26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, January 27, 2022

Shangwe, vilio vyatawala matokeo ya uchaguzi DRC

KINSHASA, DRC

WAKATI maelfu ya wafuasi wa Rais mteule, Felix Tshisekedi, wakiendelea kushangilia ushindi wao kwa nderemo na vifijo, hali kwa upande mwingine wa kambi zilizoshindwa si nzuri huku baadhi ya watu wakipoteza maisha na wengine kujeruhiwa.


Hali hiyo imetokea saa chache baada ya Tume ya Uchaguzi nchini DRC (CENI), kumtangaza Tshisekedi kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais nchini humo.


Kwa mujibu wa vyanzo vya habari kutoka vyombo vya dola nchini humo, baadhi ya maeneo yamekumbwa na machafuko ambayo yamesababisha watu 11 kupoteza maisha na wengine kadhaa kujeruhiwa.


Idhaa ya Kiswahili ya Redio Ufaransa imesema, watu sita wamepoteza maisha katika mji wa Kikwit uliopo katika Mkoa wa Kwilu, Mashariki mwa Jiji la Kinshasa na wengine wengi kujeruhiwa kwa mujibu wa mashuhuda, huku Jeshi la Polisi nchini humo likipoteza maofisa wawili.


Vyanzo vya habari kutoka Mkoa wa Kikwit zinasema maofisa wawili wa polisi na raia wanne ndio waliopoteza maisha katika makabiliano ya kupinga matokeo hayo.


Katika mji wa Kimbanseke, watu wawili wameuawa kwa kupigwa risasi na wengine 22 wamejeruhiwa wakati wa makabiliano kati ya wafuasi wa Martin Fayulu na wale wa Tshisekedi.


Katika miji kadhaa ya nchi hiyo kulishuhudiwa maandamano ya furaha na makabiliano kati ya vikosi vya usalama na watu wenye hasira wakipinga matokeo hayo ya uchaguzi. Watu wengine10 wamejeruhiwa katika makabiliano hayo.
Umoja wa Afrika umetoa wito kwa wananchi wa DRC kuwa na utulivu na kuwataka wagombea ambao hawakuridhishwa na matokeo hayo kutumia utaratibu wa sheria kwa amani kwa kuwasilisha madai yao mbele ya Mahakama ya Katiba.


Wakati huo, viongozi wa Jumuiya za kimataifa wamesisitiza kuzungumzia lakini kwa uangalifu mkubwa matokeo ya uchaguzi wa urais katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, yaliyotangazwa mapema juzi huku wengi wakichagua kutompongeza kiongozi wa upinzani aliyetangazwa mshindi na kutoa mwito wa mivutano yote kumalizwa kwa amani.

Matokeo ya awali yalipeleka ushindi kwa kiongozi wa upinzani, Tshisekedi. Lakini mgombea mwenzake ambaye pia anatokea upinzani, Martin Fayulu, mara baada ya kutangazwa matokeo hayo alilalamikia mchezo mchafu na kuyaita matokeo hayo mapinduzi ya uchaguzi.


Jana, Marekani ilitoa tamko la kutaka ufafanuzi zaidi wa matokeo hayo, huku ikiwapongeza wapiga kura wa taifa hilo kwa ujasiri waliouonyesha.
Naibu Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Robert Palladino, amesema kupitia taarifa ya wizara hiyo kwamba, baada ya Tume ya Uchaguzi ya CENI kutangaza matokeo hayo ya awali, Marekani itahitaji ufafanuzi zaidi juu ya maswali yaliyoibuliwa kuhusiana na kuhesabiwa kura. Lakini pia amewataka wadau wote kuwa watulivu wakati mchakato huo ukiendelea.


Msemaji wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, Stephane Dujarric, amesema kiongozi huyo amezitaka pande zote kujiepusha na machafuko na kusaka suluhu ya mivutano ya uchaguzi kwa amani.


Katibu mkuu ameelezea matumaini yake kwamba, tume huru ya uchaguzi, Serikali, Mahakama ya Katiba, vyama vya siasa na asasi za kiraia kwa pamoja watasalia kwenye misingi ya majukumu yao ili kuendeleza utulivu na demokrasia.


Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Faki Mahamat, naye akitolea mwito kama huo. Nao Umoja wa Ulaya umesema unasubiri uamuzi utakaotolewa na waangalizi wa uchaguzi.


Msemaji wa EU, Maja Kocijancic, amesema umoja huo kwa wakati huu unawaomba wanasiasa nchini humo kujiepusha na aina yoyote ya machafuko na kuruhusu mchakato wa kidemokrasia kuendelea. Ufaransa hata hivyo, iliyapinga wazi matokeo hayo.


CENi ilimtangaza Tshisekedi kushinda kwa asilimia 38.57 ya kura, akimpiku Martin Fayulu aliyepata asilimia 34.8. Ramazani Shadary, mteule wa Rais Joseph Kabila, aliambulia asilimia 23.8 tu ya kura.


Matokeo ya uchaguzi wa wabunge ambao pia ulifanyika sambamba na huu wa urais, yalitarajiwa kutangazwa jana na wabunge wengi wa Chama cha Kabila wamejitangaza kushinda viti vya ubunge.


Chaguzi mbili zilizopita za mwaka 2006 na 2001 ambazo Rais Kabila alishinda ziligubikwa na umwagikaji mkubwa wa damu na wengi wanahofia kurudia kwa machafuko hayo iwapo matokeo ya uchaguzi yatakosa uhalali.


Tayari polisi wawili na raia wawili wameuawa jana na wengine 10 kujeruhiwa, baada ya kuzuka maandamano katika mji wa Magharibi mwa Congo, Kikwit ambako ni ngome ya Fayulu.


Katika hatua nyingine, Kanisa Katoliki nchini humo limesema matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa hayafanani na yale yaliyoonwa na maelfu ya waangalizi wake.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
176,866FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles