SHAKA AWATAKA VIJANA KUJIUNGA NA UJASIRIAMALI

0
777

Na Mwandishi Wetu -Kigoma

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umesema vijana wanaoendelea kulalamika bila kufanya kazi, kujituma na kutoa jasho la uchapakazi watakawia sana kufikia malengo chanya na kujikwamua kiuchumi.

Hayo yameelezwa jana mjini hapa na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, alipotembelea kikundi cha ujasiriamali cha Kata ya Mwandiga wilayani Kigoma.

Alisema hakuna njia mbadala na ya mkato ya kujikwamua kimaisha na hali ngumu yoyote ya umasikini bila kijana mwenyewe kuamua kujishughulisha na kuzalisha mali hatimaye waweze kujitegemea.

Aliwasifu wanakikundi kwa kujikusanya, kupanga mipango na mikakati ya mradi wa kufyatua matofali, kuzalisha sabuni na kuwa na kikundi cha Vicoba kwa mtindo wa kuweka na kukopa pia kununua hisa.

“Vijana wengi huwa wanawaza, wanapanga na kutaka kutenda  hawatendi, kikundi hiki ni makini na kimeamua kuonyesha kwa vitendo jinsi kilivyopania kujikwamua na umasikini wa vipato hatimaye kujijenga kiuchumi,” alisema Shaka.

Kutokana na hali hiyo, aliwahimiza watendaji wa Halmashauri ya Kigoma kuona haja ya kukipa umuhimu kikundi hicho kwa kuwapatia wataalamu, mitaji na vyanzo vya fedha.

“Vijana mnakawia, wakati ni huu jiungeni pamoja kupitia vikundi vya uzalishaji kwa lengo la kuacha utegemezi badala yake mjiajiri na kujitegemea kiuchumi,” alisema.

Kaimu Katibu Mkuu huyo pia alizindua kikundi kwenye Kata ya Kalinzi, kutazama maendeleo ya mradi wa ujenzi wa tangi la maji hatimaye akazungumza na wanachama katika kikao cha ndani katika Kata ya Mgaraganza mkoani hapa.

Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Kigoma, Zainabu Katimba (CCM), aliahidi kusaidia kikundi hicho kwa kuwapatia vyerehani vitano ili kuongeza mradi mwingine wa ushonaji kwa kinadada wa kikundi hicho.

“Ingelikuwa vijana wote wa Kigoma na Tanzania wanapitisha maamuzi mazito kama kikundi hiki, nchi yetu isingekuwa na vijana wanaolalamika, wanaosaka ajira au kulalamikia umasikini,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here