharakishe kesi za masheikh wa uamsho na kama baadhi yao hawana makosa waachiwe huru.

Alisema wakati wa kampeni za mwaka 2015, alitoa ahadi nyingi ikiwa ni pamoja na kupitia upya mikataba ya madini, pamoja na kuwaachia masheikh wa uamsho hivyo kama Rais John Dk. Magufuli amefanyia kazi la madini, afanye hivyo pia kwa masheikh hao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles