23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Viwanda vinne kubangua korosho

FLORENCE SANAWA, MTWARA

VIWANDA vinne vya kubangua korosho vimeingia mkataba na Serikali kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kwa ajili ya kubangua korosho zaidi ya tani 7,500 mkoani Mtwara.

Mkataba huo umefikiwa jana baada ya Serikali kufanya mazungumzo na viwanda hivyo ambapo hadi sasa imekusanya zaidi ya tani 200,000.


Akizungumza katika kikao na wamiliki wa viwanda hivyo, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, alisema Serikali ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha kuwa korosho zinabanguliwa hapa hapa nchini.
 

Aliongeza kuwa ubanguaji wa korosho hapa nchini mbali na kuongeza ajira nchini bado Serikali itaingiza mapato kupitia korosho zilizobanguliwa kuliko kuuza korosho ghafi nje ya nchi.

“Unajua zoezi la ubanguaji lilishaanza katika Shirika letu la Viwanda vidogo vidogo (Sido) ambapo wameajiri wafanyakazi 155 mara baada ya kuingia mkataba na bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko ambapo tunaamini watazingatia ubora wa kubangua korosho.

“Tunatamani kuona korosho zetu zikiuzwa duniani kwa jina la nchi yetu kwa kuwa sisi ndio wazalishaji wa korosho bora duniani, tuna kila namna ya kuboresha na kuongeza thamani zao hili kutokana na uwezo mkubwa wa kuchangia pato la taifa.”

“Awali Serikali ilichukua Kiwanda cha Buko kilichopo mkoani Lindi lakini sasa kitaitwa Kiwanda cha Ubanguaji Lindi baada ya ukarabati, kinatarajiwa kuanza kazi hivi karibuni lakini pia Serikali inachukua kiwanda cha Agrofocus cha Newala, lakini bado tuko kwenye mazungumzo na kampuni nyingine ambazo zitaongezeka hivi karibuni,” alisema Hasunga.

Kwa upande wake Ofisa Mawasiliano na Mahusiano wa Kiwanda cha Export Trading Group, Frank Mtui, alisema wamepokea korosho kwenye viwanda vyao vitatu ambapo katika kiwanda cha Micronix Newala watabangua tani 2,400, Micronix Mtwara tani 1,200 na Korosho Afrika tani 2,400.

“Viwanda vyetu vyote vitatu vina uwezo wa kubangua tani 12,500  kwa sababu tumeshachelewa tutaweza kubangua tani 10,000 tu, hivi sasa tumechukua chache kwa kuwa mikataba iko wazi tunatarajia tukimaliza tutachukua nyingine.

“Unajua ukisimama bila kubangua korosho kwa muda mredu ni madhara zaidi, lakini kitendo cha Serikali kutuletea korosho kwetu imesaidia hata wafanyakazi wa kiwanda chetu kupata ajira,” alisema Mtui.

Naye Meneja Uzalishaji wa Kiwanda cha Hawte Investment Limited, Saadat Abdul, alisema kiwanda hicho kinatarajia kuanza ubanguaji mwezi huu ambapo wafanyakazi wote watarejea kazini.

“Sisi tuna wafanyakazi 700 ambao ndio walikuwa wakifanya ubanguaji wa korosho, lakini walienda likizo kwa muda sasa upatikanaji wa korosho hizi utarejesha wafanyakazi wote kazini ambapo tunatarajia kufungua kiwanda Januari 17 na uwezo wetu kwa mwaka ni tani 1,500 ingawa tunatarajia kuongeza uzalishaji hivi karibuni,” alisema Abdul.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles