POLISI WAMVURUGA LISSU

0
462

*Wamkamata uwanja wa ndege dar baada ya kuruka kihunzi cha dodoma

Na Asha Bani – dar es salaam


SIKU moja tangu Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), kung’ang’ania ndani ya Mahakama ya Wilaya ya Dodoma ili kukwepa kukamatwa na polisi, jana alikamatwa akiwa Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Lissu anadaiwa kukamatwa kutokana na mkutano wake na waandishi wa habari alioufanya hivi karibuni, ambao aliutumia kuzungumza mambo mbalimbali kuhusu Serikali na viongozi wake yanayodaiwa kuwa ya uchochezi.

Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene, alithibitisha kuwa Lissu alikamatwa jana akiwa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere akielekea Kigali nchini Rwanda kuhudhuria mkutano wa wanasheria wa Afrika Mashariki.

“Amekamatwa kweli saa 12 jioni akiwa anaelekea Kigali, hadi sasa hivi hatujui wamempeleka kituo gani cha polisi, tunaendelea kumtafuta,” alisema Makene.

Mbali na Makene, jana majira ya jioni kwenye mitandao ya kijamii kulikuwa na ujumbe mfupi uliodaiwa kuandikwa na Lissu.

Ujumbe huo ulisema: “Wajumbe  wa halmashauri, nipo uwanja wa ndege najiandaa kuelekea Kigali kwenye kikao cha Halmashauri ya EALS kinachoanza kesho (leo). Watu waliojitambulisha kama maafisa kutoka ofisi ya ZCO Dar es Salaam, wamekuja kunikamata na kunipeleka Kituo Kikuu cha Polisi.”

Hata hivyo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam, Lucas Mkondya, aliliambia MTANZANIA kuwa leo atatolea ufafanuzi suala hilo la kukamatwa kwa Lissu.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni, alisema taarifa hizo hazijafika kwenye meza yake.

 

TUKIO LA DODOMA

Juzi, Lissu aling’ang’ania ndani ya Mahakama ya Wilaya ya Dodoma kwa saa saba akidai kuwa amepata taarifa za kuwapo kwa polisi waliovalia kiraia waliotumwa kumkamata.

Alipoulizwa na gazeti hili sababu za kung’ang’ania mahakamani, alisema kuwa hakuna maana yoyote kisheria, bali ameamua kufanya hivyo kwa sababu ndiyo sehemu salama kwa nchi zinazoheshimu utawala wa sheria duniani kote.

“Nimeamua kung’ang’ania mle ndani kwa kuwa ni salama zaidi… mbali na mahakama, kwingine ambako ningeweza kwenda ambako ni salama ni msikitini au kanisani, kwenye nchi zinazoheshimu demokrasia na utawala bora, hawawezi kukukamata,” alisema Lissu.

Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alisema dunia nzima kama utakuwa umekimbilia mahakamani, ni sehemu salama, huwezi kukamatwa na askari.

Alisema aliingia mahakamani hapo saa 2 asubuhi kuwatetea wateja wake, ambao ni walimu walioamua kukishtaki Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Wilaya ya Dodoma na kulazimika kukaa humo kwa saa saba.

Lissu alisema baada ya kumalizika kwa kesi hiyo saa 8:23 mchana, alilazimika kubaki ndani ya mahakama kutokana na taarifa aliyodai kupewa ya kukamatwa na askari waliokuwa nje.

Alisema kuwa alilazimika muda wote kuwa na mazungumzo na viongozi wa Chadema waliofika mahakamani hapo baada ya kupata taarifa za kukamatwa kwake.

Hali hiyo ilizua taharuki na kumfanya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa kufika mahakamani hapo saa 10:04 jioni akiwa na mlinzi wake na kumtaka Lissu aondoke ndani ya mahakama hiyo kwani hakuna atakayemkamata.

MATUKIO YA LISSU KUKAMATWA

Agosti 2016, Lissu alikamatwa na polisi muda mfupi baada ya kuhutubia mkutano wa hadhara katika mji mdogo wa Ikungi mkoani Singida.

Februari 2017, alikamatwa akiwa nje ya Bunge mjini Dodoma.

Machi 6, alikamatwa tena akiwa kwenye maeneo ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mara baada ya kumaliza kusikiliza kesi yake ya uchochezi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here