24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Shehena ya sukari ya magendo yakamatwa

kayomboNA KOKU DAVID, DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imefanikiwa kukamata mashua katika Bandari ya Lindi iliyokuwa na bidhaa mbalimbali za magendo zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 159.361.

Miongoni mwa bidhaa zilizokuwemo katika mashua hiyo ni pamoja na sukari mifuko 3,725 yenye thamani ya Sh. milioni 127 iliyoingizwa nchini kutoka Brazil, huku ikiwa imehifadhiwa katika mifuko yenye nembo ya mchele.

Akizungumza jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo, alisema ukamataji wa mashua imesaidia watuhumiwa kutozwa kodi ya Sh  milioni 10.500.

“Tunatarajia bidhaa zote ambazo hazikuwa na nyaraka zitatozwa kodi ya Sh milioni 19.529.

“Katika kuhakikisha tunaziba mianya yote ya upotevu wa mapato, TRA imeimarisha doria ukanda wa Bahari ya Hindi, Ziwa Victoria na mipaka yote nchi kwa kutumia vikosi vyetu maalumu vya kuzuia magendo (Fast Team) pamoja na  kushirikiana na Jeshi la Polisi,” alisema Kayombo.

Alisema mashua hiyo ambayo ilikamatwa na maofisa wa TRA, Februari 3 mwaka huu ilikuwa imebeba betri katoni 50, mchele mifuko 3,087, mafuta ya kula madumu 80, majokofu manne ya mtumba, baiskeli nne za mtumba na katoni 20 za amira.

Alisema wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara haramu wameanza kutumia Bandari ya Lindi, baada ya kuimarika udhibiti wa mapato katika sehemu nyingine ambazo walikuwa wakizitumia.

Katika hatua nyingine, Kayombo alisema mamlaka hiyo, imefanikiwa kukamata bidhaa mbalimbali za magendo zenye thamani ya Sh milioni 19.2 katika eneo la Mbweni, jijini Dar es Salaam ambazo kodi yake iliyotakiwa kulipiwa ni zaidi ya Sh milioni 13.

Alizitaja bidhaa hizo, kuwa ni madumu ya mafuta ya kula 578, jola 33 za kanga, mifuko 14 ya sukari na mifuko minne ya mchele, huku watu sita wakishikiliwa na polisi kwa uchunguzi zaidi.

Alisema katika Bandari ya Dar es Salaam, mamlaka hiyo, kwa kushirikiana na polisi wamefanikiwa kukamata jahazi la Takbiri lenye namba za usajili Z 875 likiwa na lita 19,700 za mafuta ya dizeli.

“Januari 17, mwaka huu tulikamata majahazi matatu katika eneo la Kigombe mkoani Tanga, yakiwa na bidhaa za magendo yenye thamani ya Sh milioni 99.5, juhudi za oparesheni hii ni kutokomeza bidhaa za magendo.

“Kwa kushirikiana na polisi tumeunda kanda maalumu  ya kupambana na magendo katika maeneo ya Mbweni, Msasani, Kunduchi na Kigamboni,” alisema.

Alisema majahazi hayo yalikuwa yamebeba magunia 275 ya sukari, magunia 284 ya mchele, galoni 390 za lita 20 za mafuta ya kula, matairi 14 ya gari yaliyotumika, lola 76 za nyaya za kuzuia mbu, betri katoni tatu, rangi za kupuliza katoni 30, biskuti katoni 48, jokofu moja la mtumba, matairi 47 ya mtumba na ovener moja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles